Tanzania,Askofu Sangu kwa Sosthenes:Jibidishe kutenda kwa unyenyekevu,utii&upendo
Patrick P. Tibanga- Radio Mbiu Kagera.
Mnamo tarehe 20 Julai 2023, Mhashamu Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania alitoa homilia yake, kwa waamini wakati wa Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ya utoaji Daraja Takatifu ya Upadre kwa aliyekuwa Shemasi Sosthenes Ntemi Charles, wa Parokia ya Mtakatifu Luka, Bariadi, jimboni humo. Katika mahubiri hayo aliwahimiza na kutoa wito kwa Wakristo wote na wenye mapenzi mema kuomba Roho Mtakatifu ili awasaidia kutenda kati ya kuhubiri na kutangaza Injili ya Kristo.
Askofu Sangu katika mahubiri hayo alisema kuwa ukimpokea Roho Matakatifu utampeleka kwa watu wengine kwa upendo, huku upendo huo ukianzia kwa familia, Jumuiya na jamii inayokuzunguka. Vile vile aliwataka wakristo wanapompokea Roho Mtakatifu ili waishi na kumuonesha kwa vitendo kwa watu wanaowazunguka badala ya kuwa watu wa masengenyo na vitendo ambavyo havimpendezi Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo Askofu Sangu akimgeukia Padre mpya alimwomba afanye utume wake kwa upendo, huku akimhubiri Kristo, bila kuchoka na wala kukata tamaa, na akiongozwa na Roho Mtakatifu. Hakuishia hapo bali alimtaka Padre mpya Sosthenes Ntemi Charles, kujibidiisha katika kufanya kazi yake ya utume aliyoitiwa na Mungu kwa unyenyekevu, utii na upendo mkubwa huku akiongozwa na Mungu mwenyewe.
Askofu Sangu alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa utume wake ndani ya Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania kwa sababu tangu apewe majukumu rasimi ya kuwa askofu wa Jimbo hilo, amewapadrisha mapadre 33 na kwa idadi hiyo imepelekea kufikia mapdre kwa saa 78 ndani ya jimbo la Shinyanga.
Na hii ni kutaka kuonesha wazi kwamba Mungu anazidi kuita katika shamba lake kubwa kila wakati ambalo kama alivyowambia wanafunzi wake kuwa: “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. (Mt 9,37-39; ( Lk 10,2).
Njoo mnifuate, nitawafanya wavuvi wa watu. Bwana Yesu anasema. Aliyechagua Kristo hana haja ya kutazama nyuma bali ni kumkimbia na kuwaacha wafu wazikwe wafu wao.