Mikataba Mitatu Mahususi Ya Uwekezaji Katika Bandari ya Dar Es Salaam, Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki hafla ya utiaji saini wa Mikataba Mahsusi 3 ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam tarehe 22 Oktoba, 2023 Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma, amesema Mikataba ya Uwekezaji wa Bandari iliyosainiwa imezingatia maoni yaliyotolewa kupitia makundi mbalimbali ya kijamii, pamoja na sheria na taratibu za nchi. Tarehe 22 Oktoba 2023 Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia halfa ya utiaji saini mikataba mitatu ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Serikali na Kampuni ya DP World ya Dubai iliyowakilishwa na Sultan Ahmed Bin Sullayem, Mkurugenzi mkuu wa DP World Dubai. Mikataba hii iliyosainiwa ni matokeo ya ya makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Tanzania na Mamlaka ya Dubai ambao wameridhia mahitaji na matakwa ya Tanzania kama yalivyoainishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa. DP World Dubai itaanza kuwekeza kiasi cha dola za kimarekani milioni 250 na kiwango hiki kinaweza kuongezeka hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 1.
Mkataba huu utatekelezwa katika kipindi cha miaka 30, watalipa kodi zote za Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi. Wamewekewa “perfomance key indicators” na watafanyiwa tathmini kila baada ya miaka mitano. Serikali ya Tanzania itachukua asilimia 60% ya mapato au faida itakayopatikana. Serikali ya Tanzania ina uwezo wa kuvunja mkataba wakati wowote. Mkataba huu sio wa Gati zote za Bandari ya Dar es Salaam. Gati ambazo hazipo kwenye mkataba huu zitatafutiwa Mwenyekezaji mwingine. Mkataba huu hauhusishi Bandari yoyote mwambao wa Bahari ya Hindi wala Maziwa Mkuu. Mikataba iliyosainiwa ni “Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement; Mkataba wa Upangishaji wa Ardhi (Lease Agreement na Mkataba wa Uendeshaji wa Bandari (Concession Agreement.) Uwekezaji huu unapania pamoja na mambo mengine kukuza biashara, kuboresha shughuli za kiuchumi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali sanjari na kukuza uchumi wa Taifa. Mikataba hii imesaniwa kwa kuzingatia Kifungu cha 2 cha Sheria ya Ubia Namba 6 ya Mwaka 2023 (The Public Partinership Act Cap 103 na Kifungu cha 2 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 5 ya Mwaka 2023 (The Public Procurement Act No 5 of 2023. “Kila pale ambapo sekta binafsi inaweza kuweka fedha, serikali tusiweke fedha – [badala yake] tuitumie kwa maendeleo ya jamii. Waje wawekeze, tufanye nao biashara, wapate, tupate. Na yale mapato ya serikali tuyapeleke kwenye matumizi mengine zaidi. Mmesikia hapa tuna asilimia kubwa ya watu wetu ambao ni maskini, tutumie kuwanyanyua katika ngazi tofauti tofauti,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan.
“Katika mzunguko wote wa majadiliano, nilichobaini ni kwamba sote Watanzania tunakubaliana kuwa tunayo changamoto pale bandarini. Tunatofautiana tu juu ya namna ya kuzitatua. Wapo wanaoamini sisi wenyewe bila mbia tungeweza kuzitatua. Ni mawazo mazuri ya kimapinduzi, lakini yapo mbali na uhalisia. Na njia hiyo itatuchukua muda mrefu sana kufika. Wakati Dunia inakwenda mbio, sisi tutakua bado tunasota. Na isitoshe tulishajaribu lakini hatukufanikiwa. Kwa hiyo mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa kwa mtu mmoja mmoja na kupitia makundi ya kijamii pamoja na sheria na taratibu zote za nchi yetu. Nataka niwahakikishie kuwa maslahi yote mapana ya nchi yamelindwa.” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr Samia Suluhu Hassan. “Nataka niwahakikishie kuwa au niwape uhakika Watanzania wote kwamba maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa. Kwa mfano amesema hapa Mkurugenzi hakuna atakayepoyeza kazi. Awe mwajiriwa wa bandari au hata wanaofanya kazi zao bandarini. Hakuna atakayepoteza kazi. Kutakuwa tu na kufuata mfumo fulani katika kufanya kazi zetu ili viwango zile vikae sawa tuendane na Dunia. Kinachofanyika kama nilivyosema ni kuhakikisha bandari inaendeshwa katika viwango vinavyokubalika duniani, kukuza ufanisi na biashara na hatimaye kukuza mapato ya nchi yetu,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan.
Naye Plasduce Mkeli Mbossa, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) amesema, “Meli nyingi husubiri nangani kwa muda mrefu kabla ya kuhudumiwa. Mpaka sasa tunazo meli 29 zinazosubiri kuingia bandarini. Lakini katika gati 12 ambazo tunazo, tuna meli 12 ambazo zilihudumiwa. Mheshimiwa Rais, wastani wa meli kusubiri nangani ni siku 5 kwa kiwango cha chini hadi siku 10 ikilinganishwa na bandari za wenzetu kama Mombasa ambao wastani ni siku 1.25 lakini kwa bandari ya Durban ni siku 1.6.” “Pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za maboresho katika bandari ya Dar es Salaam, bado ufanisi wa utoaji huduma za bandari haujafikiwa viwango vya kimataifa. Hali ya sasa ya utendaji wa bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda” – Plasduce Mkeli Mbossa, Mkurugenzi Mkuu TPA. “Hili linatokana na kukosekana kwa uwekezaji mkubwa kwa muda mrefu ambazo zingeweza kupelekea kuongeza idadi ya gati katika maana ya kwamba tunazo gati 12 tu katika bandari ya Dar es Salaam. Lakini tunazo meli 30 ambazo zinasubiri kuingia. Lakini pia ni lazima uhudumie meli zile kwa wakati ili uweze kuingiza meli nyingine.” Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa. “Athari za kutokuwa na ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na meli kusubiri muda mrefu nangani jambo ambalo linatokea mpaka sasa, ambapo kunasababisha kuongezeka kwa gharama za kutumia bandari ya Dar es Salaam” Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mkeli Mbossa.