Kuna umuhimu wa kuzuia milipuko ya magonjwa kuliko kuponya. Kuna umuhimu wa kuzuia milipuko ya magonjwa kuliko kuponya. 

WHO yakabidhi jengo la magonjwa ya mlipuko mpakani Mtukula-Tanzania

Baada ya mwaka mmoja tangu mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya virusi vya Marburg ulipotangazwa kuisha kabisa nchini Tanzania uliotokea mwanzoni mwa 2023,Shirika la WHO na Maendeleo ya Kimataifa la Marekani(USAID )hivi karibuni walikabidhi Wizara ya Afya Tanzania,Jengo maalum kwa ajili ya kuhudumia watu wanaoshukiwa kuwa na magonjwa ya kulipuka huko Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni (WHO) nchini Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), hivi karibuni limekabidhi kwa Wizara ya Afya nchini humo jengo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wanaohisiwa kuwa na magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza wanapopita katika mpaka wa Mutukula unaounganisha Tanzania na Uganda kaskazini. Kwa mujibu wa Habari za Umoja wa Mataifa (UN) zinabainisha kuwa: Hatua hii ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mapema dhidi ya milipuko ya magonjwa imekuja ukiwa umetimia mwaka mmoja kamili tangu mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya virusi vya Marburg ulipotangazwa kuisha kabisa nchini Tanzania baada ya kuwa umetokea mwanzoni mwa mwaka  2023  katika mkoa wa Kagera, kaskazini magharibi mwa nchi.

Dk. Janeth Masuma, Afisa wa Kitengo cha WHO - Tanzania cha kuzuia na kudhibiti maambukizi alisema, “ kwa kuwa na mafanikio haya makubwa ya jengo la utambuzi wa wagonjwa katika mpaka wa Mutukula kutasaidia uchunguzi wa haraka na kuwatenganisha wote wanaohofiwa kuwa na maambukizi ili kuhakikisha kuwa mipaka yote imelindwa, kulinda nchi nyingine na kuhakikisha kwamba hakuna wasafiri wowote watapeleka ugonjwa nje ya Tanzania kwa mujibu wa mapendekezo na wajibu wa afya kimataifa.”

Naye Salum Rajab Kimbau, Mratibu wa Chanjo wa Mkoa wa Kagera alieleza ilivyo faida kubwa kuwa na jengo la namna hii mpakani kwamba: “huu mradi kiujumla una faida kwenye mkoa. Tumeupokea na furaha na pia furaha hii iko upande wa halmashauri ya mkoa na nchi kwa ujumla. Mradi una sehemu mbili za matibabu na kinga. Awali tulikuwa tunatumia hema moja ambalo lilikuwa linakusanya wahisiwa wote wa kike na wa kiume lakini hata mazingira yenyewe siyo rafiki kwa maana ya joto kali lakini pia akiingia mgonjwa badala ya kupona kwa haraka au badala ya kukaa kustahimili vizuri inakuwa kazi.” Kituo hiki ni moja ya mipango mingine mingi  inayoendelea ili kuhakikisha uimarishaji wa mifumo ya afya nchini Tanzania ili kuongeza kasi ya ajenda ya afya kwa wote.

25 June 2024, 14:49