Tafakari Dominika IV KIpindi cha Majilio: Bikira Maria Sababu Furaha ya Ulimwengu
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Leo tunawasha Mshumaa wa amani. Je, mishumaa yote inawaka sasa? Tusikae gizani mshumaa wa matumaini uwake, mshumaa wa Upendo uwake, mshumaa wa furaha uwake na mshumaa wa amani uwake. Maisha yetu yawake matumaini, Mapendo, Furaha na Amani. Leo Bikira Maria Mtakatifu kwa ndio yake Mungu anautwaa mwili katika tumbo lake anafanyika mwanadamu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ndiye Emanueli Mungu pamoja nasi, Eva mpya na anayesikia Neno la Mungu kwa unyenyekevu na kulitii, mjakazi huyu wa Bwana asiye na maneno mengi bali matendo yake yanamueleza jinsi gani aliyojaliwa neema tele kuliko wanadamu wote na yule atakaye mzaa ndio baraka yenyewe kwa ulimwengu. Mpendwa msikilizaji wa radio aticani tunapohitimisha kipindi cha pili cha majilio tuongozwe na tafakar ihii, “Ndio ya Bikira Maria sababu ya furaha yetu.“
UFAFANUZI: Katika hali ya kawaida uwepo wa mtu uridhihirika pale anapozaliwa, ndivyo ulivyo hata uelewa wa baadhi wa watu, juu ya uwepo wa Mungu kati ya wanadamu yaani yesu wengi huanza kuamini kuwa Yesu aliye nafsi ya pili ya Mungu anaanza kuwepo kimwili kati ya wanadamu baada ya kuzaliwa na Maria, huo sio ukweli kama mama kanisa anayotufundisha na ndio uhalisia naukweli kamili Yesu alianza kuwa mwanadamu kati yetu baada ya Malaika Gabriel kumpasha habari Maria za kumzaa Yesu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, na kitendo cha Bikira Maria kukubali mapenzi ya Mungu yafanyike ndani yake papo hapo ndipo Yesu alipotwaa ubinadamu wetu akaanza kuishi kati yetu ndani ya tumbo la Maria, na alipozaliwa kimwili akaonekana kama sisi isipokuwa hakuwa na dhambi, hivyo Maria anaposhiriki mpango wa ukombozi wa Mungu kumkomboa mtu kutoka utumwa wa dhambi, ni binti huyu wa nazareti ndiye sababu ya furaha yetu, na amani yetu. Katika somo la kwanza kutoka kwa Nabii Samweli 7: 1-5,8-11,16: Nabii Samuel anasema Mungu anahaidi kuwa huyu mtumishi wake kwamba atakuwa pamoja nawe kokote uendako, kuwakatilia mbali adui zako wote, kukufanyia jina kuu na kukustarehesha mbele ya wote akiithibitisha nyumba yako kwa milele... mkristo ukimdai Mungu zaidi ya haya basi umeishashindikana! Maana ulizi huu wala hauhitaji cctv kamera. Yafaa kutafakari zaidi kuwa Maria alitumia haki yake ya uhuru wa kuchagua, hapa ndipo kuna somo sana, ikimbukwe Maria alikuwa msichana mdogo ambaye alikuwa ameposwa, na kwa mila na tamaduni za kiyahudi msichana aliyeposwa alipaswa kuwa mwaminifu, ndio maana hata swali lake kwa malakia Gabriel lilikuwa “itawezekanaje wakati mimi simjui mume“ huu ulikuwa ni ujasiri wa hali ya juu hasa baada ya kumsililiza kwa makini malaika Gabriel na ujumbe wake alitekeleza mapenzi ya Mungu kwa uhuru kamili na utashi kamili kwa kusema „‘Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema‘ swali la kujiuliza hivi binti wa leo hii ungechagua Nini?
Hata hivyo, katika Injili ya leo, katika kujibu swali la Maria jinsi yeye, bado bikira, anaweza kuwa mama, malaika anajibu: "Roho Mtakatifu atakujilia na nguvu za Aliye Juu Zaidi zitakufunika kwa kivuli chake. Na hivyo mtoto atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu aliye juu." Binti huyu Sayuni, binti Yerusalemu, sio kwa tamaa ya nafasi hii kubwa, au ili kujipatia umaarufu na sifa, au ili dunia imuone, imtambue, imsifu na kumnyenyekea bali makusudi mapenzi ya Mungu yatimie, kwa unyenyekevu mkubwa wa nafsi yake nzima na kwa moyo wa shukrani anayapokea yote, tena bila kuelewa vizuri kwa wakati ule, akijiona mdogo na si kitu mbele ya Bwana Mungu wake, alisema “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana, iwe kwangu kama ulivyosema”… na ukubali huu ukafungua barabara nzuri kwa wokovu kumfikia mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo… asante sana Mama Bikira Maria uliyejaa neema naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa! "Ndiyo" ya Bikira Maria ilibadilisha ulimwengu. Utiifu wake kwa wito wa Mungu ulibadilisha maisha ya sisi sote - waumini kwa namna moja au nyingine. Labda utii sio maarufu katika ulimwengu wa leo wakati watu wanataka kuwa huru kwa kila jambo. Uhuru usi ona mipaka wa kuamua kile unachotaka ikumbukwe uhuru bila mipaka ni fujo na ukweli sasa tunashuhudia dunia ikiwa imelemewa na fujo za kilaaina. Leo kuna uraibu wa madawa ya kulevya, Uraibu wa madaraka, uraibu wa starehe, uraibu wa ngono, uraibu wa mali kupindukia, uraibu wa umaarufu, nk. Ulimwengu unahusisha utiifu na udhaifu na ukosefu wa maarifa. Utiifu wa kweli unatokana na uchaguzi huru uliofanywa kwa mwanga wa kile kilicho cha kweli na kizuri. Utiifu wa kweli unahitaji ujasiri mkubwa kwa sababu unaweza kuhusisha kwenda kinyume na wimbi la matarajio ya kijamii. Maria lazima alikuwa na mengi ya kuelezea kuhusu mimba yake ya mapema.
Utiifu wa kweli haulengi kwa usalama kulingana na matarajio ya wale wenye nguvu zaidi kuliko wengine, bali kujiweka katika huduma ya kitu ambacho ni kikubwa kuliko nafsi yako. Katika maandiko matakatifu hasa Injili zote, lililo kubwa si wale ambao wana utawala wa kulazimishwa juu ya wengine lakini wale ambao hutoa rasilimali zao binafsi kutumikia na kujenga. Ukuu wa kweli, basi, ni vyema kukubali kile ambacho Mungu anataka tufanye au kile anachotaka tufanye. Wewe unadaiwa jambo moja tu, nalo lakutosha kabisa… fungua moyo wako, upe utayari utashi wako na ivalishe unyenyekevu akili yako, “usikaze ubongo”, na kwa moyo wa imani matumaini na mapendo, ukijiachilia kabisa bila kujibakiza mikononi mwa Mungu useme pamoja na Mama Maria: “Mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema.” Pengine labda una hofu na huna hakika ukijihoji moyoni mwako “litakuwaje neno hili?”(Lk 1:34)… jitulize umtazame, anakungoja akisubiri maamuzi yako akikutazama kwa huruma na upole katika mashaka na hofu uliyonayo ili kukupa moyo na kukuondolea mashaka yaliyoujaza na kuutesa moyo wako akisema “Roho Mt atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli, kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu Mwana wa Mungu” (Lk 1:35) Jisalimishe kwake ili kupokea agano lake kama lituambiavyo somo la I leo (2Sam7:1-5, 8-11, 16) ya O mwanadamu mimi, ingekuwa heri kwangu kuiishi karama hii ya unyenyekevu kama Mama Bikira Mtakatifu… kutotamani makubwa kupita uwezo wangu, kutomnyanyasa yeyote kwa nafasi yangu niliyojaliwa na Mungu, kutomdhalilisha yeyote kwa vile amekosea na kufanya isivyofaa kwa macho yangu ya kibinadamu, kutokumuaibisha yeyote kwa vile ni mnyonge asiye na chochote na hawezi kunifanya lolote, kutokumnyima haki yeyote ajaye mbele yangu. Kutokumdhulumu mtu fedha, mali, utu, uhuru, haki na heshima yake kama kiumbe wa Mungu aliyebeba sura na mfano wake, kutodhania kwamba mimi ndio nimefika na hivi watu wote si lolote wala si chochote ila mimi tu ndio kila kitu, kutokumfanya yeyote akose furaha na amani kwa namna yoyote ile… badala yake kumtendea jirani yangu vile ningependa mimi kufanyiwa na kutomtendea mwenzangu yale ambayo ningependa nisifanyiwe… hakika ingekuwa heri kwangu! Usisahau, Mwenyezi Mungu anauangalia unyenyekevu wa mjakazi wake, anawakweza wanyenyekevu na kuwashusha wenye vyeo na kuwatawanya wenye kiburi ndani ya mioyo yao, rehema zake zadumu kizazi hata kizazi kwa wote wenye kumcha (Lk 1:46-55 - Magnificat! tunapotiwa moyo na neno hili la faraja tujiaminishe kwake tukipiga moyo konde na hamu ya mioyo yetu itatimizwa… amina!