Papa Francisko:Shukrani ya makaribisho nchini Kazakhstan
Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa Mahujaji na Waamini waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican,Dominika tarehe 18 Septemba 2022, amesema “Ninamshukuru Mungu kwa safari ambayo nimeitimiza hivi karibuni nchini Kazakhstan, katika fursa ya Kongamano la VII la Viongozi wa Dini Ulimwenguni na dini za Jadi na kwa maana hiyo ninapendekeza kuzungumza wakati wa katekesi ijayo.
Maskitiko ya Papa kwa ajili ya Azerbaigian na Armenia
Baba Mtakatifu akiendelea amekumbuka mapigano ya hivi karibuni kati ya nchi mbili Azerbaigian na Armenia. Kwa maana hiyo ameonesha uchungu na kuelezea ukaribu wake wa kiroho kwa familia za waathirika na kushauri sehemu zote mbili kuheshimu na kuacha mapigano hayo, katika matazamio ya makubaliano ya amani. Papa amesema “Tusisahau kwamba amani inawezakana zinaponyamaza silaha na kuanza mazungumzo”. Papa vile vile ameomba kuendelea kusali kwa ajili ya nchi ya Ukraine na kwa ajili ya amani ya kila nchi iliyomwagikiwa na damu kutokana na vita.
Mafuriko Mkoa wa Marche Italia
Baba Mtakatifu pia amependa kuwahakikishia sala zake watu wa Mkoa wa Marche, Italia walishambuliwa na mafuriko ya nguvu sana. Anasali kwa ajili ya marehemu, familia zao, waliojeruhiwa na wale wote waliopata hasara kubwa. “Bwana awajalie nguvu jumuiya hiyo”, amesema Papa.
Baada ya kusema hayo Papa amewasalimia waroma, mahujaji wa kutoka pande zote ambao walifika kwa wingi katika uwanja wa Mtakatifu Petro, kwa namna ya pekee watawa wa Maria Msafi wa Moyo na jumuiya mbali mbali za Afrika, Amerika Kusini, Asia na Ulaya na wengine wengi yakiwemo makundi ya kiparokia. Papa amesalimia hata vijana wa “Economy of Francesco”, yaani Uchumi wa Francisko, ambao walikuwa kwenye uwanja huo na kuwaleza kuwa waendelee mbele zaidi na wataonana muda si mrefu huko Assisi. Amehitimisha kwa kutakia Dominika Njema na kuwaomba wasisahau kusali kwa ajili yake.