Uchafuzi wa hali ya hewa unasababisha vifo kila kunapokucha. Uchafuzi wa hali ya hewa unasababisha vifo kila kunapokucha.  (AFP or licensors)

Uchafuzi wa hewa wasababisha vifo zaidi ya watu milioni 8 duniani

Kwa sasa uchafuzi wa hewa ni sababu ya pili kwa kusababisha vifo,kupita tumbaku na lishe duni.Miongoni mwa waliokufa kwa sababu ya hewa chafuzi ni watoto wa umri wa chini ya miaka 5.Kupikia kuni na mkaa ndani ya nyumba ni moja ya visababishi vya vifo vingi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ripoti mpya ya kina inayoonesha athari hasi ya hewa chafuzi kwenye afya imetolewatarehe 19 Juni 2024  nchini Marekani huku ikiweka bayana kuwa uchafuzi wa hewa umeibuka na kushika nafasi ya pili duniani kama kihatarishi kinachoweza kusababisha kifo. Ripoti hiyo kwa kupewa jina la Hali ya Hewa Duniani au SoGA, imetolewa katika majimbo ya Massachussets na New York nchini Marekani na taasisi ya Health Effects au HEI kwa ushirikiano kwa mara ya kwanza na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. Kwa mujibu wa SoGA inasema mnamo  mwaka 2021 watu zaidi ya milion 8 walikufa kwa sababu ya hewa chafuzi. Ripoti inasisitiza ongezeko la madhara zaidi ya hewa chafuzi kwa afya ya wakazi wa dunia na kwamba imezidi hata tumbaku na lishe duni kwenye uwezekano wa kusababisha vifo.

Tazama miji inavyokuwa na hali chafu
Tazama miji inavyokuwa na hali chafu

Ikimulia watoto, ripoti hiyo ilionesha jinsi gani hewa chafuzi inavyoathiri vibaya watoto kwani takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kuwa zaidi ya watoto 700,000 waliokuwa na umri wa chini ya miaka mitano walikufa kwa kuvuta hewa chafu. Kwa njia hiyo “Hii ina maana hewa chafuzi imezidi hata hatari ya mtoto wa umri huo kufa kwa utapiamlo. Moshi wenye hewa chafu ndani ya nyumba, utokanao na kupika kwa kutumia nishati inayochafua hewa umeripotiwa kusababisha vifo vya watoto 500,000 kati ya hivyo 700,000 hasa barani Afrika na Asia,” ilisema ripoti hiyo.

Ikiwa imetumia pia takwimu za ripoti ya Mzigo wa Magojwa duniani yam waka 2021, ripoti ilichambua zaidi madhara ya vichafuzi vilivyoko kwenye hewa kama vile chembechembe ndogo zaidi za hewa chafuzi au PM2.5, ambayo si rahisi kuibaini kwa macho, hewa ya Ozoni au  (O3), naitrojeni dioksaidi (NO2), na moshi ndani ya nyumba katika zaidi ya nchi 200.Ripoti ilibainisha kuwa chembe chembe hizo ndogo zimesababisha zaidi ya asilimia 90 ya vifo vyote zaidi ya milioni 8 duniani. “Chembe chembe hizi ni ndogo mno kiasi kwamba zinaweza kuingia moja kwa moja kwenye mapafu na mfumo wad amu na kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari, saratani ya mapafu na moyo kushindwa kufanya kazi,” imesema ripoti hiyo.

Mji wa Thailand unavyoonesha hali ya hewa chafuzi
Mji wa Thailand unavyoonesha hali ya hewa chafuzi

Rais wa HEL, Dk, Elena Craft akizungumzia ripoti hiyo alisema “tunatumaini SoGA itatoa taarifa na hamasa ya mabadiliko. Hewa chafu ina madhara makubwa kwenye afya. Tunafahamu kuwa kuhakikisha kuna hewa safi na kuboresha afya ya umma ni mambo yanayowezekana na yanaweza kufanikiwa.” Ripoti pia inachambua uhusiano kati ya uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi ikisema kwamba chembe chembe hizo ndogo aina ya PM2.5 ni matokeo ya kuchoma nishati kisukuku, viyoyozi vya kwenye makazi, mitambo ya makaa ya mawe, shughuli za viwanda na mioto ya nyika.

Utoaji wa hewa hiyo unapunguza ubora wa hali ya hew ana inachangia katika mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa hewa chafuzi. Matokeo yake, jamii zilizo hatarini zinabeba mzigo wa hea chafuzi na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa mara ya kwanza ripoti imechunguza madhara ya hewa ya NO2 au Naitrogeni Daioksaidi kwenye ugonjwa wa pumu kwa watoto. Hewa hii chafuzi inatoka kwenye magari na huathiri kwa kiasi kikubwa wakazi wa mijini, hasa kwenye nchi za vipato vya juu.

Uchafuzi wa hali ya hewa
Uchafuzi wa hali ya hewa

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Kitty Van Der Heijden alisema licha ya maendeleo katika afya ya mama na mtoto, kila siku takribani watoto 2,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakufa kutokana na madhara ya afya yasababishwayo na uchafuzi wa hewa. “Kutochukua kwetu hatua kuna madhara makubwa kwa kizazi kijacho, kwenye afya yao na ustawi wao. Udharura wa jambo hili haukwepeki. Ni vema serikali na sekta ya biashara wazingatie takwimu hizo na wazitumie vema ili kupunga uchafuzi wa hewa na kulinda watoto.”

Licha ya takwimu zenye kiza, SoGa inasema kuna nuru ya matumaini kwani hatua zimeanza kuchukuliwa kwani tangu mwaka 2000 vifo vya watoto vinayohusiana na hewa chafuzi vimepungua kwa asilimia 53 kutokana na hatua za kupanua huduma za nishati safi na salama ya kupikia. Halikadhalika uboeshaji wa huduma za afya, lishe bora na kuongezeka kwa uelewa kuhusu uchafuzi wa hewa majumbani. Hatua zingine maeneo yenye viwango vya juu vya uchafuzi wa hewa yanachukua hatua kama vile kufuatilia uchafuzi, kuweka kanuni kali na kusongesha matumizi ya magari yanayotumia nishati salama ya umeme mathalani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

25 June 2024, 15:10