Guterres azindua'SOS'ya kimataifa kuhusu kuongezeka kwa Bahari ya Pasifiki
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres alizindua dharura ya hali ya hewa duniani(SOS) kuhusu kuongezeka kwa bahari ya Pacifiki katika kilele cha mkutano kuhusu Visiwa vya Pasifiki, huku akifunua utafiti uliogundua bahari ya eneo hilo inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko wastani wa kimataifa. Bwana Guterres akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Tonga, Nuku’alofa, ambako yuko ziarani, alisema ongezeko la kina cha maji ya bahari linatishia paradiso hii ya Pasifiki, wito aliotoa baada ya ripoti kutoka Umoja wa Mataifa kuakisi ongezeko lisilo la kawaida la kiwango cha maji ya bahari sambamba na joto, vikichochewa na utoaji wa hewa chafuzi utokanao na nishati kisukuku.
Ripoti ya WMO
Katika Ripoti iliyotolewa tarehe 26 Agosti 2024 na shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO kuhusu Hali ya Tabianchi Kusini-Magharibi mwa Pasifiki sambamba na Ripoti ya Timu ya Hatua kwa Tabianchi kutoka Umoja wa Mataifa ikipatiwa jina “Ongezeko la Kina cha Bahari katika dunia yenye ongezeko la joto” inaonesha kuwa hali inazidi kuwa mbayá na mabadiliko katika baharini na yenye madhara makubwa. Kwa pamoja ripoti hizo zinaonesha ni kwa vipi viwango vya joto kwenye bahari kila mwezi vinaendelea kuvunja rekodi. Viwango vya kina cha maji ya bahari vinaongekeza kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka 3000 iliyopita, huku ukanda wa Pasifiki ukikumbwa na madhara makubwa zaidi. “Ripoti za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa viwango vya joto baharini na matukio ya mawimbi joto baharini ni vikubwa na vinaongezeka kwa kasi,” amesema Guterres.
Mafuriko ya maeneo ya pwani na vimbunga vyatishia visiwa
Mafuriko maeneo ya pwani, yakichochewa na ongezeko la kina cha maji ya bahari na vimbunga vinatishia visiwa vilivyoko bahari ya Pasifiki, ambako idadi kubwa ya wakazi wanaishi karibu na pwani. Viwango vya joto kwenye bahari huko kusini-magharibi mwa Pasifiki vinaongezeka mara tatu zaidi ya wastani wa kiwango cha ongezeko duniani, na kina cha maji ya bahari katika baadhi ya maeneo kinaongezeka zaidi ya sentimeta 15 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, amesema Katibu Mkuu. “Iwapo viwango vya joto duniani vitaendelea kuongezeka, madhara ya muda mrefu yanaweza kujumuisha kupotea kabisa kwa mabamba makubwa ya barafu na uwezekano wa ongezeko la kina cha maji ya bahari kwa hadi mita 20,” amesema Katibu Mkuu.
Dunia iamue haraka kupunguza madhara
Guterres anasema hali halisi hivi sasa inahitaji hatua za dharura kutoka kwa viongozi wa dunia kupunguza utoaji wa hewa chafuzi, kuongokana na nishati kisukuku na kukumbatia hatua thabiti za kuhimili tabianchi. “Bila hatua za dhahiri na mabadiliko ya haraka, gharama za kiuchumi na kibinadamu zinaweza kufikia matrilioni ya dola, huku miji ya pwani na jamii zao duniani kote wakikabiliwa na hatari kubwa.” Katibu Mkuu alisema dunia iamue haraka kupunguza madhara hayo na kuzingatia mustakabali endelevu hasa kwa maeneo yaliyo hatarini zaidi kama visiwa vilivyoko bahari ya Pasifiki. Kwa upande wa jumuiya ya kimataifa, Bwana Guterres alisema, “lazima isikie Wito wa Okoa Bahari Zetu na ichukue hatua muhimu kutatua janga la sasa kabla hali haijawa mbaya zaidi.” Akimulika mkutano wa baadaye mwaka huu wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabiachi, Katibu Mkuu alisihi nchi zihamasishe ufadhili bunifu. Nchi tajiri lazima zitimize ahadi zao ambazo ni kuongeza maradufu angalau dola bilioni 40 kila mwaka ifikapo mwaka 2025.
Mkutano wa COP29
Ikumbukwe mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi kwa Mwaka 2024(UNFCCC COP 29) utafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 22 Novemba huko Baku, nchini Azerbaigian. Tukio hili litajumuisha: kikao cha 29 cha Mkutano wa Wanachama(COP 29), mkutano wa 19 wa COP unaotumika kama Mkutano wa Wanachama wa Itifaki ya Kyoto(CMP 19) na mkutano wa sita wa COP inayojulikana kama Mkutano wa Wanachama wa Makubaliano ya Paris(CMA 6)ambao utakutana ili kukamilisha, miongoni mwa masuala mengine, mfumo wa kwanza wa uwazi ulioimarishwa na lengo jipya la pamoja lililodhibitishwa kuhusu fedha. Vipindi vya 61 vya Shirika Tanzu la Ushauri wa Sayansi na Teknolojia (SBSTA 61) na Shirika Tanzu la Utekelezaji (SBI 61)pia vitakutana. Kwa maelezo zaidi: https://unfccc.int/cop29