Tafuta

Kila taasisi ya kidini inapaswa kujitolea kulinda watoto na watu walio katika mazingira magumu. Kila taasisi ya kidini inapaswa kujitolea kulinda watoto na watu walio katika mazingira magumu. 

Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika ulimwengu wetu wa leo!

“Kanisa linaweka wakfu huduma ya uangalifu kwa ulinzi wa watoto na watu wazima walio katika mazingira magumu.Kazi hii ya ulinzi na matunzo inaangukia Kanisa kwa ujumla wake,lakini hasa kwa Wachungaji wake ndiyo inabidi itekelezwe.”(As loving Mother).Katika hilo Padre Mkude anauliza:Je,mazingira yetu:makanisa,jumuiyani,nyumba,mikusanyiko ya kidini na kijamii,mashuleni na mitaani yapo salama kwa mtoto?

Padre Gaston Mkude na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika barua binafsi ya Papa Francisko ya Motu proprio Come una madre amorevole, yaani kama mama mwenye upendo, iliyochapishwa tarehe 4 Juni 2016 inaanza kifungu cha kwanza kueleza kwamba: “Kama mama mwenye upendo, Kanisa linawapenda watoto wake wote, lakini linawajali na kuwalinda wale walio wadogo na wasio na ulinzi kwa upendo wa pekee sana: hii ni kazi ambayo Kristo mwenyewe anaikabidhi kwa jumuiya nzima ya Kikristo kwa ujumla. Kwa kufahamu hili, Kanisa linaweka wakfu huduma ya uangalifu kwa Ulinzi wa Watoto na Watu wazima walio katika mazingira magumu. Kazi hii ya ulinzi na matunzo inaangukia Kanisa kwa ujumla wake, lakini hasa kwa Wachungaji wake ndiyo inabidi itekelezwe. Kwa hiyo Maaskofu wa Majimbo, Mapatriaki na wale wanaowajibika kwa ajili ya Kanisa mahalia wanapaswa kutumia bidii ya pekee katika kuwalinda wale ambao ni wanyonge kati ya watu waliokabidhiwa"(Rej.Kifungu 1).

Tunahitaji kuwasindikiza watoto
Tunahitaji kuwasindikiza watoto

Ndugu msomaji wa makala hii ni katika muktadha huo, ambapo wachungaji/wote, kila mahali walipo na taasisi mbali mbali za kitawa wanao wajibu wa kufundisha na kueleza ukweli wa maisha hasa katika ulinzi na utetezi wa watoto na watu walio katika mazungira magumu. Kwa misingi hiyo, Padre Gaston Mkude anatoa tafakari pana juu ya ulinzi huo muhimu ili kumwepusha mwathirika wa leo hii katika madhara mengi ya kimwili na kiroho lakini pia hakosi kuuliza maswali ya kutafakari kwa kina kuhusiana na suala hili zima ambalo linanyanyasa watoto duniani leo hii.

Nawiwa kwanza kama mwanadamu, lakini zaidi kama mwenye jukumu mbele ya Mungu la kuwalinda na kuwasindikiza watoto wadogo kwenye utakatifu kama Mkristo na zaidi sana kama kuhani wa Bwana katika Kanisa lake. Mtoto anapaswa kulindwa kwa malezi mema na pia dhidi ya yale yote yenye kumletea madhara iwe kiroho, kimwili au kiakili na kisaikolojia. Je, natambua wajibu wangu wa pekee katika hilo kama kuhani, mzazi, mlezi, ndugu, jirani, mwalimu, mchungaji, katekista, sheikh, imamu, ustadhi, na mengine? Huu ni wajibu sio utokanao na wadhifa wangu au wako, bali kwanza ni wa kila mwanadamu mwenye kutambua umuhimu wenye ulazima katika kumlinda mtoto!

Watoto wengi wananyanyaswa, usalama wao hatasehemu ambazo huwezi tegemea
Watoto wengi wananyanyaswa, usalama wao hatasehemu ambazo huwezi tegemea

Je, mazingira yetu iwe katika maeneo ya makanisa yetu, jumuiyani, nyumba na katika mikusanyiko ya kidini na kijamii, majumbani, mashuleni, mitaani na kadhalika yapo salama kwa mtoto? Je, tumeweka mikakati gani ya kuhakikisha watoto wanapokuwa katika mazingira ya kanisani, majumbani, mashuleni, mitaani, michezoni, na kadhalika wanakuwa salama? Tufanye nini kuwalinda na kuhakikisha usalama wa watoto iwe majumbani, mashuleni, michezoni, mitaani na makanisani na kwingineko? Ni swali la kujiuliza. Tumeshaweka mikakati au mazingira ya kuhakikisha usalama wa watoto? Ninaguswa kweli na kuwiwa na usalama wao? Ninatambua kweli wajibu wangu wa kuifahamisha jamii ya Mungu umuhimu wenye ulazima katika kumlinda mtoto ili abaki salama?

