WHO yaitisha kikao cha dharura kwa sababu ya Mlipuko wa Mpox huko DRC
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mkurungenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, ameitisha kikao cha Kamati ya masuala ya dharura kufuatia ripoti za kuenea kwa ugonjwa wa homa ya nyani au Mpox nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi tarehe 7 Julai 2024, Dk. Tedros alisema “kitendo cha Mpox kusambaa nje ya DRC na uwezekano wa kuenea zaidi kimataifa na ndani na nje ya Afrika nimeamua kuitisha kikao cha Kamati ya Dharura kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za Afya.”
Mlipuko wa Mpox unaleta hofu duniani
Mkuregeniz Mkuu huyo wa WHO aidha alisema kamati hiyo itamshauri iwapo mlipuko wa sasa wa Mpox unaleta hofu duniani. “Kamati hii itakutana haraka iwezekanavyo na itaundwa na wataalamu huru kutoka nyanja tofauti tofauti duniani kote.”
Kenya na Afrika ya Kati zimeripoti uwepo wa mlipuko wa Mpox
Hata hivyo tayari serikali ya Kenya na ile ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, zimethibitisha kuweko kwa mlipuko wa Mpox kwenye nchi hizo. Nchi zingine ambako ugonjwa huo umeripotiwa ni DRC nyewe, Afrika Kusini, Cameroon, huku nchi nyingine kama Rwanda na Burundi zikiwa zimechukua hatua ya kuepuka kuibuka kwa Mpox kwenye nchi zao kutokana na kuwa jirani na maeneo yenye virusi husika.