Tafuta

Bi Amina akisalimiana na Sima Bahous,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake-UN Women. Bi Amina akisalimiana na Sima Bahous,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake-UN Women. 

Bi Bahous,UN Women:kufungwa kazi za UN zinatishia mstakabali wa wanawake

“Tunapendekeza Baraza la Usalama lihakikishe kuwa mipito ya uwepo wa Umoja wa Mataifa inalinda mafanikio yaliyopatikana ya usawa wa jinsia na ushiriki fanisi wa wanawake kwa njia inayowezekana.”Yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, Bi Bahous wakati akihutubia Baraza la Usalama tarehe 7 Agosti 2024 huko New York,Marekani.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, Sima Bahous wakati akihutubia Baraza la Usalama hii leo jijini New York, Marekani tarehe 7 Agosti 2024 alisema kuwa “Nina wasiwasi mkubwa na madhara yanayoweza kutokea kutokana na kasi kubwa inayoendelea ya kufunga misheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa sambamba na misheni mahsusi za kisiasa.” Alizungumza hayo katika Baraza lililokutana kwenye mkutano ulioitishwa na Sierra Leone ambayo inashika urais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Agosti, kumulika uendelezaji wa ahadi kuhusu Wanawake, Amani na Usalama katika muktadha wa kufungwa au kupunguzwa kwa operesheni za umoja wa Mataifa za ulinzi wa amani.

Kufunga operesheni wakati mgumu wa mizozo na ukosefu wa usalama

Bi. Bahous alisema uamuzi wa kufunga operesheni hizo unafanyika wakati idadi na ukubwa wa mizozo na ukosefu wa usalama vikiongezeka. “Tunapendekeza Baraza la Usalama lihakikishe kuwa mipito ya uwepo wa Umoja wa Mataifa inalinda mafanikio yaliyopatikana ya usawa wa jinsia na ushiriki fanisi wa wanawake kwa njia inayowezekana,” amesema Mkuu huyo wa UN Women. Kwa mujibu wake alisisitiza kuwa Baraza lifanye hivyo awali ya yote: “kupitisha uamuzi mara kwa mara, halikadhalika kutoa taarifa, bila kusahau kuwa na mazungumzo na serikali husika na mashirika ya kikanda yanayounga mkono shughuli za ulinzi wa amani. Pili, “Baraza liendelee kukaribisha wanawake kutoka mashirika ya kiraia kuja kutoa taarifa barazani mara kwa mara na kutoa uchambuzi wa mtazamo wao wa kijinsia. Na kwa kundi la wataalamu, mara tu misheni ya Umoja wa Mataifa kuondoka, wafanye ziara katika maeneo mahalia kufuatialia na kuripoti kuhusu hali ya wanawake na wasichana ili uchambuzi huo uweze kutumika kwenye upitishaji wa uamuzi.” Vile vile Mkuu huyo alipongeza Baraza la Usalama kwa ufadhili kamilifu akisema dhima ya Mfuko wa Ujenzi wa Amani ni muhimu kwa hilo kwani ni ushirikiano thabiti na mashirika ya kifedha ya kimataifa. Halikadhalika, mipango ya kuondoka kwa misheni iende sambamba na kuelekeza fedha kwa kazi za wanawake, amani na usalama ili kuendeleza mafanikio yaliyokuwa yamepatikana.

