2024.09.12Kongamano la V la  Ekaristi Takatifu  nchini Tanzania. 11-16 Septemba 2024. 2024.09.12Kongamano la V la Ekaristi Takatifu nchini Tanzania. 11-16 Septemba 2024. 

Kongamano la V la Ekaristi Takatifu,Tanzania:Tafuta kumjua Mungu kwanza!

Kuhani ni kiungo kati ya Mungu na watu na kazi yake kubwa kama kuhani ni kumtolea Mungu sadaka,kuunganisha na kupatanisha watu wa Mungu.”Hayo yalisemwa na Askofu Nzigilwa,wa Jimbo la Mpanda na Makamu Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC)karika Misa Takatifu siku ya Pili ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa,linaloendelea Msimbazi hadi Septemba 16.

Na Tekla Revocatus -Radio Maria na Angella Rwezaula – Vatican.

Askofu Nzigilwa amewataka waamini wanapotoa Sadaka na matolea yao, wahakikishe wanaunganisha sadaka na nafsi zao, ili zipokelewe na Mungu mwenyewe kupitia kuhani. Wito huo umetolewa tarehe 13 Septemba 2024 na Mhashamu Eusebius Alfredy Nzigilwa, Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda na Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) kwenye Adhimisho la Misa Takatifu siku ya Pili ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, linaloendelea Msimbazi Centre hadi tarehe 16 Septemba katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Askofu Nzigilwa alisema “kuhani ni kiungo kati ya Mungu na watu na kazi yake kubwa kama kuhani ni kumtolea Mungu sadaka, kuunganisha na kupatanisha watu wa Mungu sehemu ambayo pana upungufu fulani kati ya mtu na mtu au mtu na jamii yake anayoishi.” Aidha, aliwasisitizia Wakristo kuweka nia kila wanaposhiriki Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ili waunganishwe na Kristo mwenyewe na daima kuomba upatanisho wewe na Mungu.”

Kongamano 5 la ekaristi Takatifu kitaifa
Kongamano 5 la ekaristi Takatifu kitaifa

“Ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo umebadilisha kila kitu, hakuna tena familia ya Walawi wa Haruni, bali watu wote ni sawa kwa Kristo” alisema Askofu Nsigilwa. Katika adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu Askofu vile vile, alisema kuwa Mungu anapendezwa zaidi na sadaka ya nafsi kuliko sadaka ya vitu, hivyo ni lazima kumuomba Mungu kila mara wakati wa maandalizi ya kwenda kukutana na Yesu Kristo mwenyewe, na kwamba “hakuna zawadi kubwa ambayo Mungu amempatia mwanadamu zaidi ya zawadi ya kumtoa mwanaye wa pekee Ulimwenguni kwa ajili yako, hivyo kitu pakee ambacho unaweza kikifanya ukiwa hapa duniani ni kutafuta kumjua Mungu kwanza.

Kuabudu Ekaristi
Kuabudu Ekaristi

Askofu Nzigilwa, aliendalea kusema kuwa kwa Mkristo yoyote, kitu pakee ambacho ni cha kwanza kuomba ni ukombozi, ambao Mungu mwenyewe aliona ni jambo kubwa na la muhimu, hivyo hakikisha katika kuomba kwako unaomba Neema ya Ukombozi. “Ugua usiugue, oa au usiolewe lakini cha kupambania na cha kukitafuta ni ukombozi ambao Mungu amemtoa mwanaye kwa ajili yetu,”alisema Askofu Nzigilwa. Kwa kuhitimisha aliwasihi wakristo waliohudhuria na wanaofuatilia Kongamano hilo la Tano la Ekaristi kutumia nafasi hii ya kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kujipatanisha na Mungu na alisisistiza kwamba kwa  “kupokea kweli Yesu wa Ekaristi  lazima kuacha kuishi vinyongo vingongo.”

Mama Maria ni Mama wa Kanisa
Mama Maria ni Mama wa Kanisa

Kwa njia hiyo ni waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambao wamewahi kuandaa makongamano ya Ekaristi Takatifu, ngazi ya Jimbo mnamo mwaka 1998 na la kanda la Mashariki 2017, ambao wameandaa tena tukio hili la kitaifa. Katika hilo wameandaa wimbo na sala rasmi za Kongamano, na vile vile  kuna vitenge, fulana, vipeperushi na mabango yanayochochea ushiriki wa tukio hili. Kwa hakika Jimbo zima na waaamini wote, wanaendelea kuiishi Ekaristi Takatifu na hasa kutimiza mwaliko wa kauli yake isemayo: Udugu katika kuuponya ulimwengu: Ninyi nyote ni ndugu (Mt 23:8), iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuongoza Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Kimataifa, linaloendelea huko Quito nchini Ecuador hadi tarehe 15 Septemba 2024.

Mada zinazotolewa katika Kongamano 5 la Ekaristi kitaifa nchini Tanzania  ni: Ukuu wa Adhimisho la Misa, lililotolewa na Askofu Simon Masondole wa Jimbo la Bunda, Udugu wa Kikristo kama nyenzo muhimu ya kuutukuza utu wa mwanadamu, na Padre Joseph Mosha wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam; Ekaristi Takatifu na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo mada ilitolewa na Padre Benno Kikudo toka Baraza la Maaskofu Tanzania; Wakati Ekaristi Takatifu na Maadili, ilitolewa na Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo Katoliki la Kahama.  Ekaristi Takatifu na uponyaji katika familia, na Padre Rogasian Msafiri, wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,  Changamoto za Upetentekoste itatolewa na Padre Leonard Maliva wa Jimbo Katoliki la Iringa. Historia ya Uinjilishaji Kanda ya Mashariki, itatolewa na Askofu Msaidizi Mstaafu wa Jimbo la Bukoba Methodius Kilaini.  Mada hizi pia ndizo zinafafanuliwa kwa watoto wanaondelea katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

Ekaristi ni chakula cha Uzima
Ekaristi ni chakula cha Uzima

Siku ya Jumamosi tarehe 14 Septemba 2024, kutakuwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka viwanja vya Chuo Kikuu cha DUCE Chang'ombe mpaka viwanja vya Msimbazi Centre, yatakayopokelewa na Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora na ndiye atakayeadhimisha Misa ya siku hiyo.

Misa ya ufunguzi iliadhimishwa na Askofu mkuu Jude-Thadeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na wakati wa Misa ya kilele itaadhimishwa na Askofu Wolgang Pisa wa Jimbo la Lindi, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,(TEC.) Katika Misa hiyo ya kilele itashuhudia kufungwa kwa Mwaka wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka hamsini(50) ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo nchini Tanzania.

Tamko la Maaskofu wa Tanzania katika hitimisho la Kongamano la V la Ekaristi Septemba 15
13 September 2024, 14:21