Sudan:matumaini ya amani kutoka mazungumzo ya Nairobi,Kenya!
Na Angella Rwezaula - Vatican
Sudan Kusini ilizaliwa mnamo mwaka 2011 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoifanya kujitenga na Sudan. Miaka miwili baada ya uhuru, vita vingine vya umwagaji damu vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka mnamo Desemba 2013, ambavyo vilikomeshwa na makubaliano ya amani ya 2018. Hata hivyo, baadhi ya waasi wa upinzani hawakujiunga na makubaliano ya mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 400,000 na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao; kukosekana kwa utulivu hivyo kunaendelea kuathiri maeneo mbalimbali ya nchi.
Makubaliano ya vipengele 11
Makubaliano yenye vipengele 11 yalitiwa saini tarehe 16 Mei 2024, ambayo ni msingi wa dhamira ya pande husika katika mazungumzo, kuzingatia usitishwaji wa uhasama na kufikia mustakabali usio na ghasia nchini Sudan Kusini. Makubaliano hayo yaliyozinduliwa mnamo tarehe 9 Mei 2024, mazungumzo hayo yamepewa jina la Tumaini), na yanapatanishwa na aliyekuwa kamanda wa jeshi la Kenya Lazarus Sumbeiywo. Hasa, pande zinazohusika zinakataa ghasia kama njia ya kutatua mizozo na kuwaalika raia wote wa Sudan Kusini kushiriki katika mazungumzo yenye kujenga, kuendeleza mazingira ambayo malalamiko yanaweza kushughulikiwa kwa amani. Pia walikubali kufungua nafasi za kiraia na kisiasa na kuwawezesha wananchi kushiriki katika michakato ya amani ya kisiasa na kuheshimu, kulinda na kuhakikisha uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kujumuika.
Makabaliano yanawakilisha hatua ya kwanza ya mazungumzo yanaoendelea
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya ilisema makubaliano hayo yanawakilisha “hatua ya kwanza” katika mazungumzo yanayoendelea ambapo pande zinazozozana zimeahidi kujitolea kwao kukomesha ghasia na uhasama. Mchakato wa amani wa Nairobi ulioongozwa na Kenya ulisaidia kujadili makubaliano ya amani ya kina ambayo yalimaliza mzozo mrefu zaidi barani Afrika, Kiir alisisitiza, akikumbuka vita vya muda mrefu vya uhuru wa Sudan Kusini. “Amani hiyo ilisababisha uhuru wa Jamhuri ya Sudan Kusini mwishoni mwa kipindi cha mpito mnamo 2011. Nina imani kuwa juhudi za sasa zitaleta matokeo sawa wakati nchi inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.”