Italia,Savignano(ACR):Likizo ya kiangazi kwa watoto:“Unalo Neno langu Yeremia”
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika ya Camping za kila mwaka zinazoandaliwa na Parokia ya Mtakatifu Lucia, huko Savignano Sul Rubicone, Jimbo Katoliki la Rimini nchini Italia, kuanzia watoto wa shule za msingi hadi Vyuo Vikuu ni mojawapo ya vipindi muhimu sana katika makuzi ya kiroho kwa vijana kila mwaka! Hata kwa mwaka 2024, Parokia hiyo imeendeleza Camping mbali mbali pia kwa Watoto wa shule ya Msingi katika Nyumba ya likizo za kiangazi katika Mkoa wa Toscana kwenye msitu uitwao Casentino kuanzia tarehe 28 Julai hadi 4 Agosti 2024. Watoto hao wa Chama cha Matendo ya vijana Katoliki, Savignano (ACR), walisindikizwa na wahuishaji wao wakiwa na Paroko wao wa Parokia, Padre Giorgio Farina. Kauli mbiu iliyoongoza likizo na mafunzo ya vijana 2024 ni :“Unalo Neno langu Yeremia” kwa njia hiyo, ni masomo kutoka kitabu cha Nabii Yeremia.
Katika siku hizo watoto kuanzia umri wa miaka 7 hadi 11 wamefanya uzoefu wa kuishi pamoja maisha ya kijumuiya. Siku ilikuwa ikianza mapema na mazoezi, kifungua kinywa na wakati wa tafakari fupi kupitia maigizo kwa kuoongozwa na kitabu cha Nabii Yeremiah. Ni somo gumu lakini kwa ubunifu wa viongozi wa watoto hao na usikivu, kila mwisho wa siku watoto walitoa muhtasari mzuri wa kushangaza kwa kile ambacho waliweza kukiishi kupitia somo hilo. Kwa njia hiyo mada ziligawanyika kwa siku kuanzia Dominika tarehe 28 Julai 2024 ambayo ilikuwa ni Kukaribisha na kusikiliza. Ili kufanya kazi kuwa rahisi, watoto waligawanywa katika makundi madogo yaliyopewa majina ya Agano jipya ili kubaki katika mantiki ya somo lilioongoza siku hizo. Kwa hiyo kulikuwa na kundi la Wababilonia, Wasiria, Wamisiri na Wamedia katika kuharakisha shughuli zao ndogo ndogo za michezo na mafunzo yak ila siku.
Jumatatu tarehe 29 Julai 2024 mada ilikuwa ni mshangao na kutafuta (kwa kuongozwa na Somo la Yeremia 7,1-15. Siku hiyo iliwafundisha watoto kuwa na mshangao kwa kila kitu na kutafuta kutazamana wao kwa wao na kupokeana jinsi walivyo na kumtafuta Bwana. Baada ya chai na maigizo ilikuwa ni safari ya mlimani, wakiwa wanatembea walizungumza kati yao, na walitakiwa baadaye watazame mandhari ya msitu uliojaa mimea na miti na uzuri wa kazi ya uumbaji. Baadaye ilikuwa ni kutazamana uso kwa uso ili kujuana vizuri, na kuulizana maswali.
Tarehe 30 Julai 2024 kwa kuongozwa na Somo la Yeremia 17, 5-10, watoto walifundishwa kuamini Mungu hata wakati hatujuhi yote yale yanatotusibu. Mungu anao mpango kwa kila mmoja wetu na tunaweza kuamini Yeye kwa sababu anatujua vizuri zaidi ya mwingine yeyote yule. Tunapaswa kubaki kwa hiyo waaminifu, karibu na Yeye na kufanya kile cha haki hata kama daima siyo jambo rahisi.
