Tafuta

Kujenga usawa kupitia ushirikiano wa kimataifa kunamaanisha,kutambua nafasi ya wanawake wanaojihusisha na ushirikiano wa kimataifa na kuwafanya kuwa chanzo cha hamasa wote wanaotaka kushiriki katika mabadiliko hayo. Kujenga usawa kupitia ushirikiano wa kimataifa kunamaanisha,kutambua nafasi ya wanawake wanaojihusisha na ushirikiano wa kimataifa na kuwafanya kuwa chanzo cha hamasa wote wanaotaka kushiriki katika mabadiliko hayo. 

Mchango wa wanawake katika ushirikiano wa kimataifa watambuliwa

Kila tarehe 25 Januari ni Siku ya kimataifa ya wanawake katika Ushirikiano wa Kimataifa,ikiwa na lengo la kutambua mchango muhimu wa wanawake katika kuhamasisha haki za binadamu,amani na maendeleo endelevu ndani ya mfumo wa ushirikiano.Azoulay(UNESCO): kutambua nafasi ya wanawake na kuwafanya kuwa chanzo cha hamasa wote wanaotaka kushiriki katika mabadiliko hayo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Siku ya kimataifa ya wanawake katika ushirikiano wa kimataifa ifanyikayo kila tarehe 25 Januari ya kila mwaka, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la  Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi ya Utamaduni, UNESCO Audrey  Azoulay alisema kujenga usawa kupitia ushirikiano wa kimataifa kunamaanisha, kutambua nafasi ya wanawake wanaojihusisha na ushirikiano wa kimataifa na kuwafanya wao kuwa chanzo cha hamasa kwa wale wote wanaotaka kushiriki katika mabadiliko hayo.

Kundi la wanawake huko Guinea Bissau
Kundi la wanawake huko Guinea Bissau

Bi. Azoulay alisema hayo kupitia Tovuti ya  UNESCO ambayo ndiyo inasimamia siku hii iliyoanzishwa na Mkutano wake Mkuu tarehe 23 Novemba 2021 kupitia azimio namba 41 C/57. Azimio hilo lilitangaza mnamo tarehe 25 mwezi Januari ya  kila mwaka kuwa Siku ya kimataifa ya wanawake katika ushirikiano wa kimataifa ikiwa na lengo la kutambua mchango muhimu wa wanawake katika kuhamasisha haki za binadamu, amani na maendeleo endelevu ndani ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa. Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO alisema tayari wanawake walio katika nafasi zinazowawezesha kushiriki katika ushirikiano wa kimataifa wamekuwa chanzo cha hamasa kwa wengine wanaotaka mabadiliko. Kaulimbiu ya mwaka huu  2024 ilikuwa ni “Usawa wa kijinsia katika kutatua dharura ya mabadiliko ya tabianchi.”

Wanawake wakiwa katika shughuli  ya pamoja ya kujiendeleza
Wanawake wakiwa katika shughuli ya pamoja ya kujiendeleza

Kwa njia hiyo lengo kuu la UNESCO ni kutambua wanawake viongozi katika mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ili kuchagiza mazungumzo kuhusu majawabu ya kimataifa dhidi ya ubaguzi wa kijinsia ambao unakwamisha hatua dhidi ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi. Halikadhalika kuhamaisha juu ya  ongezeko la uwakilishi wa wanawake kwenye nafasi za msingi za kupitisha maamuzi ambayo yanaumba na kutekeleza ajenda za ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha ushirikiano huo unafanya kazi kwa ajili ya wanawake na wasichana kupitia hatua za kuleta mabadiliko chanya ya kijinsia na mikataba.

Kundi la wanawake nchini India katika harakati za kujiendeleza
Kundi la wanawake nchini India katika harakati za kujiendeleza

Miongoni mwa wanawake viongozi katika nyanja ya ushirikiano wa kimataifa alikuwa  ni Joyce Msuya ambaye ni Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya uratibu wa misaada ya dharura. Kupitia ukurasa wake wa X zamani katika Twitter, katika fursa ya Siku hiyo Bi. Msuya aliandika: “kama mwanasayansi ninayejivunia, mwanamke na mwana ushirikiano wa kimataifa nataka kusaidia wanawake wengi zaidi waingie katika tasnia hii.”

Bi. Msuya ambaye ni Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA aliongeza kuandika kuwa: “kunahitajika wanawake wengi zaidi katika meza ya kupitisha maamuzi, hasa pindi linapokuja suala la mabadiliko ya tabianchi na mwangwi wa   siku ya wanawake katika ushirikiano wa kimatafai.”

Bi Amina Mohammed,Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Bi Amina Mohammed,Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Siku hiyo ilidhimishwa kwa kufanya  mkutano wa viongozi wanawake kwenye mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ukimulika majibu ya kimataifa katika ubaguzi wa kijinsia unaokwamisha hatua dhidi ya dharura za tabianchi. Mapendekezo ya mkutano huo yatawasilishwa kwenye mikutano ikiwemo ule wa Umoja wa Mataifa kuhusu Muongo wa Bahari utakaofanyika Barcelona, Hispania mnamo mwezi Aprili 2024, siku ya uhuru wa vyombo vya habari Mei 2024, Jukwaa la Sayansi duniani, Novemba 2024 na Mkutano wa kimabatia  kuhusu bahari mwezi Juni mnamo mwaka 2025.

Siku ya wanawake katika ushirikiano na kimataifa
06 February 2024, 13:27