Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei” ni usemi uliochaguliwa na Serikali ya Italia inayoongozwa na Waziri Mkuu Giorgia Meloni. Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei” ni usemi uliochaguliwa na Serikali ya Italia inayoongozwa na Waziri Mkuu Giorgia Meloni.  (ANSA)

Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika

Amani na ugawaji sawa wa rasilimali za dunia na kwamba, kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya unaofumbatwa katika usawa na wala si wanyanyang’anyi, mwelekeo wa ubaba au kama wahisani. Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika unajikita katika mambo makuu matano: Elimu, Majiundo, Afya, Kilimo, Maji na Nishati, utakaogharimu kiasi cha Euro bilioni 5.5, sawa na shilingi bilioni 969. Tanzania itafaidika katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei” ni usemi uliochaguliwa na Serikali ya Italia inayoongozwa na Waziri Mkuu Giorgia Meloni, ili kufanya muhtasari wa mpango mkakati wa ujenzi wa ushirikiano mpya kati ya Italia na Mataifa ya Afrika, mpango wa nishati na kijamii kwa Bara la Afrika kama kumbukizi ya Rais wa zamani wa Kampuni ya Eni, Enrico Mattei aliyezaliwa tarehe 29 Aprili 1906 na kuaga dunia tarehe 27 Oktoba 1962. Lengo ni kuondokana na mbinu ya unyonyaji iliyokuwa inatekelezwa na nchi nchi za Ulaya na hivyo kukuza maendeleo endelevu na ya kudumu. Rais Sergio Mattarella wa Italia katika hotuba yake ya kuwakaribisha wakuu wa Nchi tarehe 29 Januari 2024 amekazia mshikamano wa dhati kati ya Italia na Bara la Afrika, katika mambo msingi kama vile: Amani na ugawaji sawa wa rasilimali za dunia na kwamba, kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya unaofumbatwa katika usawa na wala si wanyanyang’anyi, mwelekeo wa ubaba au kama wahisani. Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika unajikita katika mambo makuu matano: Elimu, Majiundo, Afya, Kilimo, Maji na Nishati, utakaogharimu kiasi cha Euro bilioni 5.5, sawa na shilingi bilioni 969. Tanzania ni kati ya nchi nane ambazo zimechaguliwa kushiriki katika Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei” kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Nishati, Elimu na Kilimo. Hii ni taarifa ambayo imetolewa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari alipokutana na kuzungumza na Januari Makamba Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pembezoni mwa Mkutano wa Nne wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia.

Mkutano kati ya Italia na Nchi za Kiafrika 2024
Mkutano kati ya Italia na Nchi za Kiafrika 2024

Utekelezaj wa miradi hii unaanza mara moja baada ya mkutano huu. Hii ni pamoja na kugharimia gharama za upembuzi yakinifu wa miradi hiyo. Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba ameipongeza Serkali ya Italia kwa kuonesha nia ya kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika kupitia Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei” ambapo sekta ya nishati, elimu na kilimo zimepewa kipaumbele. Pamoja na mambo mengine, Mkutano huu umepania kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ili kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya Mataifa haya mawili kupitia Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei.” Bara la Afrika litatengewa nafasi na kupewa kipaumbele maalum katika ajenda ya Italia kwenye kipindi chake cha urais wa kupokezana katika Umoja wa Nchi Saba Tajiri Duniani, maarufu kama G7. Mbali na Italia, G7 inazileta pamoja Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Uingereza, na Marekani. Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alitangaza Jumatatu katika Kongamano Kuu la Italia-Afrika lililoandaliwa jijini Roma kwamba lengo la Italia–iliyochukua urais wa G7 mapema Januari, ni “kubuni sera madhubuti ya ushirikiano wa Kimataifa yenye lengo la kuifanya Afrika miongoni mwa ajenda zake katika urais wake G7.” Meloni alisema hayo alipohutubia viongozi 25 kutoka Afrika na wawakilishi wa taasisi kadhaa za Muungano wa Ulaya waliohudhuria kikao cha kongamano hilo kuu.

