Tafuta

Majina ya waathirika wa mauaji ya kimbari huko Srebrenica – Bosnia miaka 30 iliyopita. Majina ya waathirika wa mauaji ya kimbari huko Srebrenica – Bosnia miaka 30 iliyopita. 

Tarehe 9 Desemba ni Siku ya Kimataifa ya kumbukizi ya wathirika wa uhalifu wa mauaji

Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu na kuenzi utu wa Waathirika wa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari na Kuzuia Uhalifu inaadhimishwa kila ifikapo tarehe 9 Desemba.Mwaka 2024 inaongozwa na kauli mbiu:“Kumbukumbu na kuzuia mauaji ya kimbari.”Tukio hili linafanyika kati ya kumbukizi 2 za kihistoria:Aprili 2024,nchini Rwanda iliadhimisha miaka 30 ya mauaji ya kimbari 1994 dhidi ya Watutsi.Na mwezi Julai 2025,Bosnia na Herzegovina zitaadhimisha miaka 30 ya Srebrenica 1995.

Na Angella Rwezaula -Vatican

Tarehe 9 Desemba 2024 ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu na kuenzi utu wa Waathirika wa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari na Kuzuia Uhalifu huo katika kuadhimisha siku hii Umoja wa Matifa ulisisitiza kuwakumbuka na kuwaenzi waathirika kwa kuhakikisha uhalifu huo hautotokea tena kwa kufanya kila juhudi kuuzuia. Siku hii ilianzishwa kunako tarehe 9 Disemba 1948, ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kauli moja Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari (CPPCG), na kuwa mkataba wa kwanza wa kuratibu mauaji ya kimbari kama uhalifu na chombo muhimu cha haki za binadamu. Mwaka huu 2024 ambapo Mkataba unafikisha miaka 76,  Siku hii inaongozwa na kauli mbiu:“Kumbukumbu na kuzuia mauaji ya kimbari.”

Ofisi ya Mshauri Maalumu wa Umoja wa Mataifa Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliaandaa kuadhimisha siku hiyo kwa tukio la ngazi ya juu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni miaka 76 pia ya kupitishwa kwa Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya kimbari. Tukio la mwaka huu linafanyika kati ya kumbukumbu mbili za kihistoria kwani mwezi Aprili 2024, Rwanda iliadhimisha miaka 30 tangu mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi. Na mwezi Julai 2025, Bosnia na Herzegovina zitaadhimisha miaka 30 tangu mauaji ya kimbari ya Srebrenica ya 1995. Kwa kuzingatia uzoefu wa Rwanda na Bosnia na Herzegovina, taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa “hafla ya leo inaangazia jukumu la kumbukumbu na juhudi za kumbukumbu sio tu kuwaenzi waathirika na manusura wa mauaji ya kimbari, lakini pia kama njia madhubuti za kuzuia mauaji yajayo ya kimbari.”

Katika hafla ya tarehe 9 awali ya yote  ilianza kwa dakika moja ya ukimya kuwawezi waathirika wa mauaji ya kimbari lakini pia imeelezea baadhi ya mafanikio na changamoto zilizopo katika nyanja za kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari, kwa kuzingatia mafunzo kutoka Rwanda na Bosnia na Herzegovina, na kupitia mijadala minne.  Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya Kimbari, Bi  Virginia Gamba alisema: “Haja ya kuweka kipaumbele katika kuzuia mauaji ya kimbari, kama ilivyokusudiwa na Mkataba wa Mauaji ya Kimbari miaka 76 iliyopita, inasalia kuwa muhimu kama zamani. Kwa hili lazima azimio katika kuhakikisha kwamba juhudi za kuwakumbuka na kuwaenzi zinaungwa mkono na kwamba tuliyojifunza kutoka Rwanda na Bosnia na Herzegovina yanakuwa hali halisi. Ni kwa njia hiyo tu ndipo mambo ya hatari ya mauaji ya kimbari yanaweza kutambuliwa, kubainika na kuzuiwa mapema.”

Naye Katibu MKuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hiyo  na hasa katika kumbukumbu ya miaka 76 tangu ya kupitishwa kwa mkataba wa kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari alisisitiza kuwa: “Mkataba huo ulioundwa baada ya mauaji ya Holocaust ni ahadi ya kuzuia ukatili huo katika siku zijazo”. Hata hivyo amesema “Licha ya hayo, mauaji ya kimbari bado ni tishio kutokana na migawanyiko na ghasia zinazoendelea duniani. “ Katibu Mkuu alizitaka serikali zote “kuridhia na kutekeleza Mkataba huo, kuhakikisha uwajibikaji kwa wahalifu, na kuimarisha zana za kuzuia, ikiwemo kupitia elimu na kupambana na taarifa potofu.”  Bwana Guterres alihitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza umuhimu wa kuzingatia maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kuwa waangalifu katika kutambua dalili za mapema: “Heshima kubwa kwa waathirika na manusurika ni hatua madhubuti ili kuzuia mauaji ya kimbari yasitokee tena.”

Siku ya kuzuia mauaji ya kimbari

 

10 December 2024, 15:49