Ukraine.Miaka Mitatu ya Vita:Ulaya kama Muigizaji wa Amani
Massimiliano Menichetti
Miaka mitatu iliyopita mnamo tarehe 24 Februari 2022, Urusi ilivamia Ukraine na vita vilirejea katika moyo wa Ulaya. Hii imekuwa miaka mitatu migumu sana ambapo vifo, hofu na mateso vimeweka alama kwenye mioyo ya mamilioni ya watu. Hakuna idadi rasmi za majeruhi wa kijeshi na raia. Magazeti ulimwenguni kote yanaripoti kuhama kwa karibu watu milioni saba, kulingana na data kutoka katika mashirika ya Umoja wa Mataifa, ambao walilazimika kuacha kila kitu nyuma na kukimbilia nchi jirani ambazo zilitoa ukarimu au njia ya kupita hadi maeneo mengine salama. Ndani ya nchi, iliyokandamizwa katika miezi hii na baridi kali ambayo inafikia hata digrii ishirini chini ya sifuri, kuna karibu watu milioni nne waliokimbia makazi yao wanaotafuta hifadhi kutokana na ghasia. Wanaume, wanawake, watoto, wazee ambao mara nyingi, katika maeneo ya mpakani yanayoshambuliwa, wanaishi kwenye anadaki za kujikinga na mabomu au mashambulizi ya ndege zisizo na rubani. Miji mingi kwa sasa imeharibiwa na wingi wa vifusi, mara nyingi unakosekana umeme, kama ilivyo ukosefu wa uwezekano wa kupata joto, wa chakula na hata kutibiwa.
Papa, katika ujumbe huo uliotolewa jana ((23 Februari 2025) kwa ajili ya sala ya Malaika wa Bwana, alifafanua maadhimisho haya kuwa ya "uchungu na aibu kwa wanadamu wote" na katika kila hali anaendelea kurudia kwa nguvu kwamba "vita daima ni kushindwa", bila kuchoka kuomba "amani ya haki na ya kudumu" na haja ya mazungumzo. Msisitizo upo kabisa katika kivumishi hiki, kwa sababu amani ya haki inategemea kanuni ya usawa, kuheshimiana na uendelevu kwa muda. Wakati huo huo, njia ya mazungumzo lazima iwe ahadi kwa kila mtu. Kwa hiyo si suala la kusimamisha mabomu na vifaru tu, bali ni kutambua makosa yaliyofanywa, kuwa na ujasiri wa kupiga hatua nyuma, kuona sura ya mwingine, kujenga na kuunga mkono mfumo unaodhamini haki, usalama na ustawi wa pande zote. Inamaanisha, hata hivyo ni vigumu, kuanza upya pamoja.
Hadi sasa, njia iliyochukuliwa imekuwa na sifa ya silaha, matangazo na hata dhana ya matukio ya nyuklia ya mwisho wa ulimwengu wote. Maombi na majaribio ya kumaliza mzozo hayajafanikiwa, lakini matumaini hayajapotea, sawa na mshikamano wa mashirika mengi, taasisi na watu wenye mapenzi mema. Kuna shuhuda nyingi ambazo tumekusanya na kuenea katika miaka hii ya giza: hoistoria za kujitoa sadaka, mshikamano, upendo na shauku kwa ardhi ya yao, kwa ubinadamu hata katika uso wa mateso, majeraha au mapenzi yaliyovunjika, ambayo yanaonesha nia ya kuweka mioyo mbali na chuki licha ya uchokozi uliotesa na ulinzi uliofuata, licha ya wengi kushabikia kwa usahihi juu ya Warusi na uadui.
Ni suala la haraka kunyamazisha ghasia zote, kujenga upya uaminifu, kuzindua upya "Mkutano wa Kimataifa", kama ilivyodhaniwa miezi michache iliyopita na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, ambapo kile kilichofafanuliwa kama "roho ya Helsinki" kinaanza tena. Kwa sababu mnamo 1975 ilikuwa nia hasa ya kuketi pamoja kuzunguka meza ambayo iliruhusu ushirikiano kati ya mataifa ya Ulaya kukuzwa na mivutano kupunguzwa wakati wa Vita Baridi. Kwa hiyo wito pia ni kwa Ulaya ili kujitambua upya, kurudi kwenye mizizi ya baba waanzilishi: Robert Schuman, Konrad Adenauer, Alcide De Gasperi na kuwa na uwezo wa kuwa mdau mwenye nguvu na wa kuaminika kwa amani, wa kukaribisha na kuwa mfano wa udugu wa ulimwengu wote.