Bi. Pobee: Vipindi vya mpito viwekewe mipango maalum

Kwa upande wa Bi Martha Pobee, ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu kwa Afrika, aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa “kukimbilia kipindi cha mchakato wa mpito wakati kuna mazingira tete ya kisiasa, yakigubikwa na vitisho vya usalama na shaka kuhusu ulinzi, kunaweza kuharibi mafanikio makubwa ya amani yaliyopatikana, ikiwemo maendeleo ya usawa wa kijinsia.” Ni dhahiri kuwa wadau wa kitaifa wanaweza kuwa hawajiandaa kubeba majukumu ya ziada, huku msaada ukihitaji kutoka wadau wa kimataifa ambao wanaweza kuwa bado hawako tayari kufanya hivyo. Bi. Pobee ameongeza kuwa “bila ya vipindi vya mpito kuwa na mipango mahsusi, yenye ufadhili na inayojali jinsia, wanawake na wasichana watakumbwa na vikwazo. Ina maana watashindwa kupata huduma za msingi, hawatoshiriki michakato ya kupitisha uamuzi na watakuwa kwenye hatari ya kukumbwa na ghasia mpya na ukosefu wa usalama.

Mali baada ya MINUSMA kuondoka miradi ilidorora

Bi. Pobee akielendelea aliweka dhahiri juu ya mifano ya kile anachozungumza, kwa mfano nchini Mali baada ya ujumbe wa  Umoja wa Mataifa (UN) wa kulinda amani nchini humo, MINUSMA kufunga virago vyake ni kwamba miradi ya ujenzi wa amani iliyolenga wanawake na wasichana ilikumbwa na changamoto. Na huko Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kuondoka na kupunguzwa kwa walinda amani kulisababisha ombwe la usalama na kuwaacha wanawake na wasichana kuwa hatarini kushambuliwa na vikundi vilivyojihami. “ Kwa njia hiyo “Mipango hii ya kuondoka imepunguza pia uwezo wa Umoja wa Mataifa kusaidia wadau katika kutatua mizizo inayohusiana na ukatili wa kingono kwenye maeneo mahsusi ikiwemo uchunguzi, utoaji taarifa na kusaidia manusara,” aalihitimisha Bi. Pobee.

Khair: Ukatili wa kingono sasa umesamba nchini Sudan yote

Mzungumzaji kutoka shirika la kiraia, Kholood Khair ambaye ni Mkurugenzi Muasisi wa Confluence Advisory, yaani mshauri mshawishi nchini Sudan aliweka bayana kuwa mifumo ya utekelezaji wa vitendo vya ukatili wa kingono hivi sasa hauko Darfur pekee yake,  bali vitendo hivyo vimesambaa nchini kote ikiwemo mji mkuu Khartoum na Al Jazeera. “Ni dhahiri kuwa vikosi vya usaidizi wa haraka, RSF na jeshi la Sudan, SAF wamewatumbukiza wanawake na wasichana kuanzia umri wa miaka tisa hadi 60 kwenye ukatili wa kingono, uhalifu wa kivita na hakuna upande wowote umechukua hatua za dhihiri kuzuia vikosi vyake,” alisema.  Kwa kusisitiza zaidi aliongeza kuwa kutekeleza vitendo vya ubakaji, kushambulia wahudumu wa afya na hakuna uchunguzi. Matumizi ya makusudi ya vitengo vya ukatili wa kingono vinavyohusiana na mizozo  ndoa za lazima, utesaji, uporaji wa mali na watu kutoweshwa , bila kusahau utumikishaji wa watu kweye kazi vinalenga kuwajengea wananchi uoga ili wajisalimishe.

Bi. Alghali: Ikiwa UN inaondoka maisha ya wanawake na wasichana hatarini

Kikao kikiongozwa na Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi Agosti, Sierra Leone ambapo Francess Piagie Alghali, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Taifa hilo la Afrika Magharibi alizungumza kwa hadhi ya taifa lake na si kama Rais wa Baraza. Alisema uwepo mdogo wa Umoja wa Mataifa kwenye mazingira ya mizozo, kunamaanisha hata usalama kwa wanawake na wasichana unakuwa ni mdogo, na umakini wa vitendo vya ukiukwaji wa haki dhidi ya wanawake na wasichana nao unapungua, halikadhalika uwekezaji kwenye miradi ya kusongesha usawa wa jinsia.

Un Women yamulika mstakabali wa wanawake
08 August 2024, 16:31