Tafuta

Nchini Msumbiji wanaomboleza kwa sababu ya mauaji ya viongozi wa kisiasa Elvino Dias, Paulo Guambe na Venâncio Mondlane. Nchini Msumbiji wanaomboleza kwa sababu ya mauaji ya viongozi wa kisiasa Elvino Dias, Paulo Guambe na Venâncio Mondlane.  (AFP or licensors)

Msumbiji:Katibu Mkuu UN alaani kuuawa kwa viongozi wa chama cha upinzani

Katika mauaji yalitokea tarehe 19 Oktoba 2024 katika mji mkuu wa nchi hiyo,Maputo,Katibu Mkuu wa UN amelaani vikali mauaji ya Elvino Dias,mshauri wa kisheria wa mgombea urais wa Msumbiji Venâncio Mondlane na Paulo Guambe,mwakilishi wa kisheria wa chama cha siasa cha PODEMOS.Hayo yalieleza taarifa iliyotolewa na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN,Oktoba 20 New York,Marekani.

Na Angela Rwezaula – Vatican.

Kupita taarifa iliyotolewa na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dominika Mchana tarehe 20 Oktoba 2024 New York, Marekani inabainisha kuwa “Katibu Mkuu analaani vikali mauaji ya Elvino Dias, mshauri wa kisheria wa mgombea urais wa Msumbiji Venâncio Mondlane, na Paulo Guambe, mwakilishi wa kisheria wa chama cha siasa cha PODEMOS.  Bwana Farhan Haq aliandika kwamba Katibu Mkuu António Guterres anatoa pole kwa familia na wapendwa wa waliouawa. Anazitaka mamlaka kufanya uchunguzi wa haraka wa mauaji hayo na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria. “Katibu Mkuu anatoa wito kwa wananchi wote wa Msumbiji, wakiwemo viongozi wa kisiasa na wafuasi wao, kuwa watulivu, kujizuia na kukataa aina zote za vurugu kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi.” Taarifa imeeleza. Katibu Mkuu alisisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na watu wa Msumbiji na kuthibitisha uungaji mkono wake usioyumba kwa amani na utulivu katika awamu hii muhimu katika historia ya nchi hiyo.

Washambuliaji walimuua mwanasheria wa upinzani wa Msumbiji na afisa wa chama baada ya kufyatua risasi gari walimokuwa wakisafiria, na hivyo kuzua hali ya wasiwasi kabla ya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi yenye utata, Umoja wa Ulaya EU na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema. Chama kipya cha upinzani cha Podemos cha Msumbiji na mgombea wake wa urais, Venâncio Mondlane, walikataa matokeo ya muda yanayoonesha uwezekano wa kushinda kwa Frelimo, chama ambacho kimetawala Msumbiji kwa nusu karne. Walikuwa wameitisha mgomo wa kitaifa siku ya Jumatatu 20 Oktoba 2024. Kundi la waangalizi wa uchaguzi wa kiraia wa Msumbiji More Integrity lilisema shambulio hilo lilitokea katika kitongoji cha Bairro da Coop katika mji mkuu Maputo, na kuwaua wakili wa Podemos Elvino Dias na mwakilishi wa chama Paulo Guambe.

"Waliuawa kikatili yaani mauaji ya kinyama," alisema Adriano Nuvunga, mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Haki za Kibinadamu cha Msumbiji (CDD). "Dalili zinaonesha kwamba karibu risasi 10 hadi 15 zilipigwa risasi, na walikufa papo hapo." Umoka wa Ulaya (EU) ulilaani mauaji hayo "kwa maneno makali", ukitoa wito "uchunguzi wa haraka, wa kina na wa uwazi ufanyke. Katika demokrasia, hakuna mahali pa mauaji yanayochochewa na siasa," huduma yake ya kidiplomasia ilisema, na kuongeza kuwa waangalizi wake wa uchaguzi bado walikuwa nchini kutathmini mchakato unaoendelea wa uchaguzi. Kulingana na hesabu ya hivi karibuni uchaguzi, Frelimo unaongoza katika majimbo yote 11, na mgombea wake, Daniel Chapo, anatarajiwa kushinda uchaguzi lakini waangalizi wa nje wametilia shaka uaminifu wa kura hiyo. Walibainisha ripoti za ununuzi wa kura, vitisho, ongezeko la idadi ya wapiga kura katika ngome za Frelimo na ukosefu wa uwazi katika mgongano - matatizo ambayo yameathiri kura nyingi tangu Frelimo ilipoanzisha demokrasia kwa mara ya kwanza mwaka 1994 baada ya miongo miwili madarakani.

21 October 2024, 09:09