Tafuta

Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao Afrika Mashariki. Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao Afrika Mashariki. 

Padre Charles Kitima Aelezea Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Nchini Tanzania

Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maluum na Radio Vatican anasema mvua kubwa zinazoendelea kunyeesha nchini Tanzania zinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hii ni pamoja na mafuriko sanjari na maporomokoya udongo, hali ambayo inahitaji mbinu mkakati wa ujenzi wa makazi ya watu kwa kuheshimu mabonde pamoja na mikondo ya maji. Mipango miji inapaswa kujipanga vyema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la: Ujinga, umaskini na magonjwa ya mlipuko. Ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na shauku ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali, kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, huu ni mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Maporomoko ya tope yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao
Maporomoko ya tope yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao

Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolojia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko endelevu na ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuendelea kujikita katika mchakato wa kuragibisha elimu ya ikolojia na maendeleo fungamani ya binadamu. Amesema, changamoto na matatizo yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji toba na wongofu wa ndani pamoja na maamuzi thabiti yanayopaswa kufanywa na kutekelezwa kwa ujasiri.

Mvua kubwa zimesababisha madhara makubwa kwa watanzania
Mvua kubwa zimesababisha madhara makubwa kwa watanzania

Ni katika muktadha wa athari za mabadiliko ya tabianchi, Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha madhara yaliyojitokeza kwa siku za hivi karibuni nchini Tanzania kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyeesha katika baadhi ya mikoa pamoja na maporomoko ya udongo ambayo yamesababisha watu kadhaa kupoteza maisha na mali zao. Kuna haja kwa wataalam wa mipango miji kujipanga vyema zaidi ili kuhakikisha kwamba, watu wanajenga katika maeneo salama kwa maisha na mali zao. Mabonde yaheshimiwe na kwamba, hiki ni kipindi kwa watu wa Mungu nchini Tanzania kuonesha mshikamano wa upendo kwa kuwasaidia wale walioathirika kutokana na mvua kubwa zinazonyeesha pamoja na maporomoko ya udongo.

Mazingira Tanzania
17 April 2024, 17:39