Mikondo ya kibinadamu:Wakimbizi 97 kutoka Libya wawasili Italia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Wakimbizi 97 kutoka mataifa mbali mbali kama vile Eritrea, Ethiopia, Siria, Somalia, Sudan na Sudan Kusini waliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Fiumicino, Italia tarehe 5 Machi 2024 Alasiri kwa njia za mikondo ya kibinadamu. Katika kundi hili kuna familia ya watu watano ambapo ni Aisha mwenye umri wa miaka 30 na ana watoto wanne. Mkubwa ana umri wa miaka mitatu, kisha mapacha wa miaka miwili na mdogo ana umri wa miezi sita. Anatoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na alijaribu kufika Ulaya mara sita kuvuka Bahari ya Mediterania kutoka Libya, ambako alirejea kila mara na kukaa kwa miaka minne, akinusurika katika mazingira magumu ya kuwekwa kizuizini kwa wale wanaofika huko baada ya kuvuka jangwa.
Hii ni safari ya kwanza ya ndege kutoka Libya kwa mujibu wa itifaki iliyotiwa saini Desemba 2023 na Wizara ya Mambo ya Ndani na Mambo ya Nje ya Italia pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili na INMP na ambayo inatarajia kuwasili tena kwa watu 1500 katika miaka ijayo, ambao watakuwa wenyeji katika miundo ya majengo na familia nchini Italia. Watoto watakwenda shule huku watu wazima watachukua kozi za Kiitaliano na wataingizwa katika ulimwengu wa kazi.
Njia mpya ya maisha
Kwa mujibu wa Bwana Marco Impagliazzo, rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, akizungumza na vyombo vya habari vya Vatican vilivyokuwapo kwenye uwanja wakati wa mapokezi ya wakimbizi hao, alisema: “Ni watu walio hatarini zaidi ambao wamewasili Libya kwa miaka mingi. Waliteseka sana kutokana na kusafiri, lakini pia kutoka kizuizini. Wanatoka katika nchi za Kiafrika kwa shida sana, ni watu wanaohitaji sana msaada na ukarimu, kutafuta njia ya maisha yao ya baadaye na kutibiwa, kwa sababu wengi wao ni wagonjwa. Watakuwa hapa Italia na zaidi ya yote wataunganishwa na jumuiya zinazowakaribisha kwa njia mpya ya maisha.”
UNHCR: Libya si mahali salama
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR,) ambalo linafanya kazi nchini Libya pia katika mazingira magumu, liliwakuta watu hawa katika matatizo, baada ya miezi kadhaa ya kusubiri. Chiara Cardoletti, mwakilishi wa UNHCR kwa Italia, Vatican na San Marino alisema kuwa: “Libya si bandari salama. Tunajua kuwa kwa wakimbizi, Libya bado ni nchi ngumu sana. Hakujawa na maboresho makubwa juu ya hii hadi leo. Libya haikutia saini mkataba wa 1951 unaohusiana na wakimbizi na ni nchi ambayo bado leo ina matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji mkubwa dhidi ya wanawake na wanaume katika vituo vya kizuizini.”
Tangu mwaka wa 2017, karibu watu 8,000 wamewasili nchini Italia, Ufaransa na Ubelgiji kupitia itifaki mbalimbali zinazodhibiti mikonodo ya kibinadamu, na ambayo bado ni mojawapo ya njia chache za kisheria za kukabiliana na uhamiaji.