Leo tukiri kuwa mtoto hayupo salama iwe majumbani baina ya wanafamilia na ndugu au majirani, mitaani, michezoni, mashuleni, makanisani na kwingineko anapokuwa mtoto! Mtoto hayupo salama majumbani na wazazi, ndugu, jamaa, waangalizi na walezi, walimu, wakufunzi mbali mbali, makatekista, watawa, mapadre, maaskofu, masheikh, maustadhi na maimamu, wachungaji, manabii, mitume, mashemasi na kadhalika na kadhalika. Ni hali inayosikitisha na kuhuzunisha sana! Ni hali hatarishi sana! Inatisha kwani hata wale wanaotegemewa kuwa walezi wa watoto tumegeuka na kuwa hatarishi kwa watoto! Sio jambo jema hata kidogo, sio dalili njema yenye afya sio tu kiimani bali hata katika ubinadamu wetu!

Ulinzi wa watoto wadogo kila kona lazima uwekwe kipaumbele
Ulinzi wa watoto wadogo kila kona lazima uwekwe kipaumbele

Mtoto hayupo salama na njia za kisasa za mawasiliano, iwe ni simu za mikononi au mezani, maudhui ya runinga, maudhui ya redio zetu, maudhui ya (gadgets) mbali mbali za kidigitali na majukwaa mbali mbali ya mitandaoni na kadhalika na kadhalika. Hujasikia (cyber bullying), hujasikia maudhui ya ngono za watoto na wakubwa wakioneshwa na hata kuwashirikisha watoto wadogo na kusambazwa? Hujasikia ukatili wa watoto? Kuna mengi ya kutisha na kusikitisha itoshe tu kufungua macho na kuyaona yanayojiri leo. Watoto hawapo salama hata mashuleni wanaposoma. Watoto hawapo salama hata kati yao. Hawapo salama hata na baadhi ya maudhui wanayosoma mashuleni na kwenye vitabu vyao. Mtoto anakuwa kile anacholishwa! Watoto hawapo salama hata michezoni iwe baina yao na hata watu wanaowazunguka. Hawapo salama na hata aina ya michezo wanayoshiriki wakati mwingine!

Mtoto hayupo salama hata na baadhi ya mila na tamaduni zetu! Bahati mbaya sana tena sana mtoto hayupo salama hata katika maeneo ya nyumba za ibada iwe makanisani au misikitini au kwenye masinagogi na mikusanyiko mingine ya kidini. Tunafanya nini? Labda nisisambae sana katika hili, ila itoshe tujiulize tumefanya au tunafanya nini katika kuwalinda watoto wadogo? Je, kama Kanisa katika majimbo yetu kuna kamati na mikakati gani ya kuhakikisha tunamlinda na kumsindikiza mtoto? Je, katika parokia zetu tuna mikakati gani ya kumlinda mtoto? Je, katika jumuiya zetu ndogo ndogo za Kikristo au kwenye familia na mitaa yetu tuna mikakati gani ya kuhakikisha usalama wa mtoto?

Ulinzi wa Watoto wadogo ni muhimu
Ulinzi wa Watoto wadogo ni muhimu

Je, malezi anayopata mtoto leo iwe kutoka kwa wazazi, walimu, watumishi wa dini na kadhalika ni salama na yenye afya kwa mtoto? Labda mtaniuliza namaanisha nini kwa malezi salama! Mtoto anaweza kuathirika hata na namna zetu za maisha kwani matendo yanahubiri kwa sauti kubwa zaidi kuliko maneno. Mtoto anajifunza kirahisi na wepesi kile anachoona na kusikia katika mazingira yanayomzunguka. Je, namna zetu ni salama kwa mtoto? Nani anamlea mtoto leo? Je, tumemwachia nani au nini jukumu la kumlea mtoto leo mintarafu ulinzi na usalama wake? Au ndio wanalelewa na teknolojia ya kileo? Wanalelewa na runinga na (screens za computers) na (electronic gadgets) vifaa vya kieletroniki? Ni watoto wanaolelewa na (robbots AI? (yaani Roboti za Akili Mnemba) Je, tuna uhakika na usalama na ulinzi wao?

Mwanafalsafa CS Lewis (Belfast-Ireland 1898),katikakitabu chake cha “The Abolition of Man” yaani “Kukomeshwa kwa Mwanadamu" anatuonya na kututahadharisha kwani tunaweza kudhani malezi sahihi ni yale ya akili kichwani na darasani kwa kuwa tunahakikisha wanasoma shule nzuri na huku wakikosa kuwa wanadamu wenye kifua(Men without chest)! Ni hatari kwa ulinzi na usalama wa mtoto! Tunaishi nyakati za udikteta wa kimaadili na (Beh culture)! Ndio nyakati hizi za (gender ideology,) yaani itikadi za kijinsia, ndio nyakati za (Technocracy) za teknolojia. Hakuna Mungu wala kuogopwa wala kuhofiwa kwani mwanadamu anajiumba vile anavyotaka awe! Kila mmoja ni sahihi kwa kile anachoona kinafaa mbele yake! Hakuna wa kumshangaa mwingine kwani hakuna kipimo cha wote! Kila mmoja ni mungu kwa nafsi yake. Je, kuna usalama na ulinzi wa mtoto? Ni maswali ya kujiuliza na tutafakari kwa pamoja!

Tangu kutungwa kwa mimba hadi mwisho wa maisha lazima kulinda mtoto
Tangu kutungwa kwa mimba hadi mwisho wa maisha lazima kulinda mtoto

Malezi yenye usalama na ulinzi wa mtoto ni suala mtambuko! Ni suala lenye kugusa malezi yote kwa mapana yake! Tumejipangaje? Tunalionja hilo kama Kanisa na jamii kiujumla? Malezi ya ulinzi na usalama wa mtoto hayana budi kuanza tangu sekunde na dakika ile ya utungwaji wa mimba. Mtoto hana budi kulindwa hata kabla ya kuzaliwa, akiwa tumboni mwa mama na hata baada ya kuzaliwa. Ni wajibu wetu kuwalinda watoto tangu saa ile ya sekunde ya kwanza ya maisha yao. Ni wakati umefika sasa usalama wa mtoto iwe ni agenda yetu kubwa ya kila siku, kama vile tunavyokumbushana umuhimu na ulazima wa michango mbali mbali iwe majimboni, maparokiani au jumuiyani basi iwe pia agenda kuu katika majimbo yetu, maparokia yetu, vigango vyetu, jumuiya zetu na kadhalika na kadhalika. Ni mimi na wewe lazima tuone umuhimu wa kulisemea lakini zaidi sana kuona tunawiwa na ni wajibu wetu wa kuwalinda watoto. Tunafanya au tumefanya nini mpaka sasa? Uwekezaji mkubwa wa taifa lolote lile duniani ni katika kizazi cha watoto, haribu watoto umeharibu taifa, kwani umeharibu familia, Kanisa, Jumuiya, na kadhalika unayoweza kuyaorodhesha hapa. Haribu mtoto umeharibu ubinadamu wote!

Jamii lazima ihakikishe ulinzi wa watoto
Jamii lazima ihakikishe ulinzi wa watoto

Kuhusu Ulinzi wa Watoto na hati za kipapa

Mengi kuhusu ulinzi wa Watoto na hata kuanzishwa kwa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto  unaweza kuyapata kwenye Hati za kipapa, kuanzia na Barua ya Mkono wake. Baba Mtakatifu aliandika Chirography yaani maandiko ya mkono wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuanzishwa kwa Tume ya Kipapapa ya Ulinzi wa Watoto. Katika maandishi hayo mwanzoni Baba Mtakatifu anaeleza kuwa “Ulinzi madhubuti wa watoto wadogo (Minorum tutela actuosa) na kujitolea kuwahakikishia maendeleo yao ya kibinadamu na kiroho kwa kuzingatia utu wa binadamu ni sehemu muhimu ya ujumbe wa Kiinjili ambao Kanisa na washiriki wake wote wanaitwa kueneza  ulimwenguni kote. Matukio ya kuumiza yamelazimisha uchunguzi wa kina wa dhamiri kwa upande wa Kanisa na, pamoja na ombi la msamaha kutoka kwa wahanga na jamii kwa madhara yaliyosababishwa, yamesababisha kuanzishwa kwa mipango ya aina mbalimbali kwa lengo la kurekebisha, uharibifu, kufanya haki na kuzuia, kwa njia zote iwezekanavyo, kurudia kwa matukio sawa katika siku zijazo”….(Rej:Chirografo del Santo Padre Francesco per l’istituzione della Pontificia Commissione per la Tutela dei Minori (22 marzo 2014) Inglese.

