Tanzania:Jengo moja Kariakoo jijini Dar kuanguka na kusababisha vifo na majeruhi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tanzania inaomboleza kuondokewa na Ndugu jamaa na marafiki katika ajalia. Hii ni kufuatia na kuanguka kwa Jengo moja huko Kariakoo, katika Jiji kubwa la Dar - Es -Salaam, Tanzania, Watu 13 wamefariki huku 84 hadi sasa wametolewa wakiwa hai kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa nje ya nchi. Vikosi vya uokoaji nchini Tanzania vilisema jinisi walivyofanikiwa kupata mawasiliano na watu ambao walikuwa wamenaswa Jumamosi tarehe 16 Novemba 2024, baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka. Katika harakati hizo vikosi hivyo viliweza kuwatumia hata maji, glukosi na oksijeni kupitia mapengo madogo kwenye vifusi, na wakati milio ya hapa na pale ya gonga ikisikika kutoka ndani ya jengo hilo katika eneo la soko Kuu la Kariakoo jijini humo. Baadaye manusura vile vile wakiwa hospitalini walitoa ushuhuda wao kwa kile kilichowatokea hadi kupata msaada.
Rais Samia atoa pole
Umati mkubwa wa watu waliokuwa karibu walikuwa wakipiga makofi kila walipoona timu za uokoaji zikiwasafirisha manusura kwenye machela kupita rundo kubwa la vifusi vya saruji ili kuwapeleka hospitalini. Kwa bahati mbaya watu 13 wanajulikana kufariki, huku 84 hadi sasa walitolewa wakiwa hai, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, Dominika tarehe 17 Novemba 2024. Rais Samia alisema “Waziri Mkuu sasa ataongoza "ukaguzi wa kina" wa majengo yote katika eneo la Kariakoo.” Rais aliongeza kuwa Polisi watakusanya taarifa kamili za jengo lililoporomoka kutoka kwa mmiliki wake.” Hata hivyo hadi sasa haijabainika ni watu wangapi wamebaki wamenaswa ndani na zoezi linaendelea.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema mamlaka "haitapumzika hadi tuhakikishe tumeweza kuokoa kila mtu au roho iliyonaswa kwenye kifusi". Baada ya jengo hilo kuenguka kwa mara ya kwanza saa 3:00 kwa saa za huko, Jumamosi asubuhi, 16 Novemba 2024 mamia ya washiriki wa kwanza walitumia nyundo na mikono yao wazi kuondoa uchafu kama tulivyoona kwenye vyombo vya habari vya ndani na shuhuda mbali mbali.
Operesheni ngumu
Haikuwa kitu rahisi namna ya kuwaokoa watu! Cranes na mashine nyingine nzito zililetwa baadaye kusaidia. Kwa bahati nzuri, jengo hilo lilianguka kabla ya eneo la soko kuwa na shughuli nyingi kwa sababu watu watu huwa ni wengi mno kuliko. Mamlaka bado hazijabaini sababu ya kuanguka, lakini uchunguzi unatarajiwa kuanza mara tu juhudi za uokoaji zitakapokamilika, kwa sababu, viongozi wote hata rais wamesema kwamba , “ awali ni kujali kuokoa watu na baadaye kufuatilia kilichosababisha.”Ikumbukwe Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi duniani na ripoti zinasema kuwa kanuni za ujenzi mara nyingi hazifuatwi kila wakati.
Miili 13 inaagwa tarehe 18 Novemba 2024
Hata hivyo kupitia vyombo vya habari vya ndani ya nchi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alieleza na kuwaalika wahusika kufika katika Hospitali ili Jumatatu tarehe 18 Novemba 2024 alasiri kuaga kitaifa miili ya watu 13 waliokufa katika ajali hiyo, lakini akifafanua kwamba shughuli ya uokoaji bado inaendelea hadi wahakikishe kwamba hakuna anayebaki ndani.