Tarehe 31 Julai 2024, mada ilikuwa ni kushuru Mungu kupitia Somo la Yeremia, 23,1-8. Siku hiyo watoto walijifunza namna ya kumshukuru Mungu. Kwa ishara ndogo ndogo wahuishaji kupitia maigizo walitafuta kuonesha jinsi neno llinaweza kufanya kuelewa umuhimu wa mchungaji yaani kiongozi wa maisha yetu. Katika hilo Nabii Yeremiah aliwaeleza viongozi wa watu wa Israeli kile ambacho Mungu alisema kwao kwa kuwa hawakufuata Neno la Mungu na hawakuweza kutunza muungano wa watu. Katika wakati wetu tunaweza kifikiria Mungu kama Mcungaji ambaye tunamwamini. Ni Yeye ambaye anatuelekeza njia. Anatufanya tuhisi tumelindwa na anatusaidia kujikamilisha. Mungu anakabidhi watu tulio nao karibu kazi ya kutunza, na anatutazama na upendo na kwa njia hiyo lazima tumshukuru.
Tarehe 1 Agosti 2024, mada ya siku ilikuwa ni uwajibakaji na kutunzana. Watoto kupitia somo la Nabii Yeremija 29, 1-14, kama ilivyokuwa kwa wahuishaji vijana kupitia maigizo, somo lilikuwa ni kuona Mungu anavyotangazia watu wa Israeli wanavyopaswa kubaki katika Nchi ya Babilonia kwa miaka 70. Na wakati huo huo, leo hii hata sisi tunapaswa kujifunza kuwa na zawadi ya subira na wakati wa kusubiri kusiwe wakati wa kupoteza muda, bali ni muda wa kuishi kikamlilifu na uwepo wa kujionesha bora kila sekunde. Mungu katika subira hiyo hatuachi kamwe, hata katika hatua mbaya sana, ya maisha yetu, badala yake anatutunza, sisi kwa kutualika kuwajibika kwa ajili ya wengine kwa kuwasindikiza katika safari ndefu ya maisha yao.
Tarehe 2 Agosti 2024 siku hiyo iliongozwa na mada ya kushirikisha na kuona kupitia somo la Nabii Yeremia 31, 1-14. Hawa ni watoto wadogo, lakini kupitia maigizo wanalielewa somo vizuri kwamba kupitia Nabii Yeremiah Mungu anawalekea watu uhamishoni huko Babilonia ambao kwa mara nyingine watajua huruma yake na upendo mkubwa. Kiukweli licha ya ukosefu wa imani ya watu wake, Mungu hawaachi bali anapyaisha ahadi yake, na kuahidi wokovu wa Israeli. Bwana anatangaza kuwa kurudi kwa Waisraeli kutoka huko Babilonia kutakuwa ni mwanzo wa watu wote, mwanzo mpya ambao utapelekea Ushirikishwaji wa furaha kwa watu wote. Kwa njia hiyo watu wote wataweza kuona wale wanaowazunguka ishara za upendo wa Mungu.
Tarehe 3 Agosti 2024 kama kawaida siku ilianza na mazoezi na pia somo ambalo liliongoza siku nzima katika mafunzo na michezo ya kupanda na kushuka katika mlima. Mada kuu iliyoongoza ni Uwezekano. Yeremia alitangaza namna mpya ya kuishi, kutoka maneno yaliyochongwa katika mwamba, sasa yanapitia kwenye hisia zetu ambazo Mungu anatufanya kuhisi moja kwa moja katika moyo. Namna hiyo mpya ya kuwasiliana, lazima ikutane na uwezekano wa kusikiliza na kuwa tayari katika moyo wetu kwa Yule aliyetuzawadia, yaani Mungu. Kwa njia hiyo kwenda, yaani kukubali kutumwa kwa sababu moyo uliojaa Roho Mtakatifu unasukuma kwenda kila mahali na kupeleka Habari Njema ya Agano jipya la Mungu. Hayo yalikuwa ni kupitia Somo la Nabii Yeremia 31,31-34 ambaye Bwana anathibitisha jinsi ambavyo “atasamehe dhambi zao za watu wake na hatakumbuka kamwe dhambi hizo.”