Vile vile ilifuatia hata  vifungu vya  Sheria na asili na uwezo  ambapo ilichapishwa mnamo tarehe 21 Machi 2015.  Kwa kuanza na kifungu cha kwanza kinaelezea kuwa“Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto ni taasisi inayojitegemea iliyounganishwa na Vatican, yenye hadhi ya kisheria ya umma (can. 116 CIC). Tume ina kazi ya mashauriano, katika huduma ya Baba Mtakatifu(Rejea:Statuto (21 aprile 2015).

Kanisa linaitwa kuwa  mahali pa huruma na upole

Katika hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto mnamo tarehe 21 Septemba 2017, Baba Mtakatifu alibainisha kuwa: “Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Tume imeendelea kuakisi kanuni muhimu zaidi zinazoongoza juhudi za Kanisa kulinda watoto wote na watu wazima walio katika mazingira magumu. Kwa njia hiyo ilitimiza utume niliokabidhi kwao wa “kazi ya mashauriano, katika huduma ya Baba Mtakatifu”, wakitoa uzoefu wake “ili kukuza uwajibikaji wa Makanisa mahalia katika ulinzi wa watoto wote wadogo na watu wazima walio katika mazingira magumu.” (Sheria, kifungu cha 1). Kadhalika Papa Francisko alisema kuwa:“Kanisa linaitwa kuwa mahali pa huruma na upole, hasa kwa wale ambao wameteseka. Kwa sisi sote, Kanisa Katoliki linaendelea kuwa hospitali ya kambi inayotusindikiza katika safari yetu ya kiroho. Ni mahali ambapo tunaweza kuketi pamoja na wengine, kuwasikiliza, na kushiriki nao mapambano yetu na imani yetu katika habari njema ya Yesu Kristo. Nina imani kabisa kwamba Tume itaendelea kuwa mahali ambapo sauti za wahanga na walionusurika zinaweza kusikilizwa kwa maslahi. Kwa sababu tuna mengi ya kujifunza kutoka kwao na historia zao za kibinafsi za ujasiri na uvumilivu….”(Rej.Discorso del Santo Padre Francesco ai Membri della Pontificia Commissione per la Tutela dei Minori (21 settembre 2017) Inglese].

Mkutano wa Maaskofu kutoka Ulimwenguni kuhusu Ulinzi wa Watoto katika Kanisa 

Katika kuhitimishwa kwa Mkutano wa Marais wa Mabaraza ya Maaskofu duniani kuhusu: “Ulinzi wa Watoto katika Kanisa” uliofanyika kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019, Papa Francisko alisema kuwa: “Ukweli wa kwanza unaojitokeza kutokana na data iliyopo ni kwamba wale wanaofanya unyanyasaji, yaani vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono au kihisia, kimsingi ni wazazi, jamaa, waume wa watoto walioolewa, makocha na walimu. Zaidi ya hayo, kulingana na yakwimu za UNICEF ya 2017 kuhusu nchi 28 duniani kote, wasichana 9 kati ya 10 ambao wamelazimishwa kufanya ngono wanafichua kwamba walikuwa waathiriwa wa mtu waliyemfahamu au ambaye alikuwa karibu na familia yao. Ukatili wa jambo hili la ulimwenguni pote unazidi kuwa mbaya zaidi na wa kashfa ndani ya Kanisa, kwa kuwa haupatani kabisa na mamlaka yake ya kimaadili na uaminifu wake wa kimaadili.Watu waliowekwa wakfu, waliochaguliwa na Mungu kuongoza roho kwenye wokovu, wanajiruhusu kutawaliwa na udhaifu au ugonjwa wao wa kibinadamu na hivyo kuwa zana za Shetani.” (Rej:https://www.vatican.va/content/francesco/en/speeches/2019/february/documents/papa-francesco_20190224_incontro-protezioneminori-chiusura.html

Baba Mtakatifu Francisko aidha alitoa hotuba yake fupi tarehe 22 Februari kwa washiriki wa mkutano kuhusu ulinzi wa watoto, akisisitiza kuwa: "Nikimsikiliza Dk. Gisoni, nilisikia Kanisa likizungumza kujihusu. Yaani sote tumezungumza kuhusu Kanisa. Katika ngazi zake zote..." (Rej:https://www.vatican.va/content/francesco/en/speeches/2019/february/documents/papa-francesco_20190222_incontro-protezioneminori.html.)Na katika ufunguzi wa Mkutano huo Papa  alisema: "Kwa hiyo tunaanza mchakato huu tukiwa na imani na roho kuu, ujasiri na uthabiti." (Rejhttps://www.vatican.va/content/francesco/en/speeches/2019/february/documents/papa-francesco_20190221_incontro-protezioneminori-apertura.html."

Umuhimu wa kulinda watoto
Umuhimu wa kulinda watoto

Hati zote hizo za Baba Mtakatifu Francisko unaweza  kujifunza mengi zaidi kuhusu jitihada za Papa katika utetezi wa ulinzi wa Watoto. Baba Mtakatifu ameendeleza kuonya na kuelezea umuhimu wa ulinzi wa watoto na watu walio katika mazingira hatarishi, katika hotuba yake kwa wajumbe hao hao wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto mnamo tarehe 29 Aprili 2022. Papa alisema: “Katika sehemu nyingi, mbegu muhimu zimepandwa kuhusiana na hilo, lakini bado kuna mengi ya kufanywa. Katiba ya Kitume inaashiria mwanzo mpya. Mbegu zilizopandwa zinaanza kuzaa matunda mazuri. Kesi za unyanyasaji wa watoto wadogo na washiriki wa Kanisa zimepungua kwa miaka kadhaa sasa katika sehemu hizo za ulimwengu ambapo data na rasilimali za kuaminika zinapatikana. Ningependa ninyi, kila mwaka, mniandalie ripoti juu ya mipango ya Kanisa kwa ajili ya ulinzi wa watoto na watu wazima walio katika mazingira magumu. Pia kuna mahitaji fulani ya haraka zaidi ambayo Tume inaweza kusaidia kukidhi, hasa kwa ajili ya ustawi na uchungaji wa watu ambao wamepitia dhuluma. Nimefuatilia kwa shauku njia ambazo Tume, tangu kuanzishwa kwake, imetoa fursa za kusikiliza na kukutana na waathirika na walionusurika.”….

(Rej.Discorso del Santo Padre Francesco ai membri della Pontificia Commissione per la Tutela dei Minori (29 aprile 2022) [Inglese.]

Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto
Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto

Suala la ulinzi wa Watoto limekuwa muhimu na kulihamaisha  ambapo Papa Francisko alikazia zaidi katika hotuba yake kwa Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto alipokutana nao natre 5 Mei 2023 na kutaja kanuni tatu za kuzingatia  kuwa: “Hakuna mtu leo hii anayeweza kudai kwa uaminifu kwamba hajaathiriwa na ukweli wa unyanyasaji wa kijinsia katika Kanisa. Katika kazi yenu ya kushughulikia suala hili lenye mambo mengi, ningekuomba mzingatie kanuni tatu zifuatazo na kuzizingatie kama sehemu ya hali ya kiroho ya fidia: Kwanza, ambapo madhara yalifanywa kwa maisha ya watu, tunaitwa kukumbuka uwezo wa Mungu wa kuumba ili kufanya tumaini litokee katika kukata tamaa na maisha kutoka kwa kifo…” “Pili, unyanyasaji wa kijinsia umefungua majeraha mengi katika ulimwengu wetu, sio tu katika Kanisa. Waathiriwa wengi wanaendelea kuteseka na athari za unyanyasaji ambao ulifanyika miaka iliyopita, bado unaendelea kuwa kikwazo na chanzo cha kuvunjika katika maisha yao.” “Tatu, ninawahimiza kusitawisha mtazamo unaoakisi heshima na fadhili za Mungu mwenyewe. Mshairi na mwanaharakati wa Marekani Maya Angelou aliwahi kuandika: “Nimejifunza kwamba watu watasahau ulichosema, watu watasahau ulichofanya, lakini watu hawatasahau kamwe jinsi ulivyowafanya wahisi…"

(Rej. Discorso del Santo Padre Francesco ai Membri della Pontificia Commissione per la Tutela dei Minori (5 maggio 2023)
Inglese].

Tuwalinde watoto dhidi ya makucha ya hatari katika maisha yao
09 March 2024, 12:10