Hospitali ya Familia Takatifu huko Bethlehemu. Hospitali ya Familia Takatifu huko Bethlehemu. 

Nchi Takatifu,Hospitali ya Familia Takatifu:Betlehemu ni kisima cha amani

Kituo cha huduma ya afya cha watoto kinachosimamiwa na Shirika la Kijeshi la Malta kinajulikana kwa uobra wake katika eneo lote.Watoto kumi wanazaliwa huko kila siku,licha ya kuongezeka kwa vurugu katika Nchi Takatifu.Kwa kujali kila mtu na kudumisha miunganisho katika pande zote za ukuta wa kujitenga,hospitali imetuma ujumbe wa Noeli wa matumaini.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Kwa zaidi ya miaka thelathini, watoto wamezaliwa katika Hospitali ya Familia Takatifu huko Bethlehemu, akina mama vijana wamekuwa wakitunzwa, na ubora wa matibabu haujawahi kuyumba. Haya yote yamefanyika licha ya kutojulikana kutokana na vurugu katika Nchi Takatifu. Vile vile imekuwa kweli ikijikita kusaidia  tangu Oktoba 7 na shambulio la Hamas kusini mwa Israeli. Kwa hiyo kuzuka kwa vita katika Ukanda wa Gaza na kutengwa kwa Ukanda  wa Magharibi na vikosi vya jeshi la Israeli kumesababisha dosari katika eneo hilo, lakini katika hospitali ya watoto inayoendeshwa na Shirika la Kijeshi la  Malta, umakini unabaki kulenga utume wa  kukaribisha na kutibu wagonjwa, kwa gharama yoyote.

Mara tu baada ya tarehe 7 Oktoba 2023, tulikuwa na wasiwasi sana juu ya kile ambacho kingeweza kutokea, kwa sababu hakuna mtu ambaye angeweza kufikiria hayo yote lakini ikiwa wasiwasi utaendelea, Bethlehem itabaki kuwa chemchemi ya amani,” alisema Gilles Normand, mkurugenzi wa hospitali hiyo. Jiji la Kuzaliwa kwa Yesu, ambalo linaishi nyuma ya ukuta wa kujitenga, linasonga kwa mwendo wa polepole. Mnamo tarehe 2 Desemba 2023, usiku wa kuamkia Dominika ya kwanza ya Majilio, Msimamizi wa Nchi Takatifu, Padre Francesco Patton, aliweza kuingia ndani ya jiji na sherehe yenye sifa ya utulivu na pazia la huzuni katika Hospitali ya Familia Takatifu ambayo sasa  imelazimika kuzoea.

Mkurugenzi wake alilazimika kurudisha wafanyakazi wawili wa kujitolea nchini Ufaransa mnamo tarehe 19 Oktoba 2023  na baadhi ya wafanyakazi wa Palestina sasa wamehifadhiwa katika kituo cha afya kutokana na ugumu wa kufika Ukanda  wa Magharibi. “Katika hospitali kuna roho ya familia na watu wanasaidiana, na hii ni muhimu, kwa sababu inaturuhusu kuendelea na kazi yetu ya kusaidia watu katika shida.” anaelezea Gilles Normand. Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa kipindi hiki cha Noeli ni maalum kutokana na vita. Mita mia chache kutoka katika Jengo la Shirika la Kijeshi la Malta, kuna Basilika ya Kuzaliwa kwa Bwana na Uwanja wake ambao umekuwa tupu kuliko kawaida mwaka huu, kwa sababu ya vizuizi, lakini katika Familia Takatifu kila mtu, Waislamu na Wakristo, wanaombea amani ije haraka.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo aidha alisema "Roho ya amani pia inaonekana katika idara za hospitali." Siku chache zilizopita, madaktari wa Israel katika hospitali ya Hadassa mjini Jerusalem walimpigia simu Normand kumwomba amtunzie msichana kutoka Gaza ambaye alikuwa karibu kujifungua. “Hapa, kama Wakristo, tunaweza kujenga madaraja badala ya kuta. Uhusiano wetu na watu wa Israeli hautabadilika, kwa sababu tumejitolea kuwajali wengine. Huu ni ujumbe mkubwa wa matumaini.” Mkurugenzi anahitimisha, karibu  kwa kushangaa kuwa: “Bethlehemu ni chemchemi ya amani na hospitali ni mfano wa hili. Inashangaza sana, lakini hebu tumshukuru Mungu kwa hali hii.”

Habari Desemba 28, 2023
28 December 2023, 11:24