Burkina Faso, Mali na Niger Zimeathirika Sana na Vitendo Vya Kigaidi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vitendo vya kigaidi ni ukweli ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao; kiasi hata cha watu kukosa amani na utulivu wa ndani, kwa kuendea kuishi katika hofu na wasiwasi wa kushambuliwa. Vitendo hivi vimeharibu urithi mkubwa wa utamaduni, utambulisho wa watu pamoja na historia yao. Hadi sasa Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbalimbali za dunia. Vitendo vya kigaidi ni unyama dhidi ya: maisha, utu na heshima ya binadamu. Huu ni uhalifu dhidi ya binadamu na haki zake msingi. Vitendo vya kigaidi vinahatarisha usalama, maisha, mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu. Hivi ni vitendo vinavyokwenda kinyume na uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini sanjari na umuhimu wa kutunza dhamiri nyofu! Vitendo vya kigaidi vinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na viongozi wa kidini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa bila “kupepesa pepesa macho.”
Taarifa iliyotolewa na “Global Terrosrist Index 2025” inaonesha kwamba, nchi za Burkina Faso, Niger na Mali ambazo zote ziko katika Ukanda wa Sahel ni kati ya nchi ambazo zimeathirika sana kwa vitendo vya kigaidi. Taarifa hiyo inavitaja vikosi vya kigaidi vya Jamaat Nusrat Al-Islam wal Muslimeen, Jnim, kilichokita mizizi yake nchini Mali, kinahusika na nusu ya vifo vilivyotokea katika kipindi cha Mwaka 2024. Vikundi vingine ni Dola ya Kiislam, “Islamic State, IS”, Tehrik-e-Taliban Pakistan (Ttp) pamoja na Kikundi cha Al-Shabaab.
Hivi ni vikundi vinavyoendesha shughuli zao mintarafu masuala ya kisiasa, mazingira, kinzani za kisiasa na ukabila na kwamba, kwa hakika Burkina Faso ni kati ya nchi ambazo zimeathirika vibaya na vitendo vya kigaidi, ikifuatiwa kwa karibu zaidi na Mali pamoja na Niger, nchi zinazoongoza kwa kuwa na wahanga wengi wa vitendo vya kigaidi, kiasi cha asilimia 94% ya vitendo vyote vya kigaidi vilivyotokea kati ya Mwaka 2023. Nchi nyingine katika orodha hii ni Nigeria, Somalia na Cameroon. Nchi nyingine ni DRC, Kenya na Msumbiji. Taarifa inaonesha kwamba, Barani Afrika kuna matukio 190 ya kigaidi yaliyofanywa na kikundi cha Dola ya Kiislam, IS. Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kimeendelea kuwa ni tishio kwa Ukanda wa Sahel.