Mgogoro wa Sudan:taadhari ya WHO kuhusu kushambuliwa kwa hospitali muhimu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Shambulio kubwa lililofanywa na wanamgambo wa Rapid Support Forces Msaada wa Haraka (RSF) mwishoni mwa Juma lililopita katika mji wa Al Fasher kaskazini mwa Sudan limelazimisha kufungwa kwa hospitali kuu inayotegewa katika eneo hilo na hivyo kusababisha kupungua upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha. Hii ni ripoti iliyotolewa tarehe 10 Juni 2024 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni,(WHO.) Kwa mujibu wa taarifa za WHO, Wizara ya Afya ya Sudan na Shirika lisilo la kiserikali la Madaktari Wasio na Mipaka(MSF)walilazimika kuifunga hospitali hiyo kubwa pekee inayotoa huduma za upasuaji katika El Fasher nzima baada ya wanamgambo hao wa Rapid Support Forces (RSF) kuingia ndani ya hospitali na kufyatua risasi kisha wakaiba vifaa tiba na gari la wagonjwa.
WHO imelaani vikali shambulizi dhidi ya huduma za afya
WHO Sudan imeeleza kusikitishwa na shambulio hilo na wamesema: “Kufungwa kwa hospitali hiyo kufuatia shambulio hilo kumeziongezea hospitali nyingine mbili mzigo zaidi ya uwezo wake.” Pia WHO imelaani “shambulio lingine” kwenye kituo cha afya huko Wad Al-Nura katika jimbo la Al-Jazirah kusini mwa Khartoum, ambalo lilisababisha kifo cha muuguzi ambaye alikuwa zamu akihudumia wagonjwa wakati huo. “WHO inalaani vikali mashambulizi dhidi ya huduma za afya.” WHO Sudan imeeleza kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X kuwa: “Wahudumu wa afya na wagonjwa hawapaswi kuhatarisha maisha yao ili kutoa na kupata huduma za afya.” Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesisitiza ikiwa ni siku chache pia baada ya shambulio katika moja ya vijiji nalo likiripotiwa kutekelezwa na wanamgambo wa RSF wakitumia mizinga mikubwa kushambulia kijiji na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100.
Uporaji na ukatili nchini Sudan ukome
Hata hivyo naye Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada siku ya Jumatatu tarehe 10 Juni 2024 alishutumu shambulio la Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) katika hospitali ya Al Fasher nchini Sudan, iliyoko kaskazini mwa Darfur. Kwa mujibu wa Martin Griffiths aliandika kwenye X: “Machafuko yanayoongezeka katika Al Fasher ya Sudan yanatoa pigo kubwa kwa raia walio katika mazingira magumu zaidi." Bwana Griffiths aidha alisema: "kushtushwa na habari za shambulio la RSF kwenye Hospitali ya Kusini na kuwa mapigano, uporaji na ukatili tunaouona nchini Sudan mara kwa mara lazima ukome sasa."
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mzozo wa Sudan ulioanza mwezi Aprili 2023 umesababisha vifo vya zaidi ya watu 16,000, watu karibu milioni 10 kukimbia makazi yao, na kuwaacha zaidi ya watu milioni 25 wakihitaji msaada wa kibinadamu, na kuifanya kuwa mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya kukimbia na njaa duniani. Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza tawala na kundi la wanamgambo la RSF.