Tafuta

Siwaiti Tena Watumwa, Bali Rafiki: Jengeni Urafiki na Kristo Yesu

Mwanadamu tangu utoto wake, amejenga mang’amuzi ya urafiki, kiasi cha kushirikishana mambo nyeti; mafanikio katika maisha; wasiwasi na majonzi. Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Mithali linasema, “Marhamu na manukato huufurahisha moyo, kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.” Mit 27:9. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaalika waamini ili kutafakari kuhusu mahusiano na mafungamano ya urafiki, ili kuwashukuru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana. Yn 15: 12-17. Siwaiti tena watumwa bali marafiki, ni sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, sehemu ya tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa aliyoitoa Dominika tarehe 5 Mei 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Watumwa au watumishi wa Bwana kadiri ya Maandiko Matakatifu ni watu maalum waliopewa dhamana na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtumishi wake mwaminifu Musa katika Agano la Kale, Rej. Kut 14:31, Mfalme Daudi, Rej. 2Sam 7:8; Nabii Elia Rej. I Fal 18:36 hadi kwa Bikira Maria Rej. Lk 1:38. Mahusiano haya na mafungamano katika muktadha wa utumishi, kadiri ya Kristo Yesu hayatoshi. Kumbe, anakwenda mbele zaidi na kutaka mahusiano haya yasimikwe kwenye urafiki, changamoto na mwaliko kwa waamini kujenga urafiki na Kristo Yesu katika maisha na utume wao.

Siwaiti tena watumwa bali marafiki; jengeni urafiki na Kristo Yesu
Siwaiti tena watumwa bali marafiki; jengeni urafiki na Kristo Yesu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwanadamu tangu utoto wake, amejenga mang’amuzi na uzoefu wa urafiki, kiasi cha kushirikishana siri na mambo nyeti ya ndani, mafanikio katika maisha; wasiwasi na majonzi. Neno la Mungu katika Kitabu cha Mithali linasema, “Marhamu na manukato huufurahisha moyo, kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.” Mit 27:9. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutafakari kuhusu mahusiano na mafungamano ya urafiki, ili hatimaye, waweze kuwashukuru. Urafiki wa kweli ni uhusiano mzuri kati ya watu wawili au zaidi. Ni uamuzi wa mtu binafsi kuchagua uhusiano wa karibu na mtu mwingine kutokana na haja za moyo wake katika maisha kwa sababu katika maisha kuna kupenda na kupendwa; kutambulika, kujaaliwa, kuheshimiwa na kuthaminika: Urafiki ni msaada mkubwa katika kushirikiana na kusaidiana: kiroho na kimwili. Ni msaada mkubwa wa kujifahamu na kuwafahamu watu wengine; kujifunza na kujiendeleza kitabia, kiakili, kimaisha na kiroho. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, “Rafiki hupenda siku zote” Mit 17:17na wala si kama Yuda Iskarioti aliyemsaliti Kristo Yesu kwa busu. Rej. Mt 26:50.

Urafiki na Kristo Yesu usimikwe katika maisha na utume wao
Urafiki na Kristo Yesu usimikwe katika maisha na utume wao

Rafiki wa kweli ataandamana na kushikamana nawe hata pale unapoteleza na kuanguka; akakurekebisha, atakukemea na kukusamehe, lakini hawezi kukuacha. Kristo Yesu katika Injili anasema, wafuasi ni rafiki na watu anaowapenda, kiasi cha kuwakirimia upendo wake usiokuwa na mipaka, neema, Neno sanjari na kuwashirikisha kile ambacho amekisikia kutoka kwa Baba yake wa mbinguni, kiasi hata cha kutoa uhai wake kwa ajili yao, kwani anawapenda upeo, anawatakia mema yote ya mbinguni na anataka kuwashirikisha maisha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchunguza ndani mwao, ili kuangalia Kristo Yesu ana sura gani katika urafiki wao. Je, waamini wanajisikia kupendwa na Kristo Yesu, Je, ni sura ili ya Yesu wanayoitolea ushuhuda wa maisha. Je, wale wanaoteleza na kuanguka wanaweza kuonjeshwa huruma na msamaha? Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumkimbilia Bikira Maria, ili awasaidie kujenga urafiki na mahusiano na Kristo Yesu, Mwanaye mpendwa, ili hata wao waweze kuueneza na kuusambaza urafiki huu.

Urafiki
05 May 2024, 14:29

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >