Tafuta

Mama akimpatia mtoto chakula ambapo watoto wanakabiliwa na utapiamlo wa kukithiri huko Rafah kaskazini mwa Gaza. Mama akimpatia mtoto chakula ambapo watoto wanakabiliwa na utapiamlo wa kukithiri huko Rafah kaskazini mwa Gaza. 

UNICEF/WFP/WHO:Maisha ya watoto yanatishiwa na ongezeko la utapiamlo,Ukanda wa Gaza

Hali ni mbaya sana kaskazini,mtoto 1 kati ya 6 chini ya miaka 2 ana utapiamlo;kati ya hawa 3% wanahatarisha maisha yao.Huko Rafah,kusini Gaza,zaidi,5% ya watoto chini ya miaka 2 wana utapiamlo.95% ya familia wanapunguza milo na sehemu ya 64% ya familia wanakula mlo 1 tu kwa siku. Zaidi ya 95% ya familia wamepunguza kiwango cha kula watu wazima ili kuhakikisha watoto wadogo wanapata chakula.

Na Angella Rwezaula- Vatican.

Ongezeko kubwa la utapiamlo miongoni mwa watoto na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika Ukanda wa Gaza unaweka afya zao hatarini, kulingana na uchambuzi wa kina uliochapishwa na Global Nutrition Cluster yaani Kikundi cha Lishe Ulimwenguni. Wakati mzozo unaoendelea katika Ukanda wa Gaza ukiingia katika Juma lake la 20, chakula na maji salama yamepungua sana na agonjwa yameenea, na kuathiri lishe na kinga ya wanawake na watoto na kusababisha kuongezeka kwa utapiamlo. Ripoti hiyo ya “Udhaifu wa Lishe na Uchambuzi wa Hali” huko Gaza imegundua kuwa hali ni mbaya zaidi katika Ukanda wa Kaskazini mwa Gaza, ambao umekaribia kukataliwa kabisa na misaada kwa majuma. Uchunguzi wa lishe uliofanywa katika makazi na vituo vya afya kaskazini uligundua kuwa 15.6% - au mtoto 1 kati ya 6 chini ya miaka 2 - wanakabiliwa na utapiamlo wa kukithiri. Kati ya hawa, karibu 3% wanakabiliwa na utapiamlo wa kukthiri, aina inayohatarisha maisha ya watoto wenye utapiamlo, ambayo inawaweka watoto wadogo katika hatari kubwa ya matatizo ya afya na kifo ikiwa hawatapata huduma ya haraka. Kwa kuwa takwimu hizo zilikusanywa  mnamo mwezi Januari, huenda hali ikawa mbaya zaidi leo hii.

UNICEF imekuwa ikionya juu ya tishio la kukosa misaada huko Rafah

Ukaguzi kama huo katika Ukanda wa kusini mwa Gaza, Rafah, ambako misaada imekuwa ikipatikana zaidi, iligunduliwa kuwa 5% ya watoto chini ya miaka 2 walikuwa wakikabiliwa na utapiamlo mkali. Huu ni ushahidi wa wazi kwamba upatikanaji wa misaada ya kibinadamu ni muhimu na unaweza kusaidia kuzuia matokeo mabaya zaidi. Pia wanasisitiza wito wa mashirika ya kulinda Rafah kutokana na tishio la operesheni kali za kijeshi. “Ukanda wa Gaza utashuhudia mlipuko wa vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika ambavyo vitazidisha kiwango ambacho tayari kisichoweza kuvumilika cha vifo vya watoto huko Gaza,”alisema Ted Chaiban, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Watoto UNICEF wa Utekelezaji wa Kibinadamu na Operesheni za Ugawaji. “Tumekuwa tukionya kwa majuma kadhaa kwamba Ukanda wa Gaza uko ukingoni mwa shida ya lishe. Ikiwa mzozo hautaisha sasa, lishe ya watoto itaendelea kuporomoka, na kusababisha vifo vinavyoweza kuepukika au matatizo ya kiafya ambayo yataathiri watoto huko Gaza kwa maisha yao yote na yatakuwa na matokeo yanayoweza kutokea kati ya vizazi.

