Vizuizi vya barabarani vinavyochomwa huwalazimisha watu kupata makazi, huko Port-au-Prince. Vizuizi vya barabarani vinavyochomwa huwalazimisha watu kupata makazi, huko Port-au-Prince. 

Haiti,watawa sita walitekwa nyara huko Port-au-Prince.Askofu Dumas:Kitendo cha unyama

Watu wenye silaha walimiliki Bus lililokuwa limewabeba watawa hao.Gari likiendeshwa hadi kusikojulikana.Askofu wa Anse-à-Veau et Miragoâne amelaani kitendo hicho ambacho hakiheshimu utu wa wanawake waliowekwa wakfu na ametoa wito wa kuachiliwa kwa watu wote waliotekwa nyara.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mji mkuu wa Haiti unakabiliwa na ongezeko la matukio ya vurugu hadi baadhi ya vitongoji kutengwa katika siku za hivi karibuni. Kulingana na vyanzo vya ndani, watawa 6 kutoka Shirika la Mtakatifu Anna walitekwa nyara pamoja na watu wengine, akiwemo dereva, walipokuwa kwenye Bus lililokuwa likielekea chuo kikuu katika mji mkuu Port-au-Prince. Gari hilo lilisimamishwa na watu wenye silaha ambao walipanda Bus na kuwachukua abiria wote mateka. Utekaji nyara huo ulifanyika siku ya Ijumaa tarehe 19 Januari 2024 mchana kweupe na katikati mwa mji mkuu. Utekaji nyara huo, uliothibitishwa na taarifa kwa vyombo vya habari kutoka katika Mkutano wa Watawa wa Haiti, pia umeshutumiwa vikali na Askofu  Pierre-André Dumas, wa Jimbo la Anse-à-Veau na Miragoâne, ambaye alilaani "kwa nguvu na uthabiti watu wenye chuki na kitendo cha kishenzi, ambacho hakiheshimu hata hadhi ya  wanawake waliowekwa wakfu ambao wanajitoa kwa moyo wote kwa Mungu ili kuwaelimisha na kuwafunza vijana, maskini na walio hatarini zaidi katika jamii yetu."

Askofu anatoa wito wa kuachiliwa mateka

Katika barua hiyo Askofu alitoa wito wa kuachiliwa kwa mateka na kukomeshwa kwa vitendo hivi vya kuchukiza na vya uhalifu. Kisha anaalika jamii nzima ya Haiti kuungana kuunda mlolongo wa kweli wa mshikamano karibu na watu wote waliotekwa nyara nchini, ili kupata kuachiliwa kwao na kuhakikisha kurudi kwao kwa usalama kwa familia na wapendwa wao! Dumas pia anajitolea kama mateka mahali pao. Tangu Dominika tarehe 14 Januari iliyopita, magenge yenye silaha yamezidisha vitendo vyao vya mauaji, huku maandamano ya kupinga ukosefu wa usalama yakiandaliwa nchini humo. Siku ya Alhamisi 18 Januari kitongoji cha Solino, kusini mwa Port-au-Prince, kilikuwa eneo la mapigano makali ya moto kati ya magenge hasimu na hasa kundi lenye silaha kutoka kitongoji cha karibu cha Bel-Air. Mapigano hayo yalisababisha takriban vifo ishirini, kulingana na mkuu wa shirika la kibinadamu la kutetea haki za binadamu.

Maandamano dhidi ya serikali

Vitongoji vingine vya mji mkuu kama vile Carrefour Péan na Delmas 24 pia vililengwa na mashambulizi ya magenge. Katika mitaa ya Port-au-Prince, wakazi waliweka vizuizi ili kujilinda. Zaidi ya hayo, kwa majuma kadhaa, utekaji nyara umeongezeka katika Port-au-Prince. Wiki iliyopita, daktari na jaji wa amani walitekwa nyara kabla ya kuachiliwa baada ya kulipwa fidia. Wakati huo huo maandamano dhidi ya serikali yamekuwa yakitikisa nchi kwa siku kadhaa kufuatia wito wa Guy Philippe, mkuu wa zamani wa Polisi na mwanasiasa kurejea Haiti baada ya kutumikia kifungo nchini Marekani kwa utakatishaji fedha unaohusishwa na ununuzi wa dawa za kulevya. Waandamanaji hao wanatoa wito wa kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye amekuwa madarakani tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mwaka 2021, wakimtuhumu kwa kutokuwa na uwezo wa kuongoza nchi katika ngazi ya kiuchumi na kiusalama kwa ujumbla.

20 January 2024, 11:07