Congo,DRC:wanajeshi 4 walihukumiwa kifo kwa sababu ya kupora Parokia na uharibifu
Na Angella Rwezaula - Vatican
Wanajeshi wanne wa Congo walihukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi huko Butembo, Kivu Kaskazini (mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC), tarehe 31 Oktoba 2024. Wanajeshi hao wanne wanatuhumiwa kupora parokia ya Mtakatifu Joséphine Bakhita huko Mabambi, wakati wa hali ya kuzingirwa na wakati wa operesheni dhidi ya waasi wa eneo hilo. Askari hao walipatikana na hatia ya wizi, uporaji, uharibifu dhidi ya Kanisa, ukiukaji wa maagizo ya serikali ya kuzingirwa. Hata hivyo adhabu ya kifo ilibadilishwa kuwa kifungo cha maisha.
Mahakama imeamuru kulipwa fidia
Mahakama iliamuru kulipwa fidia kwa waathiriwa na kurejeshwa kwa bidhaa zilizoporwa, na kuwakumbusha waliopatikana na hatia haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya Kijeshi ya Kivu Kaskazini. Wanajeshi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Congo (FARDC) mara nyingi wanatuhumiwa kwa mauaji ya raia, unyanyasaji, kudai fidia na uporaji. Haya yote katika jimbo ambalo limezingirwa tangu Mei 2021 ambalo limetoa mamlaka makubwa kwa jeshi.