UNICEF:Joto Ulaya na Asia ya Kati liliua watoto takribani 377 kwa 2021!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Pambana na joto: afya ya mtoto katikati ya mawimbi ya joto Ulaya na Asia ya Kati ni kichwa cha Ripoti mbya inayogundua kuwa nusu ya watoto hawa walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na joto katika mwaka wa kwanza wa maisha. Watoto wengi walikufa wakati wa miezi ya kiangazi. Kulingana na ripoti iliyochapishwa tarehe 24 Julai 2024 ya Shirika la Umoja wa Matiafa la kusaidia watoto UNICE linabainisha takriban watoto 377 mwaka 2021 kulingana na uchambuzi mpya wa takwimu kutoka nchi 23. “Takriban nusu ya watoto barani Ulaya na Asia ya Kati au watoto milioni 92, tayari wanakabiliwa na mawimbi ya joto mara kwa mara katika eneo ambalo halijoto inaongezeka kwa kasi zaidi duniani. Kuongezeka kwa joto la juu kunaweza kuwa na matatizo makubwa ya afya kwa watoto, hasa wadogo, hata katika kipindi cha muda mfupi. Bila matibabu, matatizo haya yanaweza kuhatarisha maisha,” alisema hayo Regina De Dominicis, Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Ulaya na Asia ya Kati.
Mfumko wa joto unaleta madhara makubwa kwa watoto
Mfumko wa joto huwa na madhara makubwa kwa watoto, hata kabla ya kuzaliwa, na huweza kusababisha kuzaliwa kabla ya wakati, uzito mdogo, kuzaliwa mtoto aliyekufa na matatizo ya kuzaliwa. Mkazo wa joto ni sababu ya moja kwa moja ya vifo vya watoto wachanga, inaweza kuathiri ukuaji wa watoto na kusababisha idadi ya magonjwa ya watoto. Ripoti hiyo pia inagundua kuwa joto kali limesababisha hasara ya zaidi ya miaka 32,000 ya maisha ya afya miongoni mwa watoto na vijana katika eneo hilo. UNICEF inafanya kazi na Serikali, washirika na jamii ya kanda yote ili kujenga uwezo wa kustahimili mawimbi ya joto. Hii ni pamoja na kuwapa walimu, wahudumu wa afya ya jamii na familia ujuzi na maarifa yanayohitajika ili kukabiliana na mfadhaiko wa joto.
Kampeni ya Cambiamo ARIA
Tangu 2022, UNICEF Italia imekuwa ikiendeleza Kampeni ya “Cambiamo ARIA” yaani “Tubadili hewa” ili kuongeza ufahamu wa athari za mgogoro wa hali ya hewa kwa ajili ya haki za watoto na vijana na kuomba kwa haraka: kupunguzwa kwa uzalishaji wa Gesi chafuzi(CO2;) sera za mazingira zinazofaa kwa watoto na vijana; elimu ya mazingira na ushiriki wa vijana katika maamuzi ya hali ya hewa. Watoa maamuzi wana majukumu makubwa zaidi, lakini sote tunaweza kufanya sehemu yetu ili kuhakikisha sayari endelevu. Ili kutafakari juu ya uendelevu wa tabia za kila siku na kusoma ushauri wa jinsi ya kuziboresha, unaweza kushiriki katika chemsha bongo kwenye jukwaa: https://misurailtuoimpatto.unicef.it/.