Papua New Guinea:Zaidi ya 40% ya waliokumbwa na maporoko ni chini ya miaka 16
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia watoto(UNICEF) linaongeza hatua yake ya dharura kufuatia maafa ya Ijumaa tarehe 24 Mei iliyopita katika jimbo la Enga, nchini Papua New Guinea, na kusababisha vifo vya mamia ya watu, kuharibu miundombinu muhimu na kuwaacha maelfu bila makazi. Hata sasa Juhudi zinaendelea za utafutaji na uokoaji zinaongozwa na Kikosi cha Ulinzi cha Papua New Guinea katika hali ngumu sana, huku ardhi ikiwa bado haijatengemaa na barabara kuharibika, na hivyo kuzuia ufikiaji wa eneo la maafa.
“Tunafanya kazi kwa karibu na mamlaka na mashirika ya jamii nchini Papua New Guinea kutoa msaada muhimu kwa waathirika wa janga hili baya,” alisema hayo Angela Kearney, Mwakilishi wa UNICEF. Sasa ni wazi kuwa zaidi ya 40% ya walioathiriwa ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 16, walioumizwa sana na kupoteza familia zao, nyumba na njia za kujikimu.”
Katika majibu ya awali, ya UNICEF ilisambaza vifaa vya usafi vilivyokuwa na ndoo, makopo ya jeri na sabuni, pamoja na leso zinazoweza kutumika tena, wipes za matumizi mbalimbali na vitu vingine ambavyo vilikuwa vimewekwa awali na Mamlaka ya Afya ya Mkoa.
UNICEF ilishiriki katika tathmini za haraka ili kubaini mahitaji mapana ya maji, usafi wa mazingira, elimu, ulinzi wa watoto, afya na lishe kwa jamii zilizoathirika. Wakati huo huo, vituo vya uokoaji, vinavyoungwa mkono na mamlaka mahalia na Jeshi la Ulinzi la Papua New Guinea, vinatoa huduma muhimu na msaada kwa watu waliohamishwa.