Tafuta

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Jumanne, Desemba 5, 2023, ameshuhudia kazi ya kusomba matope kwenye mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Jumanne, Desemba 5, 2023, ameshuhudia kazi ya kusomba matope kwenye mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara.  (AFP or licensors)

Maporomoko ya Udongo Mlima Hanang,Mkoani Manyara,Tanzania

Serikali imesema kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang mkoani Manyara,ambao ulikuwa na miamba dhohofu iliyonyonya maji ndio chanzo cha maporomoko yaliyoleta maafa katika eneo hilo la Hanang mkoani Manyara.Maporomoko hayo ya matope yamesababisha vifo vya watu 68 na majeruhi zaidi ya 116 huku mamia ya wanachi wakipoteza mifugo,mashamba na makazi yao kwa ujumla.Serikali inaendelea kuwahudumia waathirika.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu,Hanang, - Manyara,Tanzania.

Serikali ya Tanzania imesema kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang mkoani Manyara, ambayo ilikuwa una miamba dhohofu iliyonyonya maji ndio chanzo cha maporomoko yaliyoleta maafa katika eneo hilo la Hanang mkoani Manyara. Maporomoko hayo ya matope yamesababisha vifo vya watu 68 na majeruhi zaidi ya 116 huku mamia ya wananchi wilayani Hanang wakipoteza mifugo, mashamba na makazi yao kwa ujumla. "Sehemu iliyonyonya maji ilizua mgandamizo na sehemu ya Mlima ikashindwa kuhimili mgandamizo na hivyo kusababisha kumeguka kwa sehemu hiyo na kutengeneza tope ambalo ndio lilianza kuporomoka kufuata mkondo wa mto Jorodom uliozoa mawe na miti na kushambulia makazi ya binadamu yaliyokuwa pembezoni mwa mto huo.” Hayo yamebainishwa na Msemaji mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Jumanne, Desemba 5, 2023, ameshuhudia kazi ya kusomba matope kwenye mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara, ikianza kwenye barabara kuu ya kutoka Babati hadi Singida. Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo, Waziri Mkuu amesema idadi ya watu waliokufa katika maafa hayo imefikia 65 ambapo watoto wawili waliokuwa wamelazwa wameaga dunia. Ametumia fursa hiyo kuwafikishia salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba amekatisha ziara yake nje ya nchi na tayari amewasili nchini Tanzania. "Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapa pole sana na sisi Serikali tutaendelea kutekeleza maelekezo yake ya kuwahudumia na kurejesha hali ya utulivu."

Kazi inayoendelea ni kusafisha tope ili watu waendelee na maisha kama kawaida
Kazi inayoendelea ni kusafisha tope ili watu waendelee na maisha kama kawaida

"Kazi inayofanyika sasa ni kuondoa tope lote ili tupate level ya zamani na watu waweze kuendelea na kazi zao. Tuna makamanda 1,265 wa vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, na wako hapa katika maeneo tofauti. Wataendelea kufanya kazi ili kuhakikisha tunarejesha mji wa Katesh katika hali ya kawaida. Malengo yetu ndani ya siku mbili hadi tatu hali ya kawaida irejee," ameongeza. Amesema maagizo ya Mheshimiwa Rais kuhusu kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wote yanazingatiwa, watu walioko kambini wanahudumiwa na kwamba iko timu ya wataalam kutoka Serikalini ambayo inafanya tathmini ya athari za maafa na mwishoni itatoa taarifa rasmi. Mapema, Waziri Mkuu aliwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na kutembelea wodi ya watoto, wanaume na wanawake. Pia alikutana na timu ya madaktari bingwa kutoka Dodoma na Arusha inayoongozwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ernest Ibenzi ambaye alisema timu yake ina watu 21 wakiwemo madaktari bingwa 12 ambapo sita wanatoka Dodoma na wengine sita wanatoka Arusha. "Hawa tisa ni madaktari wasaidizi, wataalamu wa usingizi na wauguzi wa vyumba vya upasuaji," alisema.

Kuna makamanda 1, 265 wa vikoasi vya ulinzi na usalama ambao wako kazini
Kuna makamanda 1, 265 wa vikoasi vya ulinzi na usalama ambao wako kazini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatembelea watu walioathiriwa na mafuriko ya tope na mawe katika mji mdogo wa Katesh, wilaya ya Hanang, mkoani Manyara na kuwapa salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Akizungumza nao kwa nyakati tofauti, Jumanne, Desemba 5, 2023) kwenye shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita ya Katesh, Waziri Mkuu amewaomba wawe watulivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu maafa hayo. Amewaomba wawe watulivu kwani watakuwa hapo shuleni kwa muda wakati Serikali ikiwatafutia sehemu mbadala. “Ninawaomba muendelee kutulia wakati Serikali bado inaratibu maafa haya kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza.” Akielezea hali ilivyokuwa, mmoja wa manusura hao, Mzee Martin Daniel Kessy alisema Jumapili asubuhi alipotaka kutoka ndani akakuta maji mengi na mengine yanaingia ndani. "Wakati nahangaika kuzuia maji, nikasikia wajukuu wakiniita babu, babu, maji yanajaa, ikabidi niwape nyundo watoboe dari na bati. Walipokuwa juu salama, nami nikaweka ngazi na kupanda juu na kusubiri msaada sababu hapo chini maji yalishanifika kifuani," alisema.

Maporomoko ya udongo Hanang mkoani Manyara yamesababisha maafa
Maporomoko ya udongo Hanang mkoani Manyara yamesababisha maafa

Mzee Kessy ambaye pia ni Balozi wa mtaa wa Katesh A Sokoni, amemthibitishia Waziri Mkuu kwamba katika mtaa wake hakuna watu waliopoteza maisha isipokuwa wote walishindwa kuokoa mali zao. "Nilicheki na watu wangu wote wako salama lakini hakuna aliyetoka na kitu, si magodoro wala mahindi, hakuna aliyetoka na kitu chochote ndani ya nyumba," amesema Mzee Kessy ambaye mtaa wake ulikuwa na kaya 40. Naye kijana Khalid Salehe ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Katesh B, alimweleza Waziri Mkuu kwamba mama, kaka na dada zake wote ni wazima na kwamba wamenusurika kwenye mafuriko hayo. Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama baba yake naye amenusurika, Khakid alijibu kuwa baba yao alikuwa amesafiri na yuko Iringa. Kijana mwingine ambaye anasoma darasa la nne na Khalid na yupo kwenye kambi hiyo, Omari Miraji alisema kuwa wazazi wake, kaka na dada zake wote wamesalimika. Alipoulizwa kama kuna rafiki zao au wanafunzi wenzao waliopotea kutokana na mafuriko hayo, alijibu kwamba hakuna aliyepotea. Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika shule hiyo wametenga chumba cha kutunza misaada wanayoipokea. Alisema hadi sasa wameshapokea, magodoro 200, mashuka, mablanketi, mikeka, maji, unga, mchele, mabeseni, ndoo na baadhi ya nguo za watoto.

Maafa Tanzania
06 December 2023, 14:55