Tafuta

Rais Samia Suluhu Hassan akimpongeza Drk. Emmanuel Nchimbi baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, CCM. Rais Samia Suluhu Hassan akimpongeza Drk. Emmanuel Nchimbi baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, CCM. 

Dkt. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, CCM

Dkt. Nchimbi ametanguliza shukrani zake za dhati kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa pamoja na Wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kumwamini na kumpitisha katika kuhudumu katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, akiwa ni Katibu mkuu wa kumi na moja, tangu kuanzishwa kwa CCM. Watanzania wengi wanamwelezea Dkt. Nchimbi kama kiongozi mwenye uelewa mpana kuhusu maswala ya Siasa, Diplomasia, Uchumi na Kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa imemteua Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na uteuzi huu kuthibitishwa na Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM katika kikao chake kilichofanyika mjini Unguja, Zanzibar. Dkt. Nchimbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo ambaye alijiuzulu kwa madai ya kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii. Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi ametanguliza shukrani zake za dhati kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kumwamini na kumpitisha katika kuhudumu katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – Taifa, akiwa ni Katibu mkuu wa kumi na moja, tangu kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi. Watanzania wengi wanamwelezea Dkt. Nchimbi kama kiongozi mwenye uelewa mpana kuhusu maswala ya Siasa, Diplomasia, Uchumi na Jamii, na wengine wanasema huenda CCM watamtumia kama karata yao muhimu wakielekea kwenye uchaguzi mkuu 2025 na hata ule wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu wa 2024. Itakumbukwa kwamba, Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya, Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986. Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia Kundi la Majeshi na baadaye Katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Dkt. Emmanuel Nchimbi anakuwa ni Katibu wa 11 wa CCM.
Dkt. Emmanuel Nchimbi anakuwa ni Katibu wa 11 wa CCM.

Dkt. Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari na kubahatika kusoma katika Seminari ya Uru, Moshi, Kilimanjaro inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Mitume wa Yesu, AJ., kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990. Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997). Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM). Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003. Alisoma shahada ya Uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya benki na fedha. Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Dkt. Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu. Dkt. Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. Dkt. Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6% dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akiteta na Dkt Nchimbi.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akiteta na Dkt Nchimbi.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009. Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa CHADEMA na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dkt. Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10% ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro. Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013. Dkt. Nchimbi alianza mbio za Urais tangu alipokuwa Naibu Waziri kwenye awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Desemba 3, 2016, Dkt. Nchimbi aliteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil na baadaye, alipangiwa kituo cha kazi Nchini Misri na kisha Agost 11, 2023 Rais Samia alimrejesha nyumbani. Januari 15, 2024, Dkt. Nchimbi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akichukua nafasi ya Chongolo aliyejiuzulu nafasi hiyo.

Dk Emmanuel Nchimbi
16 January 2024, 13:49