Tafuta

Siku ya Mtoto Afrika. Siku ya Mtoto Afrika.  (ANSA)

16 Juni ni Siku ya Mtoto wa Afrika

Ilikuwa ni tarehe 16 Juni 1976,maelfu ya watoto katika nchi ya Afrika Kusini walikusanyika katika mji wa Soweto kwa ajili ya maandamano yenye malengo ya kudai elimu bora,ambapo licha ya kuwa watoto lakini mamia ya watoto walipigwa risasi na kuuawa na watoto zaidi ya elfu moja walijeruhiwa.Tangu 1991 Jumuiya ya Umoja wa Afrika iliweka siku ya Watoto wa Afrika.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Siku ya Mtoto wa Afrika, ni siku inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Juni tangu mwaka 1991,  ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika (UA)katika kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano kwenye mji wa Soweto nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 1976 pamoja na kujengea jamii ule uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto wote. Kwa mwaka 2024 kauli mbiu inayoongoza maadhimishoni: “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi”. Kwa njia hiyo wazazi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kushirikiana katika ulinzi wa mtoto kwa kuhakikisha wanatenga muda wa kuzungumza na watoto na kufahamu changamoto wanazopitia ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwasaidia kufikia malengo yao kwa maendeleo ya baadaye. Watoto wako mawindoni kila eneno, wanahitaji ulinzi wetu na wajibu wetu.

Suala la watoto Afrika kusini na mwanzo wa siku ya watoto wa Afrika

Ilikuwa ni tarehe 16 Juni 1976, kwa hakika maelfu ya watoto katika nchi ya Afrika Kusini walikusanyika katika mji wa Soweto kwa ajili ya maandamano yenye malengo ya kudai elimu bora, ambapo licha ya kuwa watoto lakini mamia ya watoto walipigwa risasi na kuuawa, na watoto zaidi ya elfu moja walijeruhiwa. Kwa njia hiyo kila tarehe 16 ya kila mwaka, mataifa, Jumuiya mbalimbali na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wadau mbalimbali wenye kuguswa na nia hii ya kuwatazama watoto kwa ukaribu, hukusanyika pamoja kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto zinazowakumba watoto katika bara la Afrika. Hata hivyo tunataja  Mtoto  maana yake ni mwanadamu mwenye umri mdogo, ambaye bado siyo mtu mzima. Lakini pia kuna tofauti za mitazamo katika tamaduni mbalimbali kuhusu umri ambapo mtu anafikia hatua kuwa  sio mtoto tena. Na mara nyingi miaka kabla ya kubalehe inatazamiwa kuwa kipindi cha utoto na baadaye mtu anaitwa kuwa kijana.

Mkataba wa kiafrika juu ya haki na ustawi wa Watoto

Ukitazama Mkataba wa kiafrika juu ya haki na ustawi wa watoto(African Charter on the Rights and Welfare of the Child) uliokubaliwa na Umoja wa Afrika (UA) unamwona pia kila mtu hadi kufikia umri wa miaka 18 kuwa ni mtoto. Kuna nchi lakini zinazotofautiana kisheria kati ya watoto na vijana. Kwa hiyi Mtoto kwa ujumbìla hapewi madaraka kama mti mzima,  na yuko chini ya usimamizi na uangalizi wa wazazi au walezi kabla ya kufikia miaka 18. Hali ya mtoto inaamuliwa zaidi na utamaduni na mapokeo yake. Kuna tamaduni ambako kijana wa miaka 16 anatazamwa kuwa mtu mzima tayari. Hasa wasichana wanaolewa mapema na baadaye wanatazamwa kuwa mwanamke na mama kamili hata wakiwa na umri mdogo tu. Na ndiyo maana janga la watoto wakike kuozwa mapema linatawala katika nchi nyingi duniani na ni janga.

Sheria ya kukataza ajira za watoto -Tanzania(2022)

Kwa mfano mnamo  mwaka 2022,  Tanzania iliweka sheria ya kukataza ajira za kinyonyaji kwa watoto na kuwataka “kila mwajiri kuhakikisha mtoto aliyeajiriwa analindwa dhidi ya ubaguzi au vitendo vyenye athari kwake kwa kuzingatia umri na uwezo wake.”https://www.lrct.go.tz/uploads/documents/sw-1665644272-Sheria%20ya%20Mtoto.pdf. Katika mazingira ya wakulima au wafugaji mtoto mtoto anategemewa kufanya kazi kulingana na nguvu zake; anaweza kupewa wajibu kamili hata kama kisheria anatazamwa kuwa mtoto bado. Kwa lugha mbalimbali katika uhusiano na wazazi wake mtu anaendelea kuitwa mtoto hata kama ameshakuwa mtu mzima na ameshazaa mwenyewe. Sheria hiyo pia inakataza kumfanya mtoto ukatili, unyama , vitendo visivyo vya kibiadamu au udhalilishaji unayhsisha matendo ya kimila yanayoondoa utu wa mdu ay kuathiri ustawi wa akili na maumbel yake. Kwa maelezi zaidi rejea(Sheria ya Mtoto Tanzania Posted on 13th Oct 2022).