Ongezeko la utapiamlo Ukanda wa Gaza kutokana na ukosefu wa chakula

Kabla ya vita katika miezi ya hivi karibuni, utapiamlo uliokithiri katika Ukanda wa Gaza ulikuwa nadra, huku 0.8% tu ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wakikabiliwa na utapiamlo mkali. Kiwango cha juu cha utapiamlo cha 15.6% kati ya watoto chini ya umri wa miaka 2 kaskazini mwa Gaza kinaonesha kupungua kwa kasi. Kupungua kwa hali hiyo ya lishe ya idadi ya watu katika miezi mitatu haijawahi kutokea ulimwenguni. Kuna hatari kubwa kwamba utapiamlo utaendelea kuongezeka katika Ukanda wa Gaza kutokana na ukosefu wa kutisha wa chakula, maji, afya na huduma za lishe: Asilimia 90 ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 2 na 95% ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wako katika umaskini mkubwa wa chakula - ikimaanisha kuwa wamekula vikundi viwili au chache vya chakula katika siku iliyopita - na chakula ambacho wanapata hakina thamani ya lishe.95% ya familia hupunguza milo na sehemu, na 64% ya familia hula mlo mmoja tu kwa siku. Zaidi ya 95% ya familia zilisema walipunguza kiwango cha chakula cha watu wazima ili kuhakikisha kuwa watoto wadogo wana chakula cha kula.

Hakuna maji yanayofaa na maji salama kwa watu kila siku(WFP)

“Ongezeko kubwa la utapiamlo tunaloona huko Gaza ni hatari na linaweza kuzuilika kabisa. Watoto na wanawake, hasa, wanahitaji kuendelea kupata vyakula vyenye afya, maji safi, na huduma za afya na lishe. Ili hili litokee, tunahitaji maboresho madhubuti katika usalama na ufikiaji wa kibinadamu, na maeneo ya ziada ya kuingia kwa ajili ya usaidizi Gaza.”alisema Valerie Guarnieri, Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa WFP wa Operesheni za Programu.  Maji ya kunywa yasiyofaa, pamoja na maji ya kutosha kwa kupikia na usafi, huzidisha lishe duni. Kwa wastani, kaya zilizofanyiwa utafiti zilipata chini ya lita moja ya maji salama kwa kila mtu kwa siku. Kulingana na viwango vya kibinadamu, kiwango cha chini cha maji salama kinachohitajika katika dharura ni lita tatu kwa kila mtu kwa siku, wakati kiwango cha jumla ni lita 15 kwa kila mtu, ambayo inajumuisha kiasi cha kutosha kwa kunywa, kuosha na kupika. Njaa, kiu na udhaifu, na kuhara  zaidi na zaidi ni kuugua. Ripoti hiyo imegundua kuwa angalau 90% ya watoto chini ya miaka 5 wanaathiriwa na ugonjwa mmoja au zaidi ya kuambukiza. 70% walikuwa na ugonjwa wa kuhara katika majuma mawili yaliyopita, ongezeko la mara 23 ikilinganishwa na hali ya awali ya 2022.

Shirika la WHO:mifumo inayofanya kazi iimarishwe kuzuia magonjwa na utapiamlo

“Njaa na magonjwa ni mchanganyiko hatari. Watoto wenye njaa, waliodhoofika na wenye kiwewe kikubwa wana uwezekano mkubwa wa kuugua, na watoto wagonjwa, hasa wale walioathiriwa na kuhara, hawawezi kunyonya virutubisho vizuri. Ni hatari na ya kusikitisha na inatokea mbele ya macho yetu.”Alisema Mike Ryan, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Dharura wa Afya wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Bila kuongezeka kwa usaidizi wa kibinadamu, hali ya lishe huenda ikaendelea kuzorota kwa kasi na kwa kiwango kikubwa katika Ukanda wa Gaza. Huku huduma nyingi za afya, maji na usafi wa mazingira zikiwa zimezorota sana, ni muhimu kwamba zile ambazo bado zinafanya kazi zilindwe na kuimarishwa ili kuzuia kuenea kwa magonjwa na kuzuia utapiamlo usizidi kuwa mbaya.

Harakati za mashirika ya UNICEF, WFP na WHO

Mashirika ya  UNICEF, WFP na WHO yanatoa wito wa upatikanaji salama, usiozuiliwa na endelevu ili kutoa haraka msaada wa kibinadamu wa sekta mbalimbali katika Ukanda wa Gaza. Hii ni pamoja na vyakula vyenye lishe bora, vifaa vya lishe na huduma muhimu kwa watoto na wanawake walio katika hatari ya utapiamlo na walio hatarini kupata huduma na huduma za afya na lishe, hasa watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka 5. Hospitali na wahudumu wa afya lazima walindwe dhidi ya mashambulizi ili waweze kutoa huduma muhimu na matibabu kwa usalama. Usitishaji mapigano wa haraka wa kibinadamu unasalia kuwa nafasi bora ya kuokoa maisha na kumaliza mateso.

20 February 2024, 14:29