Tafuta

2022-05-31Mazishi ya Kardinali  Angelo Sodano. 2022-05-31Mazishi ya Kardinali Angelo Sodano. 

Kard.Re ameongoza misa ya mazishi ya Kard.Sodano

Dekano wa Baraza la Makardinali amefafanua juu ya kipindi kirefu cha huduma ya Sekretarieti Vatican ya Kardinali aliyefariki tarehe 27 Mei,wakati wa mahubiri yake kwenye Misa ya mazishi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.Mwishoni mwa maadhimisho hayo,Papa Francisko aliongoza Ibada ya hitimisho la Maziko kwa baraka.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, ameshiri Ibada ya mwisho ya kubariki Geneza la Kardinali Sodano katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, tarehe 31 Mei 2022, mara baada ya Misa iliyoongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa ajili ya mazishi ya Kardinali Angelo Sodano aliyefariki tarehe 27 Mei 2022 akiwa na umri wa miaka 94. Katika mahubiri yake ameanza na sentesi ya Yesu asemaye “Mimi ni ufufuo na uzima. Aniaminiye hata akifa ataishi milele (Yh 11,26). Maneno haya mawili yaliyotamkwa kwenye Injili iliyosomwa, yanaonesha wazo la kuelekea maisha ya milele ambayo Kristo kwa kifo na ufufuko wake alitupatia zawadi kwa wale ambao wanaamini na kumtumainia. Kifo kwa hakika kwa Mkristo si tu jambo la asili la kukubalika kwa hali halisi na hadhi. Kifo lakini kinapelekea kufungua njia ambayo inapelekea kukutana na aliye juu zaidi kwa  ule mkutano binafasi kwa Mungu. Sisi sote tuna hatima ya milele, amesisitiza Kardinali Re.

Watawa wakitoa heshima
Watawa wakitoa heshima

Kardinali Re amesema uhakika huo unahakisi maisha yake yote ya Kardinali, Angelo Sodano ambaye Bwana amemwita kwake kutoka katika kitanda cha Hosptali mahali alipokuwa amelazwa kwa wiki tatu. Miaka minne iliyopita akifikisha miaka 90 Kardinali Sodano aliandika Wosia wake wa kiroho kwamba “Ninasubiri sasa kwa utulivu ambapo Bana anakuja kuniita kwake, baada ya hitimisho la maisha yangu hapa duniani. Kwa mara nyingine tena ninapyaisha tendo langu la imani, la tumaini na upendo, kama nilivyojifunza nikiwa mtoto kwenye magoti ya mama yangu. Kwa mtazamo huo wa ndani ninatazama Bwana, nikitumaini kuwa siku moja atanipokea katika huruma kwenye mikono yake.  Kwa hisia hiso hizo, ninatazama Maria Mtakatifu, niliyomwomba tangu kijana kuwa ni “Mlango wa Mbingu”.

Mazishi ya Kardinali Sodano
Mazishi ya Kardinali Sodano

Kardinali Re, kwa kuongeza amesema, karibu mika 16 akiwa mhudumu wa Papa alijitahidi kwa umahiri wake na kujitoa kwa ajili ya amani. Hakukosa wakati kwa namna ya pekee jitihada ngumu katika hali halisi za kidiplomasia. Inatosha kufikiria mwisho wa vita baridi vya Ghuba, vita vya Iraq, migogoro ya Nchi za Mashariki mwa Ulaya, shambulio la kigaidi, mnamo tarehe 11 Septemba 2001 huko New York na kuzidi kuongezeka baadaye kwa ugaidi ulimwenguni. Kwa miaka mingi akiwa katika huduma ya Vatican, Kardinali Sodano aliamini kwa ufasaha Kristo na kufuata kwa uaminifu akimtumika kwa upendo na kujitoa kwa Kanisa na kwa Kharifa wa Mtume Petro. Mada ya upendo kwa Kanisa lilikuwa la kawaida kwake na mara nyingi katika mahubiri yake au katika hotuba zake zilizotajwa katika Kitabu cha Kardinali Ballestrero: “Kanisa hili ni la kupenda”, akisisitiza kuwa "haitoshi kuamini katika fumbo la Kanisa, lakini ni lazima kulipenda si kwa ujuu juu bali kwa kufanya kazi katika taasisi zake, kushirikiana matatizo ya kila siku katika Kanisa ambalo linafundisha, katika Kanisa ambalo linatakatifuza na katika Kanisa ambalo linaongoza kwenye upendo.

Mazishi ya Kardinali Sodano
Mazishi ya Kardinali Sodano

Alipohitimisha kazi yake kama Katibu wa Vatican, mnamo tarehe 15 Septemba 2006, Kardinali Angelo Sodado aliendelea hata hivyo kutoa huduma ya maana sana katika shughuli za Vatican, kama vile shughuli za Dekano wa Baraza la makardinali hadi  mwishoni mwa 2019, baada ya nguvu zake kupungua na kujikita daima katika sala ya kina. Sasa roho yake ipo katika mwanga wa Mungu. Somo la kwanza limekumbusha  kuwa roho za wenye haki ziko mikononi mwa Mungu, zipo katika amani isiyo yumba. Tumaini lao halikatishwi tamaa: halifi tena”(Sap.3,1-2). Kwa kuhitimisha amesema  wakamkabidhi sasa roho yake kwa Mungu na kumwombea marehemu huruma ya Mungu. Baadaye sala ambayo itaimbwa na Kwaya baada ya Baraka kwa  Jeneza na Baba Mtakatifu Francisko: “In paradisum deducant te Angeli, in tuo adventu suscipiant te martyres et perducant te in sanctam civitatem Jerusalem”.

