Katibu wa Un akihutubia Mkutano wa Kundi la 77 +China (G77+China)Kampala- Uganda Katibu wa Un akihutubia Mkutano wa Kundi la 77 +China (G77+China)Kampala- Uganda 

Katibu,UN:Kundi la nchi 77 ni Injini ya ushirikiano wa nchi zinazoendelea na maendeleo

Hakuna sababu ya karne ya 21 kunakili ukosefu mkubwa wa usawa uliokuweko karne ya 20.Amesema hayo Bwana António Guterres,Katibu Mkuu UN wakati wa kuhutubia Mkutano wa III wa Viongozi wa Kundi la Nchi 77 na China uliofanyika tarehe 21 Januari 2024,jijini Kampala Uganda.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa III wa viongozi wa kundi la nchi 77 na China, uliofanyika tarehe 21 Januari 2024 mjini Kampala, Uganda alisema: “Msikubali kanuni mpya kwa ajili ya teknoloija mpya ziandikwe na matajiri kwa ajili ya matajiri. Bwana Guterres alisema ushiriki wa kundi hilo lenye wanachama 134 sasa kutokea nchi 77 waliokuwako miaka 60 kundi hilo lilipoundwa ni muhimu kwani hakuna sababu ya karne ya 21 kunakili ukosefu mkubwa wa usawa uliokuweko karne ya 20. Bwana Guterres alisisitiza kuwa teknolojia za kidijitali zina fursa kubwa ya kuleta mambo bora, lakini vile vile zinachochea ukosefu wa usawa. “Shirika la Fedha Duniani, linaonya kuwa Akili Mnemba (AI) inaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.” Lakini “teknolojia mpya zinaweza kufanya kasi kubwa ufanikishaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs,” ambayo yanafikia ukomo wake 2030.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akihutubia ufunguzi wa Mkutano III wa Kundi la 77 na China huko Munyonyo Kampala Uganda
Rais wa Uganda Yoweri Museveni akihutubia ufunguzi wa Mkutano III wa Kundi la 77 na China huko Munyonyo Kampala Uganda

Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa adha alisema kuwa Mkataba pendekezwa kuhusu Matumizi ya Kidijitali Duniani, unalenga kuhakikisha katika zama mpya ya teknolojia ambayo hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma. Hivyo amesema ni matumaini  yake kuwa mkataba huo uliopendekezwa utapitishwa wakati wa Mkutano wa Viongozi kuhusu Zama Zijazo, utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu 2024 jijini New York, Marekani. Aidha Katibu Mkuu wa UN amewajulisha kuwa Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Akili Mnemba (AI) ambalo aliliunda mwaka 2023 likijumuisha wataalamu kutoka G77, ikiwa ni asilimia 50  ya nchi zinazoendelea na asilimia 50  ya nchi tajiri limewasilisha mapendekezo ya awali kuhusu usimamizi wa AI duniani na mchango wake katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs.) Bwana  Guterres alipongeza nchini Cuba ikiwa ndiyo Rais wa G77 kwa kuweka sayansi na teknolojia kama jambo la kupatiwa kipaumbele na kundi hilo.

Washiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa III wa Kundi la Nchi 77 pamoja na China huko Kampala Ungada
Washiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa III wa Kundi la Nchi 77 pamoja na China huko Kampala Ungada

Katibu Mkuu  wa UN hakuweza kuhitimisha hotuba yake bila kuzungumza mizozo inayoendelea duniani ikiwemo vita inayoendelea katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, (Hamas) kwa zaidi ya siku 100 sasa: “Mashariki ya Kati inawaka moto. Lazima tufanye kila tuwezalo kuzuia mzozo huo kusambaa ukanda mzima. Na hii ianze na sitisho la haraka la mapigano kwa sababu ya hadhi ya  kiutu ili kupunguza machungu huko Gaza,  na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikia kila mtu mwenye kuhitaji na kufanikisha kuachiliwa huru mateka wote haraka iwezekanavyo bila masharti yoyote.”

Picha ya Pamoja kundi la Nchi 77 na China waliofanya mkutano huko Kampala Uganda
Picha ya Pamoja kundi la Nchi 77 na China waliofanya mkutano huko Kampala Uganda

Katibu Mkuu vile vile alisema kuendelea kukataa hapo tarehe 20 Januari “kukubali suluhisho la mataifa mawili kwa Israel na wapalestina haikubaliki kabisa kama nilivyowaeleza viongozi wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote, NAM.” Kwa njia hiyo alirejea kauli yake kuwa kuendelea kuwanyima wapalestina haki ya kuwa na taifa lao kutaendeleza mzozo ambao tayari ni tishio la usalama na amani duniani; unaongeza mgawanyiko na kuibuka kwa misimamo mikali kila mahali. Katibu Mkuu alipongeza kundi hilo la nchi 77 na China   akisema kuwa miongo kadha limekuwa Injini ya ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea na maendeleo, ikiinua mamilioni ya watu kutoka kwenye lindi la umaskini, na kuzipatia nchi zinazoendelea sauti kwenye jukwaa la kimataifa.

Rais Museveni akipokea nyundo, ishara ya ngvu kutoka kwa Makamu Rais wa Cuba Salvador Valdes Mesa
Rais Museveni akipokea nyundo, ishara ya ngvu kutoka kwa Makamu Rais wa Cuba Salvador Valdes Mesa

Hata hivyo Katibu Mkuu wa UN alisema mamilioni ya wakazi walioko kwenye nchi hizo, bado wamekwama kwenye umaskini kutokana na madhara ya janga la Uviko-19, nchi zao zikiwa zinakwamishwa na madeni, gharama ya maisha ikiongezeka, sambamba  na gharama za kukopa fedha. Kwa kuongeza Katibu wa UN alisema: “Madhara ya majanga ya tabianchi ambayo wengi wenu mmechangia kidogo sana kusababisha yamevuruga uchumi wenu na kuongeza machungu kwa watu.” Kwa kuongezea: “ ingawa ushirikiano wa nchi za kusini umekuwa thabiti na unaimarika ukitatua changamoto hizo, hii haichukui nafasi ya nchi tajiri kutekeleza ahadi zao za ushiriki endelevu wa kusaidia kutokomeza umaskini na kusaidia kujengea mnepo nchi zinazoendelea.”

 

22 January 2024, 16:43