Afrika Kusini:Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia Afrika Kusini katika janga la moto
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Afrika Kusini iko tayari kushirikiana na mamlaka ili kutoa msaada kwa wale walioathirika moto katika jengo lenye makazi ya watu wengi mjini Johanesburg nchini Afrika Kusini. Katika taarifa iliyotolewa usiku wa tarehe 31 Agosti 2023 kwa saa za New York Marekani, na Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa: “Katibu Mkuu amesikitishwa sana na taarifa za moto huo ulioripotiwa kupoteza maisha ya zaidi ya watu 70 tarehe 31 Agosti huko Johannesburg, Afrika Kusini.”
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres kupitia msemaji wake anasema: "Katika wakati huu wa huzuni na majonzi makubwa, anatoa salamu zake za pole za dhati kwa familia za waathirika na kwa Serikali na watu wa Afrika Kusini. Anawatakia ahueni ya haraka majeruhi.” Na wakati huo ho Wasemaji mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya ndani ya Afrika Kusini na vya kimataifa vinadai jengo la ghorofa tano lililoungua moto lilikuwa moja ya majengo ndani ya Johannesburg ambayo yana vamiwa na watu na kuweka makazi yao.