Siku ya Usalama wa Chakula Duniani:kila mtu awajibike
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kila tarehe 7 Juni, ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula,siku ambayo inajikita kumulika matukio mbalimbali ya usalama wa chakula katika pande zote za ulimwengu. Kwa mwaka huu 2024, maadhimisho hayo yameongozwa na kauli mbiu inayosisitiza umuhimu wa kuwa tayari kwa matukio ya usalama wa chakula. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo(FAO)limebainisha kuwa tani milioni 931 sawa na asilimia 17 ya chakula kilichozalishwa, kiliishia kwenye mapipa ya taka ya kaya, wauzaji, migahawa na wadau wengine wa chakula.” Wakati huo huo, watu milioni 811 wana njaa na milioni 132 leo hii wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na lishe bora. Shirika hilo lilisisitiza kuwa “chakula kisichotumiwa hupoteza rasilimali kama vile ardhi, maji, nishati, udongo, mbegu na pembejeo zingine zinazotumika kwa uzalishaji wake.” Kwa mujibu wa mamlaka ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula (INFOSAN), inaeleza kuwa “usalama wa chakula ni pamoja na kutafuta njia sahihi za kuhifadhi na kufanya upya uzalishaji wa chakula kilichoisha matumizi, na hii inaweza kutupilia mbali tatizo la njaa duniani.”
Kwa njia hiyo FAO ilizindua mfumo wenye zana za kusaidia wale wote wanaofanya kazi katika sekta ya chakula kuzingatia viwango vya kimataifa vya usafi wa chakula. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO)katika fursa hiyo ya siku lilifafanua matukio ya usalama wa chakula kuwa “ni hali ambapo hatari ya afya inayotokana na matumizi ya chakula inapothibitishwa, ingawa kuwa tayari kudhibiti matukio ya usalama wa chakula kunahitaji juhudi za kujitolea kutoka kwa watunga sera, mamlaka ya usalama wa chakula, wakulima na waendeshaji biashara ya chakula na watumiaji pia wanaweza kuchukua jukumu kubwa.”
Katika kuthibitisha ukubwa wa tatizo la usalama wa chakula, WHO aidha ilieleza kuwa “kila mtu mmoja kati ya watu 10 anaugua kutokana na kula chakula ambacho si salama, na takribani watu 420,000 duniani kote hufa kila mwaka baada ya kula chakula kilichochafuliwa na watoto chini ya umri wa miaka 5 hubeba asilimia 40 ya mzigo wa magonjwa ya chakula, na vifo 125,000 kila mwaka.”
Mnamo mwaka 2004, FAO kwa kushirikiana na WHO ziliunda Mtandao wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula (INFOSAN) kama wadau wakati wa matukio ya usalama wa chakula na uripoti dharura za kimataifa ili kufanya hesabu ya matukio ya usalama wa chakula kila mwaka na kufanya tathmini ya jinsi gani ya kuepukana na matukio hayo ya usalama wa chakula duniani. Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limetoa wito wa kuwepo kwa lishe bora zaidi ya afya na uwiano katika Ulaya na Asia ya Kati.
Je, unajua?
-Chakula kisicho salama chenye bakteria hatari, virusi, vimelea au vitu vya kemikali husababisha zaidi ya magonjwa 200?
-Makadirio ya hivi karibuni yanaonesha kuwa athari za chakula kisicho salama hugharimu uchumi wa chini na wa kati karibu dola za Kimarekani bilioni 95 katika uzalishaji unaopotea kila mwaka?
-Mienendo bora ya usafi katika sekta ya chakula na kilimo husaidia kupunguza kuibuka na kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na vyakula?
Kwa njia hiyo Usalama wa chakula una jukumu muhimu katika kuhakikisha kuwa chakula kinabaki salama katika kila hatua ya mnyororo wa chakula - kuanzia uzalishaji hadi kuvuna, usindikaji, uhifadhi, usambazaji, njia yote hadi maandalizi na matumizi.
Je Serikali zifanye nini kuhakikisha usalama wa chakula?
Ili kukabiliana na tatizo hili, FAO imependekeza kwamba serikali zianzishe na kusimamia mipango ya kitaifa ya kukabiliana na dharura ya usalama wa chakula, zihakikishe kuna njia iliyoratibiwa katika mashirika ya serikali na mamlaka ya kitaifa ikijumuisha taratibu za kupashana habari haraka pindi matukio ya usalama wa chakula yanapotokea, na kutoa taarifa sahihi na za wazi kwa washika dau wakati wa matukio ya usalama wa chakula na uripoti dharura za kimataifa kwa mtandao wa mamlaka ya kimataifa ya usalama wa chakula (INFOSAN).