Wasifu wa Kardinali Sodano

Kardinali Angelo Sodano, ameaga dunia  Ijumaa Jioni 27 Mei 2022  akiwa na umri wa miaka 94. Alikuwa ni Katibu wa Vatican wakati wa Upapa wa Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI na Dekano Mstaafu wa Baraza la Makardinali. Kardinali tang tarehe 9 Mei alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Columbus- Gemelli Roma kufuatia na kuambukizwa na Uviko. Kardinali alishika wadhifa wa Katibu wa Vatican kuanzia mwaka 1991 hadi 2006 na alikuwa Dekano wa Baraza la  Makardinali kuanzia mwaka 2005 hadi 2019.  Yeye ni Mtoto wa pili kati ya watoto sita, na  alizaliwa kisiwa cha Asti, Mkoa wa Piemonte  mnamo tarehe 13 Novemba 1927. Wazazi wake Giovanni na Delfina Sodano walikuwa familia ya vijiji vya Piemonte, familia ambayo ilitoa mchango mkubwa kwa maisha ya Kanisa na Serikali. Baba yake pia alikuwa mjumbe wa Bunge la Italia tangu 1948 hadi 1963, kwa mihula mitatu. Angelo akiwa kijana alimaliza masomo yake ya falsafa na taalimungu katika seminari ya kiaskofu ya Asti, lakini huko Roma ndipo alipata shahada yake ya mara mbili: ya taalimungu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana na katika sheria ya Kanoni katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano.

Mnamo tarehe 23 Septemba  1950 ni tarehe ya kupewa daraja la kikuhani, iliyopokelewa katika Kanisa Kuu la Asti. Mafundisho ya taalimungu ya kweli na utume kati ya vijana wanafunzi ni sifa ya miaka ya kwanza ya huduma yake. Tayari mnamo 1959 aliitwa na Kadinali Angelo dell'Acqua, wakati huo akiwa  Msaidizi  wa Sekretarieti Vatican, katika huduma ya Vatican. Alihudhuria kozi za Chuo cha Kipapa cha Kikanisa, na baadaye akatumwa kwenye Ofisi za Ubalozi wa Vatican huko Equador, Uruguay na Chile, kama katibu wa Ubalozi. Mnamo mwaka 1968 alirejea Roma ambako kwa muongo mmoja alihudumu katika Baraza la Masuala ya Umma kwa  Kanisa. Mjumbe wa Tume za Vatican kwa kutembelea  Nchi za Romania, Hungaria na Ujerumani Mashariki.

Tarehe 30 Novemba 1977, Mtakatifu Paulo VI alimteua kuwa askofu mkuu wa Nova ya  Cesare na Balozi wa Kitume nchini Chile. Wiki chache baadaye, tarehe 15 Januari 1978, alipata daraja la uaskofu katika mikono ya  Kardinali Antonio Samorè katika Kanisa la Mtakatifu Secondo, huko Asti. Katika nchi ya Amerika ya Kusini alifanya kazi kwa miaka kumi: alitembelea karibu majimbo yote na alishirikiana katika hitimisho la mafanikio la upatanishi wa kipapa kati ya Chile na Argentina. Mtakatifu Yohane Paulo II mwaka 1988 alimwita kuchukua nafasi ya Kardinali Achille Silvestini katika ofisi ya Katibu wa Vatican kwa ajili ya Mahusiano na Ushirikiano na Mataifa na kujikita wakati huo kwa namna ya pekee na Tume ya Kipapa ya Urussi, ambayo alikuwa rais wake.

Amewakilisha Vatican katika mikutano mbalimbali ya kimataifa kama vile mikutano ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Mkutano wa Usalama na Ushirikiano barani Ulaya(OSCE). Mnamo Desemba 1990 alishika wadhifa wa Katibu Msaidizi wa Vatican na kuwa Katibu wa Vatican mnamo tarehe 29 Juni 1991, siku moja baada ya kuundwa kuwa Kardinali. Mwaka 2002 alichaguliwa kuwa Makamu wa Baraza la Makadinali. Alishiriki katika mkutano wa mwaka 2005 ulioweza kumchagua Papa Mstaafu Benedikto XVI, ambaye, baada ya  kukaa kwenye kiti cha upapa, akamteua tena kuwa Katibu wa Vatican mnamo tarehe 30 Aprili 2005 na kuidhinisha kuchaguliwa kwake kama Dekano wa Baraza la Makardinali, nafasi aliyoshikilia hadi hapo wakati ambapo Joseph Ratzinger mwenyewe miezi michache baadaye Papa alikubali kujiuzulu kwake kutoka wadhifa wa Katibu wa Vatican. Alifuatiwa na Kardinali Tarcisio Bertone. Mnamo 2019 Papa Francisko alikubali maombi ya kung’atuka  kwake Sodano kutoka wadhifa wa  Dekano wa Baraza la  Makardinali. Hapo awali kwa kuteuliwa na Papa alishiriki mwaka 2014 katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu “Changamoto za kichungaji katika familia katika muktadha wa uinjilishaji” na mwaka mmoja baadaye katika Sinodi ya  XIV wenye kaulimbiu “Wito na utume wa familia katika Kanisa na katika ulimwengu wa sasa”.

Kwa kifo cha Kardinali Angelo Sodano, Baraza la makadinali linaundwa na makadinali 208 ambapo 117 ni wapiga kura na 91 sio wapiga kura.

31 May 2022, 15:52