Rais wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje Wamefariki Dunia Kwa Ajali
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.
Ebrahim Raisolsadati maarufu kama Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wengine kadhaa wamethibitishwa kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili, tarehe 19 Mei 2024 huko Kaskazini-magharibi mwa Iran. Shirika la Habari la Serikali ya Iran IRNAA, linasema kwamba, ndani ya helikopta hiyo pia alikuwemo Ayatollah Mohammad Ali Al-e Hashem, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, na Jenerali Malek Rahmati, Gavana wa jimbo la Irani la Azabajani Mashariki. Kamanda wa kitengo cha ulinzi wa Rais, Sardar Seyed Mehdi Mousavi, pia amefariki pamoja na walinzi kadhaa na wafanyakazi wa helikopta ambao bado hawajatajwa.
Rais Ebrahim Raisi alizaliwa tarehe 14 Desemba 1960. Alianza kuongoza Iran kama Rais kuanzia tarehe 3 Agosti 2021 hadi tarehe 19 Mei 2024. Makamu wa kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad Mokhber, anatarajiwa kuchukua wadhifa wa Urais kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, makamu wa kwanza wa rais anastahili kuchukua wadhifa huo iwapo rais atafariki, kuondolewa madarakani, kujiuzulu au kuwa mgonjwa kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili.