Tafuta

Siku ya Kimataifa ya watu wa Asili inaadhimishwa kila tarehe 9 Agosti ya kila mwaka. Siku ya Kimataifa ya watu wa Asili inaadhimishwa kila tarehe 9 Agosti ya kila mwaka.  (Renan Dantas)

Tarehe 9 Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili

"Kulinda haki za watu wa jamii ya asili za kujitenga kwa ridhaa na kuishi maeneo yao asili,"ni kauli mbiuinayoongoza Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili iliyowekwa na Umoja wa Mataifa kila Agosti 9 Agosti ya kila mwaka.Takriban jamii 200 za watu wa asili kwa sasa wanaishi katika maeneo yao waliyojitenga kwa hiari na maeneo yao ya asili.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Siku ya kimataifa ya Watu wa Kiasili, huadhimishwa kila ifikapo tarehe 9  Agosti ya kila mwaka. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni Kulinda haki za watu wa jamii ya asili za kujitenga kwa ridhaa na kuishi maeneo yao asili. Takriban jamii 200 za watu wa asili kwa sasa wanaishi katika maeneo yao waliyojitenga kwa hiari na maeneo yao ya asili. Wanaishi katika misitu ya mbali yenye utajiri wa maliasili huko Bolivia, Brazili, Colombia, Ecuador, India, Indonesia, Papua New Guinea, Peru na Venezuela. Wanachagua kuishi kwa kujitenga na ulimwengu mwingine na mtindo wao wa uhamaji unawaruhusu kushiriki katika kukusanya na kuwinda, na hivyo kuhifadhi tamaduni na lugha zao. Watu hawa wana utegemezi mkubwa kwa mazingira yao ya kiikolojia.

Mabadiliko yoyote katika makazi yao ya asili yanaweza kudhuru uhai wa wanachama binafsi na kikundi kwa ujumla. Kwa mujibu wa Brian Keane, Mkurugenzi, shirika la Ardhi ni Uhai alisema kuwa “Ujuzi walio nao watu wa kiasili kuhusu mfumo ikolojia wao ni sehemu muhimu ya suluhisho. Inahitaji kuzingatiwa katika maendeleo ya ufumbuzi halisi wa ufanisi. Kwa bahati mbaya, hiyo si kawaida.” Kuna mambo matano ambayo yanahusu Siku ya Kimataifa ya watu wa Jamii ya Asili 2024.Kwana ni Kulinda haki za watu wa jamii ya asili za kujitenga kwa ridhaa na kuishi maeneo yao asili ni nini? Mwaka 2024, fikra ya siku hii inapelekwa kwa jamii takribani 200 ya watu wa asili wanaoishi kwa hiari kujitenga na kwenye makazi ya awali. Wanaishi wakiwa wamejitenga na sehemu nyingine ya dunia, wakiishi kwa kukusanya na kuwinda. Makundi haya yanakaa katika misitu ya mbali yenye rasilimali asilia nchini Bolivia, Brazil, Colombia, Ecuador, India, Indonesia, Papua New Guinea, Peru na Venezuela.

Kwa nini wameamua kujitenga?

Makundi haya ya watu wa asili kwa makusudi wanajiepusha na jamii kuu ili kuhifadhi utambulisho wao wenyewe, pamoja na tamaduni na lugha zao.

Ni vitisho gani wanakabili jamii zinazoishi kwa hiari na katika mawasiliano ya awali?

Moja ya vitisho vikubwa kutoka kwa mawasiliano ya nje ni kuambukizwa magonjwa. Kutokana na kutengwa kwao, Wazawa hawa hawana kinga za kingamwili za kupigana na magonjwa ya kawaida. Mawasiliano yaliyolazimishwa na ulimwengu wa nje yanaweza kusababisha matokeo mabaya na kuangamiza jamii nzima. Baadhi ya vitisho vikubwa vinatokana na maisha yetu ya kila siku. Kilimo, uchimbaji madini, utalii na shinikizo la rasilimali asilia katika maeneo yao husababisha ukataji miti katika misitu ya Wazawa, kuvuruga maisha yao na kuharibu mazingira ya asili waliyolinda kwa vizazi.

Hii inamaanisha nini kwetu na kwa sayari?

Wazawa wanaoishi kwa hiari na katika mawasiliano ya awali ni walinzi bora wa misitu. Pale haki zao za pamoja za ardhi na maeneo wanayokalia zinalindwa, misitu inakuwa na mafanikio, pamoja na jamii zao. Kuhifadhi maisha yao ni muhimu pia kwa uhifadhi wa utofauti wa tamaduni na lugha. Katika ulimwengu wa leo uliojaa mawasiliano, kuwepo kwa Wazawa wanaoishi kwa hiari na katika mawasiliano ya awali ni ithibati ya mfumo tajiri na wenye utata wa ubinadamu.

Kujitenga kunawasaidia nini?

Kujitenga kwa hiari kunasaidia kulinda tamaduni, lugha, na njia za maisha za kipekee. Kama watumiaji, kufanya chaguo endelevu kunaweza kusaidia kuokoa jamii hizi kutokomea. Moja ya vitisho vikubwa kwa watu hawa wa asili ni kampuni za  uchimbaji zinazochota lithium, kobalti, na madini mengine muhimu kwa teknolojia ya nishati mbadala. Katibu Mkuu hivi karibuni alianzisha Kikundi kazi cha Mpito wa Nishati muhimu.

Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu siku hii

Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili linasisitiza haki za watu wa asili kujitawala. Wana haki ya kikundi ya kuishi kwa uhuru, amani na usalama na haki ya kutopaswa kusajiliwa katika uharibifu wa utamaduni wao. Licha ya haki yao ya utawala binafsi, wanakabiliana na changamoto za pekee mara nyingi zinazopuuzwa na ulimwengu unaozunguka .Mpito kwa uchumi wa kijani unachochea shughuli za kisheria na zisizo halali katika sekta ya uchimbaji, ikiongeza shinikizo kwenye maeneo yao. Kutokana na kujitenga kwao, hawana kinga dhidi ya magonjwa ya kawaida, maana mawasiliano yoyote na watu wa nje yanaweza kuwa na matokeo mabaya kwa afya yao. Watu wa asili wanaojitenga na mawasiliano ya mwanzo ni miongoni mwa watu wachache wa asili duniani waliolindwa kutokana na athari mbaya za ukoloni na nguvu za soko.

“Watu wa kiasili katika kutengwa na kuwasiliana mara ya kwanza wako hatarini zaidi kwa mabadiliko ya udhibiti, ambayo yanaweza kutishia maisha yao ya kimwili na kitamaduni.” Fransisco Cali Tzay, alisema Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za watu wa kiasili. Kuhakikisha ulinzi maalumu kwa haki zao za pamoja na kuhakikisha mipaka ya wazi ya maeneo ni muhimu ili kuwaruhusu kuendelea kuishi kwa amani. Na kwa upande wa Manuel Carmona Yebra, Naibu Mkuu wa Masuala ya Kimataifa na Ubunifu na Mshauri wa Mazingira na Bahari alisema: “Watu wa kiasili wamefaulu pale ambapo tumeshindwa- kuishi kwa amani na sayari. EU inasimama pamoja na watu wa kiasili na kusherehekea ustahimilivu wao na utofauti wa tamaduni zao.”

Uzinduzi wa kitabu cha mwaka 2024 kuhusu Watu wa Asili

Hata hivyo kwa watu wa asili waliweka bayana kuhusu hali yao kwenye Toleo jipya la (IW2024. Mnamo tarehe 18 Aprili 2024 wakati wa Mkutano wa 23 wa Jukwaa la Kudumu kuhusu Masuala ya Watu wa Asili, UNPFII uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, miongoni mwa mambo yaliyofanyika pia ni uzinduzi wa kitabu cha mwaka  2024 kuhusu watu wa asili kilichpatiwa jina Dunia ya Watu wa asili, au IW2024, kikiwa ni toleo la 38. Kitabu hicho hutolewa kila mwaka ambapo kwa mwaka 2024 kinamulika kwa kina haki za watu wa asili kwenye ardhi, maeneo  na rasilimali zao. Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili, UNDRIP la mwaka 2007, limetenga ibara zake nyingi kuhusu haki za ardhi, kwa kutambua kuwa hiyo ni haki ya msingi ya kibinadamu kwa watu wa asili. Mara nyingi watu wa asili katika mataifa mengi wananyimwa haki zao.

Kupitia toleo la mwaka huu la kitabu hicho, lenye kurasa 688, watu wa asili kutoka Afrika, Asia, Amerika, Karibea, Pasifiki na Ulaya wamemulikwa hususan fursa chanya zilizojitokeza halikadhalika changamoto zao kuhusu umiliki wa ardhi, maeneo yao na rasilimali umewekwa bayana. Kwa mfanonchini Cameroon, ingawa haijaridhia UNDRIP, imefanya mabadiliko ya kisheria kuhakikisha kwamba watu wa asili wanapewa wajibu wa kusimamia na kufuatiali miradi mikubwa kama vile mabwawa, barabara na madini ambayo inatekelezwa kwenye maeneo yao. Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, nako mnamo mwaka 2022 kulipitishwa sheria ya kulinda na kuhamaisha haki za watu zaidi ya milioni 1.2  wa jamii ya asili wanaoishi misituni, sheria iliyoanza rasmi kutumika mwaka 2023 ambapo serikali kwa kusaidiana na mashirika ya kiraia wanatekeleza kanuni za uhifadhi wa misitu unaohusisha watu hao wa asili. Watu hao wa asili nchini DRC wametapakaa katika majimbo yote 26 ya taifa hilo la Maziwa Makuu ambapo IW2024 inasema mapigano mashariki mwa nchi yanaathiri maisha ya watu wa asili. 

Watu wa Asili bado wananyimwa haki zao

“Mwaka 2023, utapiamlo na ukosefu wa huduma bora za afya ulisababisha vifo vya zaidi ya viongozi 20 wa jamii hiyo kwenye kambi ya Karanyuchinya pekee, sambamba na watoto mbilikimo 43 na wanawake 23,” kimesema kitabu hicho kikibaisha kuwa, “matokeo yake, mbilikimo hao wananyimwa haki yao ya kutekeleza maarifa yao ya asili, kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.” Waliotoka Rutshuru na maeneo ya Nyiragongo jimboni Kivu Kaskazini hawakuwa wamesajiliwa hivyo walinyimwa haki yao ya kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa 2023, kimesema kitabu hicho. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho, Edward Porokwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wafugaji na Watu wa Asili,(PINGO) nchini Tanzania alisema kuwa hoja ya uhifadhi wa maeneo imekuwa ‘mwiba’ kwa watu wa asili. “Tunavyozungumza sasa Tanzania ni bingwa wa uhifadhi ambapo zaidi ya asilimia 45 ya eneo la nchi ni maeneo ya hifadhi. Je hii ina maana gani kwa watu wa asili? Ina maana kuendelea kwa uwepo wao? Ina maana kupoteza mbinu za wao kuishi?.” Haya yalikuwa ni  maswali ya  Bwana Porokwa ambayo yalitakiwa kuwa na jibu. Kwa wastani nchini Tanzania suala la Watu wa Asilia kama Wamasai bado halijapata utatuzi unaofaa kutokana na kuhamishwa katika maeneo yao ya Asili.

Nchini Uganda, kwa minajili ya uhifadhi, Mamlaka ya Uhifadhi ya Uganda mwaka 2023 walifurusha watu wa jamii ya Benet na kuchoma moto nyumba 95 na kuwakamata wengine 70, ilisema IW2024, ambapo hadi sasa licha ya suala hilo kufikishwa mbele ya Mahakama ya Haki za binadamu ya Afrika, ACHPR, bado hakuna hatua iliyochukuliwa. Huko Kenya, mapema mwezi Novemba,2023 mamlaka kutoka shirika la Kenya la uhifadhi wa wanyamapori, walifurusha watu 700 wa kabila la Ogiek, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto. Tukio lilifanyika siku chache tu kabla ya kufurushwa. Kitabu kinasema kitendo cha serikali kilikuwa kinyume na uamuzi wa ACHPR unaotambua umiliki wa kabila la Ogiek kwenye ardhi yao ya asili katika msitu wa Mau. Hata hivyo kitabu kinatambua hatua kubwa zilizopigwa hadi sasa na watu wa jamii ya asili katika utetezi wa haki zao sambamba na ushirikiano wao na serikali.

SIKU YA WATU ASILI DUNIANI 9 AGOSTI
09 August 2024, 15:51