Tafuta

Papa wakati wa kukutana na wawakilishi wa Kiyahudi wa Amerika Kusini (2022) Papa wakati wa kukutana na wawakilishi wa Kiyahudi wa Amerika Kusini (2022)  (Vatican Media)

Wakuu wa Kiyahudi na wasomi wamshukuru Papa.Amepanda mbegu ya urafiki

Wakuu wa Kiyahudi ameandika barua iliyochapishwa na Gazeti la Osservatore Romano“kwa Papa Fransisko kwa kuonesha makaribisho yake yaliooneshwa kwa Wayahudi ulimwenguni kote:dhamira ya Kanisa imebadilisha jumuiya zetu, tunashukuru dhamira yake ya kupinga kikamilifu chuki dhidi ya Wayahudi na chuki ya Uyahudi.”

Roberto Cetera na Angella Rwezaula – Vatican.

Jitihada za Kanisa za kusitawisha uelewano ambapo hapo awali kulikuwa na ushindani, urafiki ambapo hapo awali kulikuwa na uadui na huruma ambapo hapo awali kulikuwa na dharau,imebadilisha jumuiya zetu na kuacha alama ya kudumu kwenye historia zetu. Katika barua yako, Baba Mtakatifu tunapata uthibitisho wa ahadi hii, ambayo inachukua umuhimu zaidi katika wakati huu ambao ukosefu wa utulivu unatishia hata uhusiano uliokuzwa kwa miongo mingi.

Waliotia saini

Ni sehemu ya barua iliyotumwa kwa Papa Francisko na baadhi ya wakuu wa Kiyahudi na  wasomi wa mazungumzo ya Kiyahudi-Kikristo, ambayo imetiwa  saini na Mkuu wa Kiyahudi:Yehoshua Ahrens (Frankfurt/Bern), Yitz Greenberg (Jerusalem/New York) na David Meyer (Paris). / Roma), pamoja na Karma Ben Johanan (Yerusalemu) na Malka Zeiger Simkovich (Chicago). Kundi hilo hilo lilikuwa tayari limemwandikia Baba Mtakatifu mnamo mwezi Novemba, 2023 kuomba ukaribu mpya kati ya Wayahudi na Wakristo baada ya mauaji ya tarehe 7 Oktoba 2023  na kuibuka upya kwa chuki dhidi ya Wayahudi na Uyahudi iliyorekodiwa katika sehemu mbalimbali za dunia.

Kufarijiwa wakati wa mateso

Tarehe 2 Februari 2024,Papa Francisko alituma barua yake:“kwa kaka  na dada wa Kiyahudi wa Israeli”,ambapo alihakikishia mshikamano wa Kanisa zima na watu wa Kiyahudi na wakati huo huo alitoa wito wa utulivu wa haraka kati ya watu wote wa kila kabila na madhehebu ya kidini wanaoishi katika Nchi Takatifu. Tarehe 14 Februari andiko hili jipya lilifika kutoka kwa wasomi wa Kiyahudi ili kumshukuru Papa kwa maneno yake yenye kuthaminiwa. “Tunafarijiwa na ukweli kwamba umewafikia Wayahudi kote ulimwenguni na hasa kwa wale wa Israeli,katika wakati huu wa mateso makubwa,pia dhamira yako ya kupinga kwa vitendo chuki dhidi ya Wayahudi na dhidi ya Uyahudi,ambao katika siku za hivi karibuni umechukua vipimo visivyojulikana kwa wengi wetu katika maisha yetu.”Wanaandika barua hiyo.

Dini zinaweza kuwa nguvu bunifu ya kufungua njia

“Maneno yatokayo moyoni huingia moyoni” wanaandika kwa shukrani, wakimnukuu Mkuu ya Kiyahudi Moshe Ibn Ezra. “Tunaishi katika wakati wa kihistoria ambao unahitaji uvumilivu,tumaini na ujasiri. Nguvu ya mabadiliko ya Nostra Aetate ni msukumo kwetu,kwani inaonesha kwamba udugu unaweza kupatikana tena hata katika mzozo mgumu zaidi.” Kwa sababu hiyo, wanahitimisha,“tunaungana na kaka na dada zetu Wakatoliki katika imani yao kwamba dini zinaweza kuwa nguvu za ubunifu, zilizojaa uwezo wa kufungua njia ambazo zingebaki kufungwa.”

Kupyaisha uhusiano wetu leo hii

Profesa Karma Ben Johanan,mratibu wa kundi la watia saini,alithibitisha kwa kwa Gazeti la Kipapa la Osservatore Romano kuwa: “ Tunakaribishwa barua ya Papa kama mwaliko wa kuimarisha mazungumzo kati ya jumuiya zetu. Takriban miaka 60 imepita tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican uanzishe enzi mpya ya uhusiano kati ya Wayahudi na Wakristo. Leo lazima tufanye upya uhusiano wetu kupitia dhiki za wakati huu wa huzuni. Pamoja na mvutano uliopo,tuna hakika kwamba uhusiano wetu una nguvu ya kutosha kuyashinda na kusonga mbele, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya.” Barua hiyo ihitimishwa kwa kukumbusha kwamba:“maumivu ya wenyeji wa nchi hii,wawe Wayahudi,Wakristo,Waislamu,au wengine,yanaathiri maisha yetu na maisha yetu ya baadaye na tunaungana nawe,Baba Mtakatifu,katika kuombea amani,mwisho wa hofu,kwa ajili ya uponyaji wa waliojeruhiwa na faraja kwa wote walio katika mateso na huzuni.”

16 February 2024, 16:00