Tafuta

Rais Lula  akisallimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Guterres katika Mkutano wa G20 huko  Rio de Janeiro nchini Brazil. Rais Lula akisallimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Guterres katika Mkutano wa G20 huko Rio de Janeiro nchini Brazil. 

Katibu Mkuu wa UN,Guterres na Rais wa Brazil:dharura za mabadiliko ya tabianchi!

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko mjini Rio de Janeiro nchini Brazil kwa ajili ya mkutano wa mataifa 20 tajiri duniani alikutana na kuzungumza na Rais wa Brazili Luiz Inácio Lula da Silva kabla ya mkutano mjini Rio de Janeiro.Mazungumzo yao yalihusu masuala mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa,kurekebisha usanifu wa masula ya fedha wa kimataifa na kushughulikia changamoto kubwa za kimataifa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika mkutano kati ya  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antinio Guterres ambaye yuko mjini Rio de Janeiro nchini Brazil kwa ajili ya mkutano wa mataifa 20 tajiri duniani au( G20 na Rais wa Brazili Bwana Luiz Inácio Lula da Silva kabla ya kuanza kwa Mkutano huo, tarehe 16 Novemba 2024, hao wawili hao walikubaliana juu ya udharura wa kutekeleza hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Katibu Mkuu na Rais wa Brazil kwa Pamoja walisisitiza haja ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuongeza azma ya kuhakikisha mafanikio ya mkutano wa 29 wa mkataba wa nchi wanachama wa mkataba wa mkataba Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP29  ambapo pia unaendelea huko Baku hadi Novemba 222 na COP30, pamoja na kujitolea kwa malengo ya kitaifa ya kulabili mabadiliko ya tabianchi NDCs yanayoambatana na kupunguza kiwango cha joto duniani na kusalia nyuzi joto 1.5C. Katibu Mkuu alishukuru kwa mchango mkubwa wa Brazil katika ajenda ya kimataifa.

Kwa viongozi wa G20

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasihi na kuwasisitiza viongozi wa nchi 20 tajiri duniani wanaokutana mjini Rio de Janeiro nchini Brazil kushika usukani wa kushughulikia changamoto za  kimataifa kuanzia kukabili changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu. Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya ufunzi wa mkutao huo, Bwana  Guterres alisema “Kuanzia Baku hadi Brazil na kwingineko, ninaona na kusikia mada na wasiwasi unaofanana. Nyakati zetu ni za misukosuko, na tunahitaji kukimbia kwa kasi zaidi ili kukabiliana na changamoto kuu za pamoja.” Akiendelea  Bwana Guterres alisema “janga la mabadiliko ya tabianchi limeingia rekodi nyingine, na kuna uwezekano wa 2024 kuwa mwaka wa joto zaidi katika historia. Tunaona athari kila mahali. Usiangalie mbali ukame katika eneo la Amazonia na mafuriko ya kutisha kusini mwa Brazili. Wakati huo huo, migogoro inaendelea kila kona. Na suala la ukwepaji sheria limetamalaki, na ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Pia ukosefu wa usawa unaongezeka, na maendeleo ya kujikwamua na umaskini na njaa yamekwama wakati Malengo ya Maendeleo Endelevu hayazingatiwi.”

Katibu Mkuu alisema  kwamba kama hayo  hayatoshi “teknolojia mpya nazo zina uwezo usio na kifani wa wa kuwa kitu kizuri au kibaya. Na kutoweza kwetu kukabiliana na changamoto hizi na zaidi ni kuondoa imani ya watu kwa serikali na taasisi.” Kadhalika alibainisha kuwa “vitisho vinavyotukabili leo vina uhusiano wa kimataifa. Lakini taasisi za utatuzi wa matatizo duniani zinahitaji sana kuboreshwa hususani Baraza la Usalama, ambalo linaakisi ulimwengu wa miaka 80 iliyopita.”Mkuu huyo wa UN alikumbusha kuwa “mwezi Septemba, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipitisha Mkataba wa Zama Zijazo, ili kusaidia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuendeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu.” Katibu Mkuu alisema aalifika Rio na ujumbe rahisi sana kwamba:  “Viongozi wa G20 lazima waongoze. Nchi za G20 kwa ufafanuzi zina nguvu kubwa ya kiuchumi na wana nguvu kubwa ya kidiplomasia. Lazima wazitumie kushughulikia changamoto kubwa za kimataifa.” Alizitaja changamoto hizo: ni kuhusu amani, “Vita vikiendelea, watu wanalipa gharama kubwa na mbaya sana. Lazima tuchukue hatua kwa ajili ya amani.”

