Tafuta

Waandamanaji mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Waandamanaji mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).  (ANSA)

DRC:raia wakimbia kutokana na milipuko ya M23

Sake ni moja ya kitovu ch mapigano makali kati ya jeshi la Congo na kundi la waasi la M23;jiji hilo limepigwa siku zilizopita na mabomu ambayo yaliendelea kuanguka na kuwalazimu watu kuhama kutafuta hifadhi kwingine,hasa huko Goma.Idadi ya waliofariki na kujeruhiwa inaongezeka na hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya. Padre Faustin Mbara,paroko wa Sake,alielezea hali ya kutisha.

Stanislas Kambashi,SJ na Angella Rwezaula – Vatican.

“Kwa zaidi ya Juma moja, zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa Sake wamehamia Goma na maeneo mengine,” alisema hayo Padre Faustin Mbara, Paroko wa Parokia ya Huruma ya Mungu, iliyoko takriban kilomita ishirini kutoka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, na ambayo imezungukwa na vikundi vyenye silaha vya M23. Waasi wako kilomita 2 kaskazini, kuelekea Kimoka, na upande wa magharibi, kwenye kilima cha Kiwuli. Pia wako Rutoboko, karibu na shule ya Sekondari ya “Pain de Vie” na tishio lao “liko karibu”, Padre huyo alisema. Katika jiji lenyewe, aliendelea kwamba, kuna wapiganaji wa upinzani wa Wazalendo na askari wa kawaida wa jeshi.

Zaidi ya watu 50,000 waliokimbia makazi yao wakitafuta usalama

Wakati wakazi  wa Sake wakiwa bado majumbani mwao, mabomu mawili yalianguka karibu na parokia na kambi ya watu waliohamishwa ambayo ilikuwa imejengwa hapo, na kusababisha vifo na majeruhi wengi. Ili kutafuta makao, watu walielekea barabara ya kwenda Goma au maeneo mengine, “kwa sababu tulifikiri kwamba bomu la tatu lingeweza kutuangukia, na hivyo tukahama.” Padre huyo wa Congo alieleza kwamba, iliwakaribisha watu waliokimbia makazi yao ambao walikuwa wamekuja kutoka milimani hadi kukaa mjini. Jumatatu  tarehe 19 Februari 2024, bomu lingine lilianguka katika kitongoji cha Kaduki na kuua mtu mmoja na kujeruhi watatu, alisema Padre Mbara, ambaye pia alipata hifadhi huko Goma na kutembelea kambi hizo kila siku ili kupeleka faraja kwa wale ambao wamekaribishwa. Idadi ya watu waliohamishwa na Sake “inaweza kukadiriwa kuwa watu 50,000 au 60,000,” alisema. Baadhi wamehifadhiwa na familia, huku wengi wao wakiwa katika kambi za Mugunga, Kihuli, Bulengo na nyinginezo.

Hali ya kutisha ya kibinadamu

Pamoja na mmiminiko wa watu waliokimbia makazi yao katika kambi hizi ambazo zimesongamana sasa, mashirika ya kibinadamu yanakaribia kujaa. Caritas Jimbo inafanya  kazi na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), hususan kusambaza chakula, lakini hitaji hilo liko mbali na kutoshelezwa. Watu wengine “wametumia  Juma moja tu bila kupata chochote cha kula”, alielezea Padre  na wengine wanalala nje. Katika hali hiyo, kuna hatari pia ya kupata magonjwa kwa vile upatikanaji wa maji si rahisi na ukosefu wa usafi wa mazingira. Kuhusu hali ya usalama, serikali ya Congo imeahidi kukabiliana mashambulizi hayo na washambuliaji, ingawa “idadi ya watu bado inasubiri.” Pia kuna wasiwasi “kwa sababu katika nafasi zile zile ambapo M23 wanajikuta sasa, wanamgambo wa Kikosi cha Ulinzi  cha Taifa (CNDP) ambacho ni kikundi chenye silaha kilichoundwa na Laurent Nkunda mnamo 2007-2009 - pia walijikuta  hapo zamani wamezungukwa kwa miaka miwili, kwa hivyo kuna hofu kwamba historia hiyo inaweza kujirudia.

Mwaliko kwa Serikali ya Congo

Paroko wa Parokia ya Sake anaiomba serikali ya Congo kufanya kila linalowezekana kurejesha amani katika eneo hilo, akihimiza kutafuta sababu za msingi za mzozo unaosababisha vifo na ukiwa katika eneo hili la DRC na kutafuta suluhisho ambalo siyo mbadala bali lenye ufanisi na ya kudumu. Mwaliko kwa jumuiya ya kimataifa basi ni kuhamasishana ili kukomesha hali hii, “kwa sababu idadi ya watu inateseka kweli na mgogoro wa kibinadamu utatokea ikiwa hakuna uingiliaji wa haraka. Aidha amewaalika Wakristo ulimwenguni “kuombea kurudi kwa amani hii inayohitajika sana, ili tuweze kumfanyia Bwana kazi kwa amani”.

Hali ilivyo Mashariki mwa DRC 

Kwa takriban siku kumi, eneo la mashariki mwa DRC limekuwa uwanja wa mapigano makali kati ya jeshi la Kongo na kundi la waasi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, kulingana na ripoti kutoka kwa serikali ya Kongo na wataalamu wa Umoja wa Mataifa. Mapigano hayo yamejikita karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini. Huko Kinshasa, kama ilivyo katika miji mingine mingi nchini kote, maandamano yaliandaliwa kupinga kile Padre Mbara alichokiita “vita vilivyowekwa na mauaji ya halaiki ambayo hayakujulikana kwa miongo mitatu.” Maandamano ya mjini Kinshasa na Lubumbashi (kusini-mashariki) yalilenga Monusco, Utume wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini DRC, na Balozi za nchi za Magharibi zinazotuhumiwa kuunga mkono Rwanda.

21 February 2024, 13:48