Haiti:watawa sita waliotekwa nyara huko Port-au-Prince waachiliwa huru
Vatican News
Watawa sita wa Shirika la Mtakatifu Anna waliotekwa nyara mnamo tarehe 19 Januari 2024 huko Port-au-Prince, Haiti wameachiliwa huru. Watu wengine waliofuatana nao waliachiwa huru pia waliochukuliwa na watu wenye silaha mara baada ya kuzuia Bus walilokuwa wakisafiria. Uthibitisho wa kuachiliwa huru umevifikia vyombo vya habari vya Vatican kutoka kwa Askofu mkuu wa mji mkuu Max Leroys Mesidor wa Haiti, rais wa Baraza la Maaskofu wa eneo hilo, ambaye ameonesha furaha yake katika habari hii na kuwashukuru wale wote ambao walizingatia na kutoa msaada katika hali hii kwamba: “Tumshukuru Mungu! Ahsante kwa msaada wenu.”
Wito wa Papa wakati wa sala ya Malaika
Baada ya Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 21 Januari 2024 Baba Mtakatifu alizindua kwa moyo wote ombi akiwa katika dirisha la Jumba la kitume kwa ajili ya kuachiliwa watawa sita na kwa ajili ya majanga ambayo kisiwahicho kinapitia. Papa alisema kuwa: “Naomba kwa ajili ya maelewano ya kijamii katika nchi na ninawaalika watu wote kukomesha ghasia zinazosababisha mateso mengi kwa watu hao wapendwa.”
Maneno ya Askofu Dumas
Ombi la Papa la dhati lilifuatiwa na lile la Askofu Mkuu Pierre-André Dumas, wa Anse-à-Veau-Miragoâne na makamu Rais wa Baraza la Maaskofu, ambaye kwa njia ya vipaza sauti vya Radio Vatican, alikuwa amefahamisha kwamba anataka ajitoe kama mateka badala ya watawa hao. “Kuwateka nyara wanawake wanaojitolea maisha yao kuokoa maskini na vijana ni kitendo kitakachoona hukumu ya Mungu,” aliongeza kiongozi huyo, akinyanyapaa utekaji nyara ambao unaambatana na matukio mengi ya unyanyasaji ambayo yanaumiza uso wa nchi.
Kanisa la Haiti katika maombi
Hapo tarehe 24 Januari 2024, Kanisa Katoliki la Haiti liliandaa mkesha wa kuwaombea watawa na watu wote waliotekwa nyara. “Lazima waachiwe kukanyaga hadhi isiyoweza kuondolewa ya watoto wa Mungu!” aliandika Askofu Mkuu Mesidor na Padre Morachel Bonhomme, rais wa Baraza la Watawa wa Haiti, katika maelezo ya pamoja. Kwa hiyo waliwaalika waamini wote wa Haiti kuandaa mlolongo wa sala zisizokoma"kwa ajili ya kuachiliwa kwa watu nane na kutumia siku moja katika kutafakari na kuabudu Ekaristi. Kwa njia hiyo taarifa ya kuachiliwa huru ni habari njema ya ukombozi.