Ujumbe wa Papa wa amani na mshikamano utakaa Papua New Guinea kwa miaka
Na Claudia Torres – Port Moresby, na Angella Rwezaula – Vatican.
Kufika kwa Papa, Papua New Guinea ni kitu cha kipekee, kitu ambacho hakiwezi kutokea mara kwa mara kwa sababu ya umbali na kwa sababu hii si moja ya nchi muhimu zaidi duniani Padre Giorgio Licini, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Papua New Guinea na Visiwa vya Solomon, alithibitisha hilo katika mahojiano na Vatican News, muda mfupi kabla ya kuanza kwa Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Sir John Guise, Port Moresby, Dominika tarehe 8 Septemba 2024.
Mmisionari wa PIME kutoka kaskazini mwa Italia, Padre Licini amekuwa katika nchi ya Pasifiki ya Kusini tangu 2003, na uzoefu wake umempa ufahamu wa kina wa vikwazo vya msingi ambavyo Kanisa Katoliki hukabiliana navyo huko. Alieleza kwamba “linapokuja suala la kushuhudia Kristo na Injili katika jamii,” masuala ya kijamii yanaleta changamoto kubwa zaidi. Umaskini, kutengwa, na ukweli kwamba watu wengi wanaishi katika vijiji vya mbali sana na ambako shule na vituo vya afya vinakosekana, ni baadhi ya masuala aliyotaja. Padre Licini pia alitaja pia jeuri na “machafuko, nyakati fulani kutokana na mapigano ya kikabila na masuala ya mila za mababu ambayo watu hao wanaendeleza."
Mwishowe, alisisitiza kwamba huku umaskini wa mijini ukiongezeka, vijana wengi hujikuta katika hali fulani: “Hawawezi kuona wakati ujao ulio wazi pamoja na ukosefu wa fursa na elimu duni.” Hata hivyo, Padre Licini anabaki na matumaini, akiwa na uhakika kwamba “ujumbe wa Papa Francisko wa amani, mshikamano, urafiki na upatanisho utaambatana na watu wa Papua New Guinea kwa miaka ijayo.