Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataif, Bwana Antonio Guterres akihutubia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataif, Bwana Antonio Guterres akihutubia 

Guterres:Sayansi,Teknolojia,Uhandisi na Hisabati vinaivusha Afrika

Katika mijadala iliyoandaliwa na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Afrika,UNOSAA,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres alisema:“Elimu ni kichocheo cha ustawi na maendeleo ya Afrika na ndio injini ya fursa kwa vijana wa kiafrika na zaidi ya yote elimu inaunganisha waafrika na urithi wa utamaduni wa zamani huku ikiwaandaa kwa siku zijazo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

“Afrika Tuitakayo” haina budi kuungwa mkono na mifumo ya elimu ambayo Afrika inahitaji, alisema hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati wa moja ya kikao cha ngazi ya juu cha Mfululizo  wa Mijadala ya Afrika iliyokunja jamvi tarehe 30 Mei 2024 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Mlolongo huo wa mijadala uliofanyika kwa mwezi mzima ukiwa umeandaliwa na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Afrika, UNOSAA, uliojikita katika marekebisho ya mfumo wa elimu ambapo Bwana Guteress alisema mada hiyo  imekumbusha kuwa ili kuwezesha bara la Afrika kustawi, kiambato muhimu ni elimu.

Ufadhili zaidi wa mifumo ya elimu na msingi wa elimu barani Afrika

Katika kikao hicho cha tarehe 30 Mei 2024 kilichomulika Elimu kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuelekea Afrika Tuitakayo, Bwana Guterres alisema elimu ni kichocheo cha ustawi na maendeleo ya Afrika na ndio injini ya fursa kwa vijana wa kiafrika na zaidi ya yote elimu inaunganisha waafrika na urithi wa utamaduni wa zamani huku ikiwaandaa kwa siku zijazo. Hata hivyo alisema mizozo na majanga yahusianayo na tabianchi yamefanya elimu kusalia ndoto kwa mamilioni ya watoto na vijana barani Afrika, huku kukiwa hakuna walimu wenye sifa zinazotakiwa na mbinu za kufundishia zinashindwa kuwaandaa wanafunzi kwa ajira kwenye zama za dunia ya sasa hasa kwa kuzingatia umuhimu wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM. Bwana Guterres alizidi kuhamasisha juu ya ufadhili zaidi kwenye mifumo ya elimu na zaidi ya yote msingi wa mifumo ya elimu barani Afrika ijikite kwenye STEM. “Kuongeza idadi ya watoto shuleni pekee haitoshelezi, kinachohitajika ni stadi na ufahamu zaidi wa kuweza kushindana kwenye uchumi wa kisasa wa dunia,” alisema Bwana Guterres.

Mwelekeo wa STI unaweza kuchochea maendeleo ya viwanda Afrika

Naye Balozi Dennis Francis ambaye ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kuunga mkono hoja ya kuendeleza  STEM na ubia katika kuimarisha mfumo wa elimu Afrika, yeye alibainisha kuwa sayansi, teknolojia na ugunduzi (STI)  vitaziba pengo la kidijitali  na hivyo kuchochea suala la kupata elimu bora Afrika, na kuimarisha tafiti na kupunguza kasi ya wasomi wa Afrika kukimbia bara lao. “Tukiwa na mwelekeo tulioazimia, STI inaweza kuchochcea maendeleo ya viwanda Afrika na kuleta mabadiliko mapana ya kiuchumi ambayo yanaweka fursa zaidi na bora za ajira kwa watu wote,” alisema Balozi Francis. Akiendelea na hotuba yake alinukuu maneno ya Hayati Nelson Mandela ya kwamba Elimu ndio silaha yenye nguvu zaidi tunayoweza kuitumia kubadilisha dunia.”

Msingi wa dhati wa kuchukua hatua ya kisayansi,kiteknolojia na ugunduzi

Ikumbukwe kuanzia tarehe 6 Mei hadi tarehe 30 mei 2024, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani vilianza vikao vya wiki tatu kuhusu Mazungumzo ya Afrika au ADS2024 kwa kuongozwa na kauli mbi: Elimu kupitia Sayansi, Teknolojia na Ugunduzi kuelekea Afrika Tuitakayo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Msaidizi wa Katibu Mkuu na Mshauri Maalum kuhusu Afrika, Cristina Duarte alisema kuwa mwaka huu vikao hivyo vinalenga kuhamasisha hatua na kuchochea majawabu yakitumia sayansi, teknolojia na ugunduzi ili hatimaye Afrika iwe na elimu bora. “Huu kimsingi ni wito wa dhati wa kuchukua hatua,” alisema Balozi Fatima Kyari Mohammed, Mwakilishi wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa wakati akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

Changamoto kubwa ya kuunda ajira zenye hadhi Afrika

Katika mazungumzo hayo alisema kuwa  wito ni kwa nchi za Afrika kwenye Umoja wa Mataifa kupatia kipaumbele elimu kama msingi wa kusonga mbele na maendeleo. “Mpango huu unasisitiza umuhimu wa kujenga mifumo ya elimu inayoleta mabadiliko na yenye mnepo ambayo sio tu inaweza kufikiwa na watoto bali pia ni jumuishi, bora na inaendana na nyakati za sasa.” Akiwasilisha Mada ya kwanza ya ADS2024 ikiongozwa na mada ya Elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM kwa ajili ya mapinduzi ya Nne ya Viwanda, 4IR, Afrika,  ikijikita katika Kuchochea ajira zenye hadhi kwa vijana wa Afrika, Bi. Duarte alisema changamoto kubwa ni kuunda ajira zenye hadhi Afrika. “Asilimia 95 ya idadi ya watu Afrika ni vijana – hawana ajira za hadhi, ikimaanisha kwamba wakati mwingine kuwa na ajira barani Afrika si mbinu ya kukuwezesha kuondokana na umaskini,” amesema Bi. Duarte.

Lazima kutafuta njia ya kuzuia ukosefu wa utulivu 

Kuhusu ufadhili kwenye ugunduzi ili kuleta mabadiliko kwenye elimu, Mkuu huyo wa OSAA alisema “watu milioni 100 wasio shuleni na bila fursa ya kupata fedha. Tunaweza kukuhakikishia kwamba mfumo wa zamani wa ufadhili hauwezi kutatua shida hii. Kwa hiyo elimu inataka ufadhili bunifu ukipatia TEHAMA kipaumbele ili kushughulikia sual hili.” Kuhusu elimu na kujifunza kwenye maeneo yenye majanga, Bi. Duarte alisema: “ukosefu wa utulivu unaendelea kuongezeka, mizozo halikadhalika, na tunahitaji katika utungaji sera na mfumo wa msimamo wa Umoja wa Mataifa, kujadili jinsi ya kutatua ukosefu wa utulivu kwenye mizozo bila kusitisha elimu, ikimaanisha bila kufunga shule.”

Afrika tuitakayo
31 May 2024, 16:20