Askofu Jovitus Mwijage Askofu wa Jimbo la Bukoba,Tanzania,alitabaruku Kanisa la  KWAUSO na kuzika masalia ya Mwenyeheri Carlo Acutis (10.02.2024) Askofu Jovitus Mwijage Askofu wa Jimbo la Bukoba,Tanzania,alitabaruku Kanisa la KWAUSO na kuzika masalia ya Mwenyeheri Carlo Acutis (10.02.2024) 

Tanzania,Ask.Mwijage:Tulinde mahekalu na tusiyachafue kwa dhambi zetu

Tujitahidi sana kulinda mahekalu hayo na tusiyachafue kwa kutenda dhambi au kufanya chochote ambacho hakiendani na ukristo wetu,tujikinge na kuacha dhambi.Ni mahubiri ya Askofu Mwijage wakati wa kutabaruku Kanisa na Altare na kuzika masalia ya Mwenyeheri Carlo Acutis katika Kanisa la KWAUSO,Jimboni Bukoba Tanzania.

Patrick P. Tibanga, - Bukoba na Angella Rwezaula – Vatican.

Waamini Wakristu wa Mungu waliombwa kuishi maisha ya Utakatifu na kufuata mfano wa watakatifu akiwemo Mwenyeheri Carlo Acutis na daima kuzishika amri za Mungu katika maisha yao kila siku. Wito huo ulitolewa na Mhashamu Jovitus Mwijage, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania wakati homilia yake mnamo tarehe 10 Februari 2024, katika maadhimisho ya Misa Takatifu ya kutabaruku Kanisa na altare na kuzika sehemu ya masalia ya mwenyeheri Carlo Acutis katika Shule ya Sekondari ya KWAUSO yaani  ‘Kwaheshima ya Uso Mtakatifu’, Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania. Katika Misa hiyo iliyohudhuriwa na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga, Mapadre na Watawa wa mashirika mbali mbali  wakiwemo  waamini wa jimbo na wageni waalikwa, Askofu Mwijage alisema kuwa: “baada ya kupakwa Mafuta matakatifu katika ubatizo, mwanadamu anafanywa kuwa hekalu la Roho Mtakatifu,” na kumsihi kila mmoja kuiheshimu na kuitunza miili waliyopatiwa na Mungu ikiwa ni hekalu la Mungu. Na zaidi baada ya kutabaruku, Kanisa na altare vilivyotabarukiwa haviwezi kufanyiwa mabadiriko au kuamishwa bila kibali cha Askofu.”

Askofu Mwijage akipaka Mafuta Altare
Askofu Mwijage akipaka Mafuta Altare

Kwa kufanya hivyo: “tujitahidi sana kulinda mahekalu hayo na tusiyachafue kwa kutenda dhambi au kufanya chochote ambacho hakiendani na ukristo wetu, tujikinge na kuacha dhambi na kamwe tusivunje amri za Mungu na tunatakiwa kuishi maagano ya Ubatizo na kumpokea Bwana Yesu Kristu tukiwa na mioyo iliyotakata na kuishi maisha ya Utakatifu.”Alisema. Askofu Mwijage aidha akiendelea alisema kuwa Kanisa ni sehemu takatifu iliyotengwa kwaajili ya sala na sio kitu kingine ikiwemo kufanya mambo ambayo hayastahili na sio sehemu ya mazungumzo kwa kupiga soga au kufanya mambo ambayo hayaendani ni dhumuni la Kanisa. “Kanisa ni sehemu ya kuheshimu na sala yakiwemo masifu, Ibada kwa watakatifu mbali mbali na kumuomba Mungu kwa hiyo kama ulikuwa umezoea kucheza na kufanya maongezi ambayo hayafai hapa siyo mahali pake, nenda nje kafanye vitu hivyo ni kwaajili ya kutolea sadaka takatifu ya Misa na sio kitu kingine.”Alisisitiza Askofu Mwijage

Askofu Mwijage akipeleka Ubani kufikizia Altare
Askofu Mwijage akipeleka Ubani kufikizia Altare

Akigeukia Mwenyeheri Carlo Acutis ambaye sehemu ya masalia yake yalizikwa katika altare ya Kikanisa hicho, Askofu Mwijage alisema kuwa kijana Carlo alifariki akiwa na umri miaka 15 kwa ugonjwa wa wa Saratani huko Monza, Milano nchini Italia. Na  alipokuwa anakaribia mwisho wa maisha yake alisema kuwa: “Anamshukuru Mungu kwa kila dakika ya maisha yake kwa maana aliitumia muda vizuri kumtukuza Mungu, hivyo nanyi vijana tumieni muda wenu vizuri ikiwemo kusoma na kufanya mambo yanayompendeza Mungu, ndio maana Padre Stanslaus amechagua kijana huyo awe muombezi wetu kila siku hasa nyie wanafunzi wa hapa.” Alisisitiza Askofu Mwijage.

