Congo DRC,waasi wa M23 wanaendelea bado kuteka miji mingine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Waasi wa M23 wanaelekea Butembo, mji wa tatu kwa ukubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wenye wakazi 150,000. Mji huo uko umbali wa kilomita 210 (maili 130) kaskazini mwa Goma, ambako waasi waliuteka mwezi uliopita, na kuua takriban watu 3,000. Kusonga mbele kuelekea Butembo kunaonesha kuwa waasi wanaendelea kupanuka kaskazini na kusini mwa Goma.
Hatari ya migogoro ya kikanda
Rwanda - inayoshutumiwa na Kinshasa, Umoja wa Mataifa na Mataifa ya Magharibi kwa kutoa msaada kwa waasi - inakanusha mashtaka yote na kuomba haki ya kujilinda dhidi ya wanamgambo wa Kihutu wanaopigana na jeshi la Congo. Kusonga mbele kwa kasi kwa M23 mashariki kote mwa nchi kunaoneshwa na wachambuzi wa kimataifa kama kilele cha mzozo wa miongo kadhaa katika eneo la Kivu, ambao pia uligombea udhibiti wa rasilimali kubwa ya madini. Katika hali hiyo, Uganda imetangaza kuwa imepeleka jeshi lake mjini Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri, kupambana na wanamgambo wa M23 wanaoendesha harakati zao katika mji huu wa eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Licha ya operesheni hii ya kijeshi ya kuunga mkono rasmi serikali ya Kinshasa, Uganda imekuwa ikilaumiwa na wengi kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, hivyo kupata udhibiti wa baadhi ya maeneo ya kimkakati ya uchimbaji madini.
Dharura ya kibinadamu
Wakati aina yoyote ya mazungumzo kwa sasa yamesimama kutokana na Rais Felix Tshisekedi kukataa kwa uthabiti kukabiliana na waasi, hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi analaani kuwa “ Katika siku za hivi karibuni, kati ya watu 10,000 na 15,000 wamewasili Burundi wakikimbia ghasia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Wengi wanatoka eneo la Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini, ambako hali inaendelea kuwa mbaya. Wakimbizi hao wengi wao ni Wakongo, lakini pia kuna raia wa Burundi wanaorejea nchini mwao baada ya kukimbia mapigano.”
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema, Watu, hufika zaidi kwenye kivuko cha mpaka cha Gatumba, karibu na mji mkuu Bujumbura, wakiwa wamechoka na wameumia, wengi wametenganishwa na familia zao na wakiwa na taarifa kidogo kuhusu hatima yao. Pia kuna taarifa za maelfu ya watu wanaoingia Burundi kupitia vivuko visivyo rasmi vya mpakani kando ya Mto Rusizi, karibu na Rugombo, huku kukiwa na taarifa kadhaa za kufa maji. Mbali na Burundi, idadi ya watu wanaokimbia DRC kuvuka mipaka mingine imesalia kuwa ndogo, UNHCR inaripoti. Hata hivyo, nchi jirani zinajiandaa kutoa usaidizi ukihitajika.