Vipaumbele: Elimu, Afya, Kilimo, Maji, Nishati na Majiundo
Vipaumbele: Elimu, Afya, Kilimo, Maji, Nishati na Majiundo

“Italia inatambua umuhimu wa ushirikiano na mshikamano baina ya mabara, hivyo tunapaswa kutafakari jinsi tunavyoweza kuufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wetu, kama washirika wenye nguvu zinazotoshana bila hila za ufyonzaji au utegemezi,” akasema Meloni. Meloni alisema Mpango wa Italia uliopewa jina ‘Mkakati wa Mattei’, unalenga kujenga ushirikiano na Afrika kwa njia inayosaidia kutatua changamoto ya uhamiaji wa kiharamu na pia kugeuza Italia kitovu cha usambazaji wa kawi kutoka Afrika hadi Ulaya wakati ambapo bara hilo linajaribu kadri ya uwezo wake kuepuka utegemezi wa mafuta na gesi kutoka Urusi. Mataifa mengi ya Ulaya yaliiwekea Urusi vikwazo tangu iivamie Ukraine mnamo Februari 24, 2022. Mpango Mkakati wa Mattei wa Maendeleo kwa Bara la Afrika “Piano Mattei” umetengewa bajeti ya Euro 5.5 bilioni (sawa na Shilingi 969 bilioni) ambazo ndani kuna “mikopo, ruzuku, na dhamana. “Kwa kiwango hicho, Meloni alisema “takriban Euro 3 bilioni zitatoka kwa hazina ya mazingira ya Italia na 2.5 bilioni zitoke kwa mfuko wa ushirikiano wa kimaendeleo.” Tayari waziri mkuu huyo kwenye mahojiano na kituo cha habari cha TG1 mnamo Jumapili, alifichua mradi wa majaribio wa kituo cha kozi anuwai kuhusu nishati jadidifu umeanzishwa nchini Morocco. Pia alisema miradi mingine ni ya elimu nchini Tunisia, na ile ya kupanua wigo wa huduma za afya nchini Pwani ya Pembe. Tunisia na Pwani ya Pembe zinashikilia nafasi za kwanza kwanza kwa raia wake waliowasili nchini Italia wakiwa ama: wahamiaji au wakimbizi kupitia bahari ya Mediterranean mwaka 2023.

Viongozi wa Serikali ya Italia na Umoja wa Ulaya
Viongozi wa Serikali ya Italia na Umoja wa Ulaya

Mkakati wa Mattei unatokana na mtumishi wa umma Enrico Mattei, ambaye katika miaka ya hamsini (1950s) alipendekeza Italia kuunga mkono juhudi za mataifa ya Kaskazini mwa Afrika kukuza chumi zao na kunufaika kutokana na rasilimali zao. “Mkakati wa Mattei unajikita zaidi katika kugawana rasilimali na ujuzi na hivyo dhamira kuu ya kongamano hili ni kupanga namna ufanisi utakavyopatikana,” akaahidi Meloni. Alisema miradi mingine itaanza kutekelezwa nchini Kenya, Algeria, Msumbiji, Misri na DRC. Jumapili, Tarehe 28 Januari 2024 Rais wa Kenya William Ruto alisema lengo kuu la kongamano kuu la Italia-Afrika ni kuunda mtandao wa ushirikiano wa kimaendeleo. “Kongamano hili linatoa fursa nzuri ya kuunda mikakati ya ushirikiano kuangazia masuala muhimu ya utoshelevu wa chakula, kozi anuwai, kawi na ujenzi wa miundomsingi,” akasema Rais Ruto kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter) mara baada ya kuwasili jijini Roma. Pembezoni mwa kongamano kuu hilo, Rais Ruto alikutana pia na Mkurugenzi Msimamizi wa Ngazi ya Juu katika Benki ya Dunia Bwana Axel van Trotsenburg, ambaye anatekeleza wajibu wa Sera ya Maendeleo na Ushirikiano. “Tumejadili masuala mengi likiwemo Kongamano Kuu lijalo la Muungano wa Kimataifa kuhusu Maendeleo almaarufu IDA21 ambalo Kenya itakuwa mwenyeji,” amesema.

Mpango wa Mattei

 

 

30 January 2024, 14:16