Amani huko Gaza kwa kusitishwa kwa mapigano mara moja, kuachiliwa mara moja kwa mateka wote, na mwanzo wa mchakato usioweza kutenguliwa kuelekea suluhisho la Serikali mbili. Pia alisema amani nchini Lebanon pamoja na usitishaji mapigano na hatua za maana za kutekeleza maazimio ya Baraza la Usalama kwa ukamilifu. Na huko  nchini Ukraine kwa kufuata Mkataba wa Umoja wa Mataifa, maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. Na amani nchini Sudan na viongozi wanaoegemea pande zinazopigana kukomesha ghasia za kutisha na mzozo wa kibinadamu unaowakabili raia wengi. Kwa njia hiyo alisema “ Kila mahali, amani inahitaji vitendo vinavyozingatia maadili ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, utawala wa sheria na kanuni za uhuru, uhuru wa kisiasa na uadilifu wa mipaka ya Mataifa. Nchi zilizo katika mazingira magumu zinakabiliwa na zahma na vikwazo vikubwa ambavyo vimeletwa kwao. Hawapati kiwango cha usaidizi wanaohitaji kutoka kwa usanifu wa kimataifa wa kifedha ambao umepitwa na wakati, usio na ufanisi na usio wa haki.”

Mkutano wa G20 huko Brazil
Mkutano wa G20 huko Brazil

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa “Mkataba wa Zama Zijazo unatoa wito wa mageuzi kabambe ili kufanya mfumo kuwa  wa uwakilishi zaidi wa uchumi wa dunia wa leo na mahitaji ya nchi zinazoendelea na zilizo hatarini. Hii ni pamoja na kupanua wigo wa sauti na uwakilishi wa nchi zinazoendelea katika taasisi za fedha za kimataifa.” Mkataba huo  hata ivyo pia “unatoa wito wa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa ukopeshaji wa Benki za Maendeleo ya Kimataifa ili kuzifanya kuwa kubwa, shupavu na bora zaidi. Ameongeza kuwa kwa hatua madhubuti za msamaha wa madeni, na kupitia upya usanifu wa madeni ili kuwezesha nchi kukopa kwa kujiamini. Ametaka kuimarisha mtandao wa usalama wa kifedha duniani ili kuhakikisha nchi zote zinalindwa wakati majanga yanapotokea na kukuza ushirikiano zaidi wa kodi. Na jumuiya ya kimataifa inaziangalia nchi za G20 kutekeleza mikataba.”

Bwana Guterres alikazia kusema kuwa: “Nina wasiwasi kuhusu hali ya mazungumzo katika mkutano wa 29 wa mkataba wa nchi wanachama kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP29 huko Baku Azerbaijan.” Kwa hiyo asisitiza kuwa “nchi lazima zikubaliane na lengo kuu la ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi ambalo linakidhi ukubwa wa changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea. Na lengo kabambe na la kuaminika ni muhimu kwa kujenga uaminifu kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea na kuhamasisha utayarishaji wa mipango ya kitaifa ya mabadiliko ya tanianchi yenye matarajio makubwa mwaka ujao. Fedha huchochea tamaa. Ninachagiza hisia za uwajibikaji wa nchi zote za G20. Sasa ni wakati wa uongozi kwa mfano halisi kutoka kwa nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani.” Katibu wa UN alisema “ kushindwa sio chaguo. Matokeo ya mafanikio katika COP 29 bado yanaweza kupatikana, lakini itahitaji uongozi na muafaka kutoka kwa G20. Na hauwezi kuja haraka. Sera za sasa za mabadiliko ya tabianchi, katika  nchi zinatusukuma kwenye ongezeko la joto la nyuzi joto 3.1 kufikia mwisho wa karne hii. Kwa njia hiyo  “Ili kuepuka maafa mabaya zaidi ya mabadiliko ya tabianchi yajayo ni lazima tupunguze ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5. Uzalishaji wa hewa chafuzi lazima upunguzwe kwa asilimia 9 kwa mwaka hadi 2030 lakini bado unaongezeka.”

G20 huko Brazil
G20 huko Brazil

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema, “Nchi zote lazima zinufaike na teknolojia zinazoibuka kama vile Akili mnemba au AI.” Alikumbusha pia kuwa “mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali uliopitishwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Zama Zijazo unajumuisha makubaliano ya kwanza ya kimataifa kuhusu utawala wa AI ambayo huleta kila nchi kwenye meza. Unataka Jopo huru la Kimataifa la Kisayansi kuhusu AI na kuanzisha mazungumzo ya kimataifa kuhusu utawala wake ndani ya Umoja wa Mataifa. Na unaomba chaguzi za ufadhili wa hiari wa ubunifu kwa ajili ya kujenga uwezo wa AI katika nchi zinazoendelea ndani ya mwaka ujao. Bwana Guterres alihitimisha kwa kusisitiza kwamba “G20 lazima iongoze kwa kuwa mfano, Hili ni jambo la msingi katika kurejesha uaminifu, imani na uhalali wa kila serikali na mfumo wetu wa kimataifa katika nyakati hizi za misukosuko. Tunahitaji kutumia kila fursa kuongoza hatua za kuleta mabadiliko kwa ulimwengu salama, wenye amani zaidi na endelevu.”

Katibu Mkuu wa Un katika G20 huko Brazil
19 November 2024, 17:16