Guterres:Tushtue maono mapya kulinda bahari yetu tunayoitegemea
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kila tarehe 8 Juni ya kila mwaka Umoja wa Mataifa unaadhimisha Siku ya Bahari Duniani, ambapo ujumbe ulikuwa na kauli mbiu: “Shtua Maono Mapya ya hatua kwa ajili ya bahari yetu,” kwa kulenga udharura wa kuimarisha kwa kina afya ya bahari kwani ina jukumu la kuendeleza na kuimarisha uhai duniani. Katika ujumbe wake wa siku hiyo adhimu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres alisema kuwa: “licha ya bahari kuwa na jukumu hilo, bado iko kwenye matatizo na kwamba na sisi binadamu ndio wa kulaumiwa.” Mabadiliko ya tabianchi yanachochea ongezeko la kina cha maji ya bahari na kutishia uwepo wa nchi zinazoendelea za visiwa vidogo, halikadhalika jamii zinazoishi maeneo ya pwani. Maji ya bahari yamekuwa na viwango vya juu vya joto vilivyovunja rekodi na kuchochea matukio ya hali ya hewa ya kupindukia yanayotishia kila mtu.
Shughuli za utalii wa Bahari
Bwana Guterres aliendelea kusema kuwa maji ya bahari yanazidi kuwa na tindikali na kuharibu matumbawe na kuharibu uhusiano muhimu wa upatikanaji wa chakula huku utalii wa bahari ukitishiwa halikadhalika mbinu za kujipitia vipato kwa jamii za maeneo ya pwani. “Shughuli zisizo endelevu za kuendeleza maeneo ya pwani, uvuvi kupindukia, uchimbaji wa madini kwenye kina kirefu cha bahari, uchafuzi wa mazingira na utupaji wa taka za plastiki baharini vyote vinasababisha mvurugano wa mfumo anuai wa baharini duniani kote,” alisisistiza Katibu Mkuu.
Kuna nuru ya matumaini
Hata hivyo Katibu Mkuu alibainisha kuwa, kuna nuru ya matumaini, akitaja makubaliano yaliyopitishwa mwaka jana na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Sheria ya Baharini kuhusu Uhifadhi na Matumizi Endelevu ya Maeneo ya Baharini yaliyo chini ya Mamlaka ya Kitaifa, akisema, ni “Mkataba mpya muhimu zaidi wa kuwahi kupitishwa katika miongo kadhaa kuhusu usimamizi wa bahari.” Tumaini lingine ni mchakato unaoendelea wa kuandaa mkataba wenye nguvu kisheria wa kutokomeza uchafuzi utokanao na plastiki ambao ni fursa nyingine ya kusongesha lengo letu la pamoja la kulinda bahari yetu. Alitaja pia tumaini lingine kuwa ni maoni ya hivi karibuni kwenye Mahakama ya Kimataifa kuhusu sheria za Bahari akisihi nchi zichukue hatua kupunguza, kudhibiti na kuzuia uchafuzi wa bahari unaotokana na utoaji wa hewa chafuzi.
Tushirikiane kulinda bahari zetu
Katibu Mkuu alisema mkutano wa mwaka huu wa viongozi kuhusu Zama zijazo na mkutano wa mwakani 2025 huko Ufaransa kuhusu Bahari ni fursa nyingine za kuahidi kurejesha na kulinda viumbe vya baharini na mifumo anuai ya pwani. “Sasa ni wakati wa serikali, wafanyabiashara, wawekezaji, wanasayansi na jamii kushirikiana kulinda bahari yetu. Na katika siku ya kimataifa ya bahari hebu na tuitikie wito wa ujumbe wa mwaka huu na tushtue maono mapya ya hatua kwa ajili ya bahari yetu.” Alihitimisha.