Tafuta

2024.12.14Wajumbe wa kamati ya Tuzo ya Zayed 2025 (kutoka kushoto):Mohamed Abdelsalam,Ngozi Okonjo-Iweala,Macky Sall,Patricia Scotland,José Luis Rodríguez Zapatero,Kadinali Peter Turkson 2024.12.14Wajumbe wa kamati ya Tuzo ya Zayed 2025 (kutoka kushoto):Mohamed Abdelsalam,Ngozi Okonjo-Iweala,Macky Sall,Patricia Scotland,José Luis Rodríguez Zapatero,Kadinali Peter Turkson  

Kamati ya Tuzo ya Zayed:Wagombea ni Mitume wa Matumaini katika ulimwengu uliojeruhiwa

Kufuatia Mkutano wao na Papa Francisko,wajumbe wa kamati ya majaji ya Tuzo la Zayed kwa Udugu wa Kibinadamu wa 2025 wanashiriki imani yao katika umuhimu wa kutambua juhudi za ajabu ambazo watu hufanya ili kukuza amani na udugu.

Na Devin Watkins na Angella Rwezaula - Vatican

Dk. Ngozi Okonjo-Iweala, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani, alishirikisha wasiwasi wa Papa kwa ajili ya ustawi wa maskini, wakati wa mkutano na waandishi wa habari  wa Vatican uliofanyika Jumamosi tarehe 14 Desemba 2024.  Kwa njia hiyo katika maoni yake Bi Okonjo alisema: “Baba Mtakatifu Francisko anasikitishwa sana na hali ya dunia na njaa ya mamilioni ya watu ambao wana utapiamlo na kutafuta chakula kwenye lundo la takataka, huku ulimwengu ukitumia kiasi kikubwa cha fedha kutengeneza silaha.

Wajumbe sita wa kamati ya waamuzi wa Tuzo la Zayed kwa Udugu wa Kibinadamu wa 2025 walikutana na waandishi wa habari katika ofisi za Baraza la Kipapa la Mawasiliano, tu mara baada ya Mkutano wao na Baba Mtakatifu Francisko. Jaji Mohamed Abdelsalam, Katibu Mkuu wa Tuzo ya Zayed kwa Udugu wa Kibinadamu, alibainisha kuwa huu ulikuwa ni Mkutano wa  20 na Papa kwa vikundi vinavyohusishwa na Hati ya Udugu wa Kibinadamu, ambayo Papa Francisko alitia saini mnamo 2019 na Sheikh Ahmad Muhammad Al-Tayyeb, Imamu Mkuu wa Al-Azhar. Kila mkutano na Papa, alisema, kumempa moyo wa kibinafsi katika juhudi zake za kukuza maadili ya udugu wa kibinadamu. "Shauku yetu ya kuendelea katika njia hii daima inafanywa upya tunapokutana na Papa Francisko," aliongeza Jaji Abdelsalam.

Kwa upande wa Kardinali Peter Turkson, alisema “Kazi ya kamati ya waamuzi ni kuteka ujumbe wa Papa wa matumaini na udugu na kuzingatia takriban wagombea 100 wa Tuzo ya Zayed ambao wanaelezea shauku  ya wanadamu ya amani kwa njia fulani katika maisha yao wenyewe. Kwa njia hiyo Kansela wa Vyuo vya Kipapa vya Sayansi na Sayansi ya Jamii, aliongeza kusema  “Jubilei ya Matumaini inapoanza, tunapaswa kukumbuka kutoingiliwa na utamaduni wa kutupa na giza linalotuzunguka.” Kardinali Turkson alisema wagombea wanaweza kuitwa "Mitume wa Matumaini," ambao wanajaribu kukuza ujumbe wa udugu kwa njia zao ndogo na kubwa.

Kulingana na Patricia Scotland, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Tuzo la Zayed ya Udugu wa Kibinadamu huruhusu ulimwengu kuzingatia watu wanaojitahidi kuinua roho ya mwanadamu. Tuzo hiyo, aliongeza, inasaidia kila mtu kutambua kwamba amani "sio tu tumaini bali ni ukweli wa kibinadamu na kwamba watu wanajitahidi kuifanikisha."

Kwa upande wa Macky Sall, Rais wa zamani wa Senegal, alikiri kwamba ulimwengu wetu umejaa ubinafsi, mizozo na migogoro. Papa Francisko, alisema, badala yake anatoa ujumbe wa "tumaini na hekima," na kuwahimiza wengine kufanya kazi kwa ulimwengu wa amani. Pamoja na Tuzo ya Zayed, aliongeza Bwana Sall, ulimwengu unapewa ujumbe wa udugu ambao unapita kati ya dini na makabila ili kufikia wema unaojaza ubinadamu.

Washiriki kadhaa wa baraza la  kuhukumu walitambua kwamba vijana leo  hii wanakabili ulimwengu uliojaa mahangaiko, huku wengi wakihangaikia mambo ambayo wazazi wao waliyachukulia kuwa ya kawaida. "Kuna watu milioni 700 ambapo milioni 300 kati yao wako katika bara la Afrika-ambao wanalala njaa, huku pesa nyingi zikitumika kununua silaha," alilalamika  Dk. Okonjo-Iweala.

José Luis Rodriguez Zapatero, Waziri Mkuu wa Zamani wa Hispania, alibainisha kuwa wakati wetu wa kihistoria umeona mizozo mingi na vita vya wazi tangu mwisho wa Vita vya Kidunia vya pili. "Tunahitaji mkakati mpya na mtazamo kwa ulimwengu wetu," alisema. "Tunahitaji sana kuhamasishana kwa ajili ya amani." Papa Francisko, aliongeza Bwana Zapatero, anaupatia ulimwengu ujumbe "jasiri" wa matumaini, amani, na huduma kwa maskini na watu wanaoteseka kutokana na migogoro. "Sisi ni familia moja ya kibinadamu," alisema. "Dini zote, itikadi zote, nchi zote ni ubinadamu mmoja."

Akitafakari maana ya udugu, Kardinali Turkson  pia alisema neno hilo linatokana na neno la Kigiriki adelphos, ambalo kihalisi linamaanisha “kutoka kwenye tumbo moja la uzazi.” "Haiwezekani kwa watu kutoka tumbo moja kuwa na historia  tofauti," alisema Kardinali huyo mzaliwa wa Ghana. "Sote tunashiriki hadhi hiyo, na lazima tuheshimu matakwa ya uhusiano wetu. Udugu wa kibinadamu unaweka msingi huo wa msingi kwa mahusiano yetu." uzo ya Zayed kwa Udugu wa Kibinadamu, alisema Kardinali Turkson, ni ukumbusho kwamba kila mtu anaweza kutafuta kuifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi. "Mtu yeyote anaweza kuwa mhusika mkuu wa amani," alihimiza.

14 December 2024, 13:10