Wakati wa kufukizia Altare
Wakati wa kufukizia Altare

Askofu Mwijage akiendelea na mahubiri hayo alisema, “Sasa hivi mnakimbizana na simu, yeye alitumia mawasiliano kuwafundisha wenzake, ndio maana Kanisa limemuweka awe mlinzi wa Internet, na hivyo  huyu awasaide vijana kutazama mambo yatakayo wanufaisha katika maisha ya sasa na baadaye na sio kupoteza muda  na Wale ambao wanakua na vishawishi kutazama mambo yasiyofaa mumuombe huyu mwenyeheri Carlo Acutis awaombee.”Alielezea Askofu Mwijage. Katika mahubiri hayo vile vile alitoa  ombi kwa Padre Stansalaus Mutajwaha kuwa na sala  maalum ya kusali kila wakati katika misa Takatifu ili kumuomba Mweheri Carlo Acutis awasaidie wanafunzi na wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya manufaa ya kuutafuta Ufalme wa Mungu.

Kanisa la KWAUSO, -Kwa heshima ya Uso Mtakatifu
Kanisa la KWAUSO, -Kwa heshima ya Uso Mtakatifu

Katika misa hiyo kulikuwa na waamini wa ndani na nje  ya majimbo ambao walifika kushuhudia tukio muhimukatika Kikanisa cha Shule ya KWAUSO, ambapo, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican imemfika mmojawapo  kuelezea hisia yake ya siku hiyo. Bi Sylvia Matovu kutoka Jimbo Kuu Katoliki  la Dar Es Salaam Tanzania, alielezea kwamba: “Binafsi niliguswa na namna Padre  Mutajwaha, ambaye amejitoa kwa uaminifu mpaka kusimamia ujenzi wa lile Kanisa,na ambalo limekuwa ni Kanisa lililojengwa kwa muda mfupi, na la kisasa kabisa, lakini jambo lililogusa zaidi ni kuona namna shangazi yake Mwenyeheri Carlo Acutis alivyojitoa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa hilo na bado akahusika katika kusaidia kupata sehemu ya masalia ya wa mpwa wake ili kutakatifuza altare ya Bwana. Bi Matovu aidha alisema kwamba: “ huo ni ushuhuda pia uliotolewa na Padre Stanslaus Mutajwaha alivyo tamka wazi wazi wakati wa sherehe za mchana kwamba "ni muujiza wa Mungu na hata akitazama Kanisa analiogopa kwa sababu ya ukuu wa Mungu" anaouona ndani yake, na kumbe kwetu sisi inabaki kuwa tafakari na funzo la kujitoa pasipo kujibakiza kwa ajili ya Mungu.”

Askofu Almachius wa Kayanga alikuwapo katika kutabaruku Kanisa la KWAUSO
Askofu Almachius wa Kayanga alikuwapo katika kutabaruku Kanisa la KWAUSO

Kuhusu Kanisa hilo limejegwa kwa mjengo wa ghorofa na linaweza kukaliwa na watu zaidi ya elfu moja, lakini kuna sehemu kubwa huko juu ambako waamini wanaweza kuketi na kuona vizuri altare ya Bwana. Ndani ya Kanisa hilo upande wa kushoto wa Altare pembeni kuna Picha kubwa ya SANDA YA TORINO. Upande wa nyuma juu kabisa ndani ya Kanisa kuna picha ya Uso wa Yesu, wakati  pembeni juu ukutani upande wa kulia mwa Altare kuna picha ya rangi ya Mwenye Heri Acutis. Sehemu ya masalia ya Mwenye Heri Carlo Acutis yalikuja na barua inayothibitisha ukweli wa  masalia halisi ya Carlo Acuti. Barua hiyo ilitafsiriwa kutoka Kilatini kwa waamini walioshiriki misa hiyo.


Kuhusiana na  Nakala ya Sanda ya Torino  Padre Mutajwa alifafanua akizungumza na Vatican News kuwa: “Mimi nilifikiwa na wazo la Sanda kwa mara ya kwanza bila kutegemea mwezi Aprili mwaka 1985, ikiwa ni mwaka wangu wa 8 wa upadre, nilipokutana na taarifa juu yake katika gazeti moja linaloitwa National Geographic Magazine,Toleo la Juni mwaka 1980.Hisia zangu za kwanza baada kuisoma makala hii zilikuwa hasi na chanya kwa wakati mmoja.”

15 February 2024, 17:05