Katika siku hizo pia kulikuwa na matembezi ya kupanda na kushuka mlimani, ambapo watoto waliweza hata kufika mlima wa Falco wenye urefu wa mita(1658) na kuendelea hadi Mlima Falterona(1654),karibu na Falco ambao ni wa pili katika vilima vya mkoa wa Toscana na Emilia Romagna nchini Italia. Kupanda na kushuka milima kunawawezesha watoto kupumua hewa nzuri katika mazingira tofauti na waliyozoea. Lakini vile vile hapakosi kuanguka, kujikwaa nk. Na katika maisha mambo hayo hayawezi kukosekana kuanzia udogo hadi ukubwa.
Katika uzoefu huo wa kutembea katika misitu na kupanda milima vile vile watoto walipata fursa ya kutembelea Monasteri ya Kibenedikitini ya Watawa Wacalmadoli, baada ya kutembea Km 8 kutoka nyumba ya likizo. Hapo walikutana na Padre Alessandro Barban (O.S.Bcam) akiwa pamoja na Shemasi, DonBosco Mligo (O.S.BCam)kutoka Tanzania ambaye ni mmoja wa Jumuiya hiyo. Padre Alessandro Barban kwa ukarimu wake aliwaomba watoto licha ya kuchoka wampamtie dakika 20 tu za ukimya ili awaeleze historia kwa ufupi ya Monasteri hiyo. Padre alieleza juu ya Historia ya ishala zao na Kanisa la kwanza la Monasteri hiyo jinsi lilivyokuwa limejengwa kwa mbao tu na sasa limenakishiwa vizuri kwa namna mpya. Padre huyo, aidha alisimulia juu ya jengo la mwanzilishi wa Monasteri hiyo Mtakatifu Romwald na mahali alipokuwa akiishi. Watoto walifurahi sana lakini pia viongozi wao ambao walikuwa hawajapata fursa ya kuingia ndani ya Monasteri hiyo.
Dominika tarehe 4 Agosti 2024 ilikuwa ni siku ya kuagana, mara baada ya misa Takatifu wakiwa na wazazi wao waliokuja kuwapokea. Hapo ilikuwa ni kuongozwa na masomo ya siku ambapo Somo la kwanza kutoka katika (Kut 16,2-4.12-15), lilisimulia jinsi Mungu alivyowalisha Waisraeli jangwani kwa kuwa baada ya kukombolewa utumwani Misri, Waisraeli walisafiri safari ndefu ya kuchosha. Walipofika jangwani, walitindikiwa chakula na wakakosa maji. Hivyo wakamnung’unikia Musa na Haruni wakiwaambia; “Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula hata kushiba; kwani mmetutoa huko ili kutuua kwa njaa”. Mungu alisikia manung’uniko yao akamwambia Musa; “Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate na nyama kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku. Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
Katika Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yh 6:24-35) ilikuwa inaeleza mafundisho ya Yesu juu ya habari za chakula kiletacho uzima wa milele, yaani Ekaristi Takatifu. Katika kusimulia ilibanisha kwamba watu walimtafuta Yesu kwa shauku kubwa, na walimkuta ng’ambo ya bahari, na kumuuliza Rabi, umekuja lini hapa? Yesu akijua mawazo yao, aliwaambia ukweli kwamba “ni kwa sababu walikula mikate wakashiba, ndiyo maana walimtafuta. Kwa namna hiyo Yesu aliwaonya wasikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali kile chakula kinachowaletea uzima wa milele.” Watoto wakati wa misa na hasa katika wakati wa maombi walisoma maombi yao waliyoandika vizuri kabisa wakimshukuru Mungu kwa uzoevu mzuri walioushi kwa siku hiyo saba za kiroho. Na zaidi hawakuwasahau wahushaji wao Emanuel,Thomasi Davide, Sara, Giulia, Fiorella pia Padre Giorgio pamoja na wahudumu wote walioshiriki kuandaa kila siku chakula, chai na kila jambo kuwawezesha waishi vizuri kuanzia na Gabriele Vincenzi(Bebe) na wote.