Tafuta

Mvua kali imesababisha maafa makubwa hata vifo kadhaa mjini  Dar Es Salaamu, Tanzania. Mvua kali imesababisha maafa makubwa hata vifo kadhaa mjini Dar Es Salaamu, Tanzania.  (AFP or licensors)

Tanzania:Mafuriko jijini Dar es Salaam yaleta maafa makubwa

Wakati wa Mji wa Dar Es Salaam,Tanzania walijikuta wanapiga magoti kutokana na kuharibika kwa miundo mbinu na mji kugawanyika mara mbili kufuatia na kukatika kwa madaraja kutokana na mvua nyingi iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo na kusababisha hata vifo kadhaa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumamosi alfajiri tarehe 20 Januari 2024 watu wa Jiji waliona tukio kubwa ambalo wengine walikuwa hawajawahi kuona. Ni Nchini Tanzania, ambapo watu kadhaa waliripotiwa kufariki, nyumba na barabara zikiharibiwa baada ya mvua kubwa kunyesha kwa muda wa siku mbili na kusababisha mafuriko katika mji wa kibiashara wa Dar es Salaam. Nyumba kadhaa zilizo karibu na mto zilianguka, barabara na daraja zikiharibiwa kama vile huko Kunduchi na Tegeta, na sehemu nyingine, hatua ambayo ilifanya kuwa vigumu kwa watu kusafiri kutoka sehemu moja kwenye nyingine. 

Uharibifu wa miundo mbinu

Barabara kuu ya Bagamoyo inayounganisha jiji kuu la Dar Es Salaam na maeneo ya kaskazini mwa taifa la Tanzania haikuwa inapitika siku ya Dominika, mara baada ya mvua kubwa kunyesha kwenye eneo hilo hasa Jumamosi tarehe 20 Januari 2024 ambayo iliona maajabu makubwa na madhara makubwa sana. Shughuli za urejeshaji wa baraba zinaendelea.

Rais Suluhu ametoa rai kuchukua tahadhari

Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Mama Samia Suluhu, siku ya Dominika tarehe 21 Januari 2024 aliwataka raia wote kuchukua tahadhari ya kuepuka maeneo yaliyo hatarini. Mkuu wa nchi hiyo aidha alitoa wito kwa mamlaka ya uokozi ili kuhakikisha kuwa mvua inayoendelea kunyesha haisababishi vifo zaidi. Na mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa kwenye taifa la tanzania lilionya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mvua kubwa mwezi huu wa Januari 2024.

Mvua kubwa hata miezi ya mwisho wa 2023

mwaka 2023 mvua kubwa iliathiri maeneo ya kaskazini mwa Tanzania tangu Oktoba wakati wa msimu wa mvua za Oktoba na Desemba  na kusababisha mafuriko, mito kujaa na maporomoko ya ardhi. Mnamo  tarehe 2 Desemba 2023, maporomoka ya ardhi yalitokea katika kijiji cha Kateshi katika Wilaya ya Hanang Magharibi mwa Manyara, na kusababisha uharibifu mkubwa ulioripotiwa. Maporomoko hayo pia yaliharibu miundombinu ya umma, ikiwemo barabara, umeme, na mifumo ya mawasiliano na maji. Na vile vile maeneo mengine mbali mbali nchini Tanzania, kuanzia kusini, Kaskazini, mashariki, magharibi na kati.

22 January 2024, 17:46