Siku ya kimataifa dhidi ya unyanyasaji na kazi za suruba kwa watoto

Hivi karibuni tumefanya kumbu kumbu ya Siku ya Kimataifa ya dhidi ya unyanyasaji na kazi za suruba kwa watoto inayoadhimishwa ifikapo tarehe 12 Juni ya kila mwaka. Fikirieni kulingana na matokeo yaliyochapishwa hivi karibuni na  Shirika la Wafanyakazi Duninia (ILO) na UNICEF, yanabanisha kuwa Duniani kuna watoto na vijana milioni 160 kati ya umri wa miaka 5 na 17 wanaojihusisha na utumikishwaji wa watoto(Rej.https://www.vaticannews.va/sw/world/news/2024-06/ajira-ya-watoto-inanyima-utoto-kwa-watoto-milioni-160.html).Kwa njia hiyo Haki za watoto ni mojawapo kati ya vifungu vya haki za binadamu ambacho kinalenga hasa watoto. Mapatano ya kimataifa juu ya Haki za Watoto yamekubaliwa na wanachama wa Umoja wa Mataifa. Watoto wanafafanuliwa kuwa "mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane. Haki za watoto zinajumuisha haki ya kushirikiana na wazazi wote wawili, kutambuliwa kibinadamu na mahitaji ya msingi ya ulinzi wa mwili, chakula, elimu, huduma ya afya, na sheria zinazofaa kwa ukuaji wa mtoto, haki za kiraia za mtoto, uhuru wa kutokubaguliwa kutokana na rangi, jinsia, asili ya kitaifa, ulemavu, dini, kabila au sifa nyingine. Vile vile tafsiri ya haki za watoto zinalenga zaidi kuwapa watoto kuwa huru kimwili, kiakili na kimihemko kutokana na dhuluma na unyanyasaji. tafsiri nyingine ni pamoja na malezi na utunzaji wa mtoto.


Haki ya kuishi

Hii inaanza pale mama anapopata ujauzito. Kukua vizuri kwa mimba kunategemea afya, lishe na mazingira anamoishi mama. Pia kuishi kwa mtoto baada ya kuzaliwa kunategemea upatikanaji wa mahitaji ya msingi, ambayo ni chakula cha kutosha na chenye ubora unaotakiwa, huduma bora za afya na ulinzi toka kwa wazazi, jamii na Serikali. Vifo vya watoto wadogo hutokana na ukosefu wa moja ya mahitaji tajwa hapo juu.

Haki ya kuendelezwa

Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania, maendeleo ya mtoto yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii. Ili mtoto aweze kukua vizuri anahitaji kutunzwa, kuongozwa na kulelewa katika misingi mizuri. Mathalani, kuendelezwa kwa mtoto kimwili ni kukua kimaumbile na uzito kwa uwiano wa umri. Hali hii inategemea lishe na huduma bora za afya ikiwemo kupatiwa chanjo zote muhimu na upatikanaji wa viinilishe vyote muhimu. Maendeleo ya mtoto yanahitaji jitihada toka kwa mzazi, jamii na Serikali kwa pamoja.

Haki ya kulindwa

Inahusu kuzuia vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto katika hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa. Mathalani, mtoto anahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizowiana na umri wake, kudhulumiwa mali hasa kwa watoto yatima, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, utoaji mimba wa makusudi, kuonewa nk. Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania pia inasisitiza juu ya ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa mtoto ikiwemo kukeketwa, kulazimisha kuolewa/kuoa katika umri mdogo, ubakaji, nk.

Haki ya kushiriki

Ushiriki wa mtoto unapatikana pale mtoto anapopewa nafasi kikamilifu katika kutoa mawazo, kushiriki katika maamuzi ya masuala yanayohusu maendeleo yake, nk. katika hatua mbalimbali za ukuaji wake. Kitaalamu hatua za ushiriki wa mtoto huanza rasmi kuanzia umri wa miaka mitatu hadi anapokuwa mtu mzima. Misingi ya ushiriki wa mtoto huzingatia umri na aina ya masuala anayopaswa kushirikishwa.

Haki ya kutobaguliwa

Ubaguzi wa mtoto umegawanyika katika makundi mbalimbali, katika yote yapo makundi makuu mawili. Ubaguzi wa kijinsia ambao mtoto wa kike au wa kiume anaweza kubaguliwa na wazazi, walezi au jamii pia. Upo ubaguzi unaotokana na hali yake ya kimaisha kama vile utajiri au umasikini, ulemavu, ugonjwa, uyatima na jinsi anavyoonekana mbele za watu. Mfano wa kuumiza ni ubaguzi wa kimfumo ambapo katika mataifa mengi kama vile Tanzania. takwimu zinaonesha kwamba ni asilimia moja tu ya watoto wenye ulemavu wanoandikishwa kujiunga na elimu ya msingi. Hii inaathiriwa na mtazamo wa kijamii dhidi ya watoto hawa kwani wazazi huwafungia ndani ili kuficha aibu na hivyo kuwanyima fursa ya kupata elimu.

Siku ya Mtoto Afrika

 

16 